Kagame alizaliwa katika familia ya Kitutsi Kusini
mwa Rwanda Oktoba 23, 1957. Alipokuwa na miaka miwili, mapinduzi ya Rwanda
yalihitimisha udhibiti wa kisiasa wa Watutsi uliyodumu kwa karne kadhaa,
familia yake ilikimbilia nchini Uganda alikoishi utoto wake wote.
Katika miaka ya 1980 Kagame alipigana katika
jeshi la uasi la Yoweri Kaguta Museveni, na kuwa afisa wa juu wa jeshi baada ya
ushindi wa kijeshi wa Museveni kumwingiza madarakani.
Kagame alijiunga na kundi la "Rwandan
Patriotic Front" RPF, lililoivamia Rwanda mwaka 1990, kiongozi wake Fred
Rwigyema aliuawa mapema katika vita na Kagame akakalia kiti.
Kufikia mwaka 1993, RPF ilikuwa inadhibiti sehemu
kubwa ya ardhi ya Rwanda na makubaliano ya kusitisha mapigano yakasainiwa.
Mauaji ya rais wa Rwanda Juvenal Habyariman yalisababisha mauaji ya kimbari
ambamo watu 800,000 waliuawa.
Kagame alianzisha tena vita vilivyokomesha mauaji
hayo na kuishia kwenye ushindi wa kijeshi. Pia alifanikiwa jaribio la kubadili
katiba ya taifa hilo ambayo itamruhusu kuendelea kutawala baada ya kumaliza
muhula wake wa sasa mwaka 2017, na huenda akaitawala nchi hiyo hadi akiwa na
umri wa miaka 77 mnamo mwaka 2034.
YOWERI KAGUTA MUSEVENI
Rais Yoweri Museveni ameongoza Uganda kwa miongo
mitatu sasa, baada ya kuchukua uongozi akiwa kiongozi wa kundi la waasi.
Katiba, iliyokuwa imeweka kikomo kwenye muhula wa
rais, ilifanyiwa marekebisho kumruhusu kuwania urais mwaka 2006 na baadaye
akashinda tena uchaguzi Februari 2011.
Katika uchaguzi wa 2011, alipata asilimia 68 ya
kura dhidi ya mpinzani wake mkuu Kizza Besigye aliyepata asilimia 26. Besigye
alipinga matokeo hayo akisema kulikuwa na udanganyifu.
Umoja wa Ulaya ulisema mfumo wa uchaguzi ulikuwa
umeimarika ikilinganishwa na 2006, licha ya kuwapo kasoro nyingi.
Museveni amekuwa akisifiwa kwa kuhakikisha
uthabiti kisiasa pamoja na ukuaji wa uchumi Uganda baada ya miaka mingi ya vita
vya wenyewe kwa wenyewe na ukandamizaji wa wapinzani chini ya watangulizi wake
Milton Obote na Idi Amin.
Museveni alikuwa mmoja wa waasisi wa kundi
mojawapo la waasi lililosaidiana na wanajeshi wa Tanzania kumuondoa mamlakani Nduli
Idi Amin mnamo mwaka 1979. Baadaye aliunda jeshi jipya la waasi ambalo
lilifanikiwa kutwaa uongozi wa taifa hilo mnamo mwaka 1986.
Chama chake cha National Resistance Movement
(NRM) kilitawala Uganda kama taifa la chama kimoja hadi pale kura ya maamuzi
ilipofanyika 2005 na mfumo wa siasa za vyama vingi ukarejeshwa.
Museveni alishinda uchaguzi wa urais 1996, 2001,
2006 na 2011.
Pia amekuwa akishutumiwa na Umoja wa Mataifa kwa
mchango wake katika vita Jamhuri ya Kimeokrasi ya Kongo (DRC) kati ya 1998 na
2003 pia miaka ya karibuni alituhumiwa kuunga mkono makundi ya waasi huko.
Museveni alizaliwa Magharibi mwa Uganda mnamo mwaka
1944, akasomea Sayansi ya Siasa nchini Tanzania na alipigana pamoja na
wapiganaji wa Front for the Liberation of Mozambique (FRELIMO), ambapo huko alipata
ujuzi wa vita vya msituni, kisha akarudi nchini mwake kuendeleza mapambano.
Katika makala haya tutaangazia wawili hawa
kutokana na kuwa na vita baridi, nini chanzo cha hayo yote wakati walikuwa ni
watu waliosaidiana katika kuingia madarakani.
Historia yao inaanzia mbali, Kagame aliingia
nchini Uganda baada ya kukimbilia uhamishoni nchini humo wakati kundi la
Watutsi nchini Rwanda mnamo mwaka 1959 kusakwa kwa udi na uvumba. Utawala wa
Obote, Idi Amin na Tito Okello uliokuwa wa mabavu usiowajali watu wa Uganda
ndio ulimkutanisha na Museveni.
Alikuwa ni Kagame na Rwigyema wote kutoka Rwanda
walioongoza mapambano ya kumwingiza Museveni madarakani walipolikamata jiji la
Kampala mnamo mwaka 1986.
Japokuwa Kagame aliteuliwa kuwa mkuu wa usalama
wa taifa hilo bado wazo la kurudi nyumbani lilisalia katika kichwa chake akiwa
na Rwigyema walikuwa na shauku ya kurudi kuuondoa utawala wa Juvénal
Habyarimana ambao ulikuwa ukizidisha ukabila.
Kagame taratibu alianza kuvunja muungano wake na
Museveni kisha kusalia kuwa maadui kwa mbali, marafiki kwa wakati huo huo
(frenemies). Majeshi ya Uganda mikononi mwa Museveni yalitoa msaada ambao
ulikuwa na maana kubwa sana kwa Kagame kwani yalikwenda na kuushikilia jiji la
Kigali ambalo hatimaye liliangukia katika mauaji ya kimbari mnamo mwaka 1994.
Kampeni ya vita vya msituni iliyokuwa ikiendeshwa
na Museveni wakati Kagame alipokuwa akihudumu nao nchini Uganda yalionyesha
mwelekeo kwa RPF.
Kupinga vitendo vya rushwa, kuunda upya uchumi wa
taifa kwa soko huru na kuvutia wawekezaji viliongeza mvuto wa watu na matumaini
makubwa kwa RPF.
Uhasama ulianza kujitokeza taratibu pale majeshi
ya Kagame na Museveni yalipoanza kampeni za kutaka kuupindua utawala wa Mobutu
Sese Seko nchini DRC.
Awali walisaidia pakubwa kumweka madarakani
Laurent-Desire Kabila lakini kutoelewa katika mikakati ya kijeshi baada ya
kuupindua utawala wa Mobutu ulianza kuota mizizi.
Vita ya Kisangani yalipo machimbo ya Almasi
katika mto Congo yaliwaachanisha Kagame na Museveni. Wawili hawa walitofautiana
katika mgawanyo wa mali baada yao na wapiganaji wa Kongo. Mgawanyo huo ulionekana dhahiri pale majeshi
ya Uganda yalipowasaliti wale wa Kagame. Chanzo kimoja kilisema kwamba wawili
hao waliachana kutokana na kwamba Museveni alipoteza uaminifu wake kwa Kagame
na kwamba alishindwa kumheshimu na kumuona kama mtu asiye na kwao. (Museveni
had failed to treat him with respect).
TUCHIMBE KWA UNDANI
Itakumbukwa kwamba wakati wa vita nchini Uganda
katika ukanda wa kati wa Luweero Triangle
watu wanaokadiriwa laki tano (500,000) walipoteza maisha.
Majeshi ya Museveni yalikuwa yakiwatumia
wakimbizi wa Rwanda walioingia nchini humo baada ya ukosefu wa utulivu nchini
mwao. Watu hao wa Uganda walijikuta wakishindwa kufanya uzalishaji kutokana
mapigano kushamiri.
Hapo ndipo chanzo cha Jeshi la Wananchi wa Uganda
(UPDF) lilipopata nguvu na uzoefu wa kutosha na kuongeza nguvu zaidi lilikwenda
nchini Rwanda.
Haikustaajabisha wakati Museveni alipokuwa
akiingia madarakani mnamo mwaka 1986 idadi kubwa ya maofisa wa kijeshi katika
utawala wake walikuwa ni Wanyarwanda. Miongoni mwao ni Meja Jenerali Fred
Rwigyema, Mkuu wa Usalama wa Taifa Paul Kagame, Meja Dkt. Peter Baingana
alikuwa katika kitengo cha huduma za afya za Kijeshi. Pia Col. Chris Bunyenyezi
alikuwa field Kamanda, Meja Frank Munyaneza, alikuwa mobile brigade Kamanda.
Maelfu ya Wanyarwanda waliajiriwa katika jeshi la Uganda (UPDF).
Kagame na wakimbizi wenzake wakiwa ndani ya UPDF
walitaka kutimiza azma yao ya kuiteka Kigali
na wakafanikiwa pale walipovamia taifa hilo mnamo Oktoba 1990.
Kutokubaliana kati ya Jeshi la Wazalendo wa
Rwanda (RPA) na makamanda wa juu kuhusu mpango wa kuiteka Rwanda kulisababisha
Meja Jenerali Rwigyema kuuawa katika siku ya kwanza ya uvamizi huo.
Meja Jenerali Rwigyema aliuawa na snipper ili
asiharibu mipango hiyo na inaelezwa kwamba mwili wake ulizikwa kwa siri katika
mpaka wa Uganda na Rwanda.
Meja Jenerali Rwigyema alikuwa akitaka vita ya
msituni kama ilivyokuwa kwa Museveni nchini Uganda mnamo mwaka 1981, hoja
ambayo ilipingwa na makamanda wenzake ambao waliona uimara wa Rais Habyarimana
usingetakiwa kuingia msituni bali moja kwa moja Kigali kuteka ikulu.
Mpango kazi huo uliwagharimu mno maisha yao kwani
maofisa wakubwa wa jeshi wakiwamo Baingana, Bunyenyezi, Munyaneza walipoteza
maisha katika mwezi wa kwanza wa uvamizi huo. Kikosi hicho cha Kagame
kilijikuta kikisonga mbele bila makamanda hivyo wakarudi kupiga magoti nchini
Uganda kwa Museveni.
Wachambuzi mbalimbali wanasema