Machi 19, 2020 ilikuwa ni siku ngumu mno kwa mashabiki wa muziki wa Lingala, hususan Soukous. Hiyo ilitokana na taarifa za kufariki kwa gwiji wa miondoko hiyo Aurlus Mabele.
Mabele aliyewahi kutamba na makundi mbalimbali ya muziki nchini Congo-Brazzaville alizaliwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wakati huo ikiitwa Zaire. Taarifa za kifo chake zilizotolewa usiku wa kuamkia Alhamisi ya Machi 19 kwamba amekumbwa na mauti jijini Paris nchini Ufaransa.
Sababu za kifo chake zilielezwa kuwa ni virusi vya Covid-19. Bintiye nyota huyo wa zamani wa kundi la Loketo Liza Monet ambaye pia ni mwanamuziki alithibitisha taarifa za kuondokewa na mzazi wake kupitia akaunti ya twitter. Pia mjomba wake Robert Mabele alithibitisha kupitia akaunti yake ya facebook kuwa mjomba wake amefariki dunia.
Kabla ya kukumbwa na mauti Mabele alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya muda mrefu yaliyomuweka kitandani ikiwamo saratani ya kooo miaka kadhaa nyuma sambamba na kupooza. Mashabiki, wapenzi na wasanii mbalimbali waliowahi kufanya kazi na mwimbaji huyo aliyekuwa mahiri pia kwa kutunga na kucheza walitoa salamu za rambirambi juu ya kifo chake. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 67.
Miaka michache iliyopita Mabele aliwahi kuhojiwa akiwa nchini Ufaransa alikopelekwa kwa matibabu na kueleza kuwa anaumizwa zaidi baada ya aliyekuwa mkewe kumtelekeza hospitalini.
Inadaiwa tatizo kubwa lililomsumbua mwanamuziki huyo mahiri ni maradhi ya kansa ya koo yaliyoelezwa kumfanya ashindwe kuzungumza vizuri. Kipindi akiendelea kujiuguza ilikuwa ni vigumu kujua Mabele amelazwa hopsitali gani kutokana na kuwapo kwa taarifa mbili tofauti moja ikielezwa yupo Visiwa vya West Indies huko Carribean na wengine wakidai kuwa yupo Ufaransa akiuguzwa na baadhi ya marafiki zake.
Rafiki zake hao walikuwa wakiendesha harambee kupitia mtoto wa mtayarishaji wake mahiri wa muziki Jimmy Houtienou na wakiendelea kuwaomba mashabiki waendelee kumwombea.
MABELE NI NANI?
Jina lake halisi ni Aurlien Miatsonama. Alizaliwa Oktoba 23, 1953. Mashabiki wa muziki wa Kikongo walimfahamu kupitia kundi la Loketo lililojumuisha magwiji na nyota mbalimbali wa muziki barani Afrika na hasa kutoka nchi za DRC na Kongo-Brazzaville.
Mabele alianza kufahamika tangu akiwa kwao Kongo-Brazzaville kupitia kundi la Ndimbola Lokole lililoasisiwa mwaka 1974 akiwa sambamba na kina Jean Baron, Pedro Wapechkado na wengine. Miaka michache baadaye walianzisha kundi la Loketo. Mtunzi na mwimbaji huyo aliyekuwa mahiri pia katika kunengua jukwaani alizaliwa katika Poto Poto, Kongo-Brazzaville.
Historia ya maisha yake ya utotoni haitwajwi sana. Lakini kama ilivyo kwa wanamuziki wengi alianza sanaa tangu akiwa mdogo kupitia makundi kadhaa mitaani yaliosaidia kumpata uzoefu. Ilielezwa kuwa kabla ya kugeukia utunzi na uimbaji wake, Mabele alikuwa akidansi , lakini kutokana na kipaji cha muziki alibadilisha upepo mapema.
Safari yake ya kimuziki ilianza rasmi mika ya 1970 alipoungana na wanamuziki Jean Baron, Pedro Wapechkado, May Cacharel na waasisi wengine wa kundi la Ndimbola Lokole mnamo mwaka 1974.
Kundi hilo lilijipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya Afrika na ziara za mara kwa mara barani Ulaya zilikuwa hazikauki. Jean Baron ambaye kwa sasa naye ni marehemu na Mabele waliungana na kutengeneza kundi la Loketo. Kundi hilo liliasisiwa mnamo mwaka 1987 na Mabele mwenyewe, Diblo Dibala, Jean Baron, May Cacharel baadaye waliungana na wakali wengine Fred Mayunga, Lucien Bokilo, Mack Makaire, Jean Bilongo, Komba Bello Mafwala na Awilo Longomba mbaye alikuwa mpiga tumba katika kundi hilo.
