Shirika la lisilo la Kiserikali la Utafiti Twaweza
limesema tangu serikali ianzishe zoezi la usajili wa laini za simu, uhuru wa
maoni kwa njia ya simu kwa alama za vidole umepungua tofauti na hapo awali.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Idhaa ya
Kiswahili ya DW, Mkurugenzi wa shirika hilo Aidan Eyakuze alisema uwazi katika
utoaji wa maoni kwa njia ya simu umepungua baada ya serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuanza zoezi la usajili wa laini kwa alama za vidole mnamo
mwaka 2019.
Eyakuze alisema hapo awali walipokuwa wakifanya
utafiti wa masuala mbalimbali yakiwamo ya kisiasa nchini miongoni mwa njia
ambazo walikuwa wakitumia ni kuwapigia simu wananchi na kutaka maoni yao
walikuwa wakifunguka bila hofu lakini hali imekuwa tofauti na ilivyo sasa
ambapo wengi wamekuwa wakihofia usalama wao baada ya utoaji wa maoni yao kwa
njia hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema utafiti kwa njia hiyo umekuwa
mgumu kwani wengi wamekuwa waoga wakihofia kukamatwa na vyombo vya usalama hasa
ukizingatia sheria nyingi zilizopo nchini tangu mwaka 2015 zimekuwa kikwazo cha
utoaji huo wa maoni akitaja Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya
Takwimu, Sheria ya Makosa Mtandaoni.
Alipoulizwa kuhusu hatima ya taasisi yake Eyakuze
alisema bado wanaendelea kufanya kazi yao kama walivyojiwekea malengo yao tangu
kuanzishwa kwake miaka 10 iliyopita na kwamba kwa sasa wamepanua wigo wa
kufanya utafiti wao wakizifikia Kenya na Uganda.
Hata hivyo Eyakuze alisema Twaweza imekuwa ikikusanya
maoni katika medani zote huku medani ya siasa ikifuatiliwa kwa karibu na wadau
mbalimbali wakiwamo waandishi wa habari, lakini kutokana na hali ya kisiasa
nchini medani hiyo imekuwa ngumu kuifanya kutokana na sheria zilizopo.
Aidha Eyakuze aliweka bayana kuhusu hatima ya pasi
yake ya kusafiria (Passport) ambayo bado imeshikiliwa na mamlaka husika tangu
mwaka 2018 hadi sasa kwamba bado anasubiri mamlaka hizo zitasema nini kuhusu
yeye.
Idara ya Uhamiaji ilikaririwa mnamo mwaka 2018 kuwa ni
utaratibu wa kawaida mtu anapotuhumiwa kuwa sio raia wa Tanzania, Idara hiyo
huzuia 'passport' kwakuwa ni mali ya Rais kwa maana hiyo 'passport' ni mali ya
serikali, na wakikamilisha uchunguzi basi taratibu nyingine hufuata.
0 Comments:
Post a Comment