Ujenzi wa Ukuta wa Berlin ni moja ya matukio makubwa katika karne ya 20. Ukuta huo ulivunjwa mnamo Novemba 9, 1989.
Usiku wa Agosti 12 kwenda 13 mwaka 1961 wanajeshi na polisi elfu kadhaa walitumwa kusimama mpakani mjini Berlin walipoangalia wafanyakazi walioanza kujenga ukuta na kufunga mpaka ndani ya jiji.
Madirisha na milango ya nyumba zilizokaa mpakani moja kwa moja yalifungwa pia na wakazi walipaswa kutumia milango ya nyuma. Usafiri kwa mabasi na treni kati ya pande mbili za jiji ukasimamishwa vilevile.
Ukuta wa Berlin ulitenganisha sehemu mbili za jiji la Berlin. Ukuta huo ulikuwa na urefu wa kilomita 45.3 ukiwa sehemu ya mpaka kati ya madola mawili ya Ujerumani yaliyokuwepo kuanzia 1949 hadi 1990.
Ukuta wa Berlin ulikuwa mfano uliojulikana zaidi wa "Pazia la Chuma"
katika Ulaya lililotenganisha nchi za Kikomunisti za Ulaya Mashariki na nchi za
Ulaya Magharibi. Takriban watu 200 waliuawa walipojaribu kuvuka ukuta kutoka
mashariki kwenda magharibi.
Chanzo
cha ukuta kilikuwa ugawanywaji wa jiji la Berlin baada ya Vita Kuu ya Pili ya
Dunia tangu 1945. Nchi washindi ziliamua kuigawa Ujerumani yote. Wakaanzisha
kanda nne zilizotawaliwa na Umoja wa Kisovyeti, Marekani, Uingereza na
Ufaransa.
Jiji
la Berlin lilikuwa ndani ya kanda ya Kisovyeti lakini likiwa mji mkuu wa
Ujerumani, lilitangazwa kuwa mkoa wa pekee likigawanywa pia katika kanda nne za
washindi. Mashariki ya Berlin ilikuwa sehemu ya nchi ya kikomunisti Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Ujerumani na magharibi ya jiji ilikuwa chini ya mamlaka ya
Marekani, Uingereza na Ufaransa.
Tangu
mwaka 1946 washindi walianza kutoelewana, na kipindi cha vita baridi kilianza
ambako nchi za magharibi (Marekani, Uingereza, Ufaransa) zilisimama dhidi ya
nchi za mashariki zilizoongozwa na Umoja wa Kisovyeti.
Migongano
ya kimasilahi ya pande hizi mbili ilisababisha kutokea kwa madola mawili ndani
ya Ujerumani, moja chini ya uangalizi wa nchi za magharibi (Shirikisho la
Jamhuri ya Ujerumani) na nyingine chini ya usimamizi wa Kisovyeti (Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kijerumani).
Berlin
ya Mashariki iliunganishwa na Ujerumani ya Mashariki ikawa mji mkuu wake.
Berlin ya Magharibi iliendelea kama mkoa wa pekee chini ya usimamizi wa nchi
washindi wa vita ikawa kama kisiwa ndani ya Ujerumani ya Mashariki.
Mnamo
mwaka mwaka 1948/49 Wasovyeti walijaribu kuondoa nchi za magharibi katika
Berlin kwa kuzuia umeme, maji na usafirishaji wa vyakula na bidhaa kwa jumla
kuingia Berlin Magharibi. Nchi za magharibi walilisha wakazi wa mji kwa njia ya
ndege ("Daraja la Angani") hadi Wasovyeti walipoondoa vizuizi.
Mwaka
1961 serikali ya Mashariki iliona ni lazima kuzuia wakimbizi wengi kwenda
Berlin Magharibi. Hapo walikata shauri la kutenganisha sehemu mbili za jiji kwa
njia ya ukuta na fensi. Walipata kibali cha uongozi wa Umoja wa Kisovyeti
wakaandaa akiba za matofali, saruji na waya ya miiba.
Ukuta uliendelea kujengwa hata sehemu za nje ya Berlin ya Magharibi ambako jiji linakutana na mashamba ama kwa kujenga uzio mkubwa au ukuta pia. Tangu kuanzishwa mwaka 1961 hadi mwisho wake mwaka 1989 ukuta uliendelea kuboreshwa na kupanuliwa. Nyumba zilizosimama zikabomolewa polepole na wakazi wakahamishwa.
0 Comments:
Post a Comment