UFALME WA SOUKOUS
Uimbaji na ucheshi wake jukwaani sambamba na kipaji chake cha kuburudisha vilimfanya Mabele kupewa jina la Mfalme wa Soukous ambapo ilikuja kuzaa albamu yenye jina la kama hilo la King of Soukous (Soukous la Terreur iliyotoka kati ya mwaka 1989 na 1991).
Sura yake ilikuwa imejaa tabasamu muda wote ilimfanya Mabele awe kipenzi wa mashabiki wengi hasa wa kike, uvaaji wake ndio kabisa uliwafanya wengi wapagawe hata wasanii wengine kama King Kester Emeneya nao walijikuta wakianza kuiga uvaaji wake nadhifu.
Haikutosha uchezaji wake vilimtofautisha na wanamuziki wengine wa miaka hiyo. Nyimbo kama Asata de, Zebola, Ebouka, Wakawaka, Liste Rouge, Zenab, Mawa, Evelyne, Generation Wachiwa, Betty, Femme Ivoirienne, Rosine, Mali Bamako, Doce Isabelle, Keba, Soukous Trouble, Loketo, Khadydja, Rosa, Embargo, Stop Arretez na nyinginezo zilimbeba na kumtangaza duniani.
Ziara ndefu aliyoifanya na Loketo barani Ulaya ilimtangaza na wenzake hasa kupitia albamu ya Extra Ball na haikuwa ajabu baadhi yao kulowea barani humo. Mabele ni kina Diblo Dibala waliweka maskani yao nchini Ufaransa na wengine walikimbilia Ubelgiji na kuna wengine walienda kuweka makazi yao nchini Marekani.
Kutoka Soukous Stars wengine walijitoa kutoka humo na kuendelea na maisha yao miongoni mwao ni Yondo Sister, Shimita, Lokasa ya Mbongou na Ngouma Lokito.
Kuishi kwake Ufaransa kunaelezwa kuwa kulimsaidia kupata mtoto wa kike aliyetambuliwa zaidi na mashabiki wake Liza Monet aliyetoa taarifa ya kufariki dunia kwa baba yake. Binti huyo wa Mabele anaelezwa kujulikana zaidi kuliko watoto wengine wa Mabele ambao alijaliwa kuwa nao.
UTAJIRI WAKE KUPITIA MUZIKI
Inaelezwa kuwa kwa miaka zaidi ya 25 ya kuwapo kwenye medani ya muziki, Mabele aliuza zaidi ya nakala milioni 10 na kuvuna pesa za kutosha zilizomfanya aishi kitajiri.
Watayarishaji wakubwa wa muziki aliofanya nao kazi na kumtengenezea njia ya kuvuna pesa kupitia albamu na nyimbo zake ni pamoja na Jimmy Houtienou kupitia Jimmy's Production, Afro Rythmes, JPS, Jip Records nawengine.
Ukiacha albamu ya Soukous la Terreur, albamu ya Stop Arretez ndiyo iliyompa fedha nyingi zaidi ikifuatiwa na ile ya Toure de Controle. Baadhi ya albamu zilizomtangaza Mabele ni pamoja na na albamukama Soukous la Terreur (1991), Stop Arretez (1993), Tour de Controle (1999), Dossier X (2000), na Fiesta d'Or aliyoifyatua mwaka 2002.
SINTOFAHAMU NA DIBLO DIBALA
Licha ya kupata mafanikio makubwa wakiwa pamoja na Diblo Dibala, Mabele alitofautiana na mwenzake huyo huyo na Diblo aliamua kutengana ndani ya muda mfupi mwishoni mwa miaka 1990 japokuwa baadaye walikuja kushirikiana tena kufanya kazi binafsi.
Inadaiwa Diblo Dibala hakupendezwa na tabia ya kutembea na wanenguaji wao kwani ilifikia hatua ya kuwapa nafasi kundini kiasi ch akuwashirikisha kuimba nyimbo zao.
Tangulia Mabele......Tangulia gwiji wa miondoko ya Soukous...Tangulia baba.
STORY & CONTRIBUTION: Mwananchi Communication Ltd & Jabir Johnson
EMAIL: jabirjohnson2020@gmail.com
DATE: Machi 21, 2020
0 Comments:
Post a Comment