Makala ya leo itajikita katika medani ya michezo hususani
soka la Tanzania mnamo mwaka 1965 pale YANGA ilipojitoa katika mashindano ya
Klabu Bingwa na kuipa SIMBA SC rekodi ya kwanza kutwaa taji hilo na kuifanya
SIMBA SC kuwa klabu ya kwanza kutwaa taji kubwa nchini Tanzania.
Historia ya Ligi kuu ilianza rasmi kuwekwa kumbukumbu
msimu wa mwaka 1977/78. Hii haina maana kwamba kabla ya hapo hapakuwepo na
mashindano ya soka wa vilabu.
Mashindano yalikuwepo na vilabu vingi vya kandanda
vilikuwa ni vya sehemu za kazi zaidi isipokuwa vichache sana.
Wazo la kuanzisha Ligi Tanzania Bara kwa timu za
vilabu lilianza mnamo mwaka 1965 wakati huo Tanzania Bara ilipompata mwalimu wa
soka kutoka nchini Yugoslavia ya zamani.
Mwalimu huyo aliiitwa Milan Celebec ambaye alishauri
kuwepo na mashindao ya kutafuta klabu bingwa taifa na miongoni mwa sababu alizozitoa
ni kwamba mashindano hayo yangetoa fursa kwa chama cha soka nchini wakati huo
FAT na yeye mwenyewe kuwapata wachezaji wazuri zaidi ambao watakuwa wamepata
mazoezi ya muda mrefu zaidi katika kujianda kwa mashindano ya vilabu kabla ya
kujiunga na timu ya taifa.
FAT ikakubali wazo lake na kuanza kuyaendesha
mashindano ya kutafuta klabu bingwa wa taifa kwa mwaka 1965 na kwa kuanza mashindano
hayo yalishirikisha timu sita zilizoteuliwa na FAT ambazo ni; T.P.C Moshi,
Tumbaku (TCC) Dar es Salaam, Yanga, Simba (zamani Sunderland), Coastal Union ya
Tanga na Manchester United ya Tanga.
Mashindano hayo yalifanyika katika viwanja vya Ilala
sasa Karume na Manispaa ya Tanga sasa Mkwakwani. Kitu kimoja kilichojitokeza
katika mashindano hayo ya kwanza ilikuwa ni kwamba viongozi wa FAT, viongozi wa
vilabu vyote vilivyoshirikishwa na wachezaji wenyewe hawakuzielewa vizuri
sheria na kanuni za mashindano na hata ujuzi wao wa kuzielewa sheria za mchezo
wenyewe wa soka ulikuwa duni.
Katika kudhihirisha hilo klabu ya Yanga ilijitoa katika
mashindano ya kwanza ya kutafuta klabu bingwa Tanzania Bara na ubingwa ukaenda
kwa hasimu wake na mtani wa jadi Simba SC. Hivyo kwa takwimu hizo Simba SC ndio
timu ya kwanza nchini (Tanzania Bara) kutwaa ubingwa wa vilabu.
Madhumuni ya mashindano hayo ilikuwa ni kumpata mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya Kombe la Klabu Bingwa wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Timu mbili za daraja la kwanza (sasa ligi kuu) yaani
mshindi wa kwanza na mshindi wa pili wa Tanzania Bara ziliungana na timu mbili
kutoka Zanzibar kuingia katika michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania nzima ambayo
nayo ilikuwa ikichezwa katika mfumo wa nyumbani na ugenini ili kumpata mshindi
wa kwanza na wa pili.
0 Comments:
Post a Comment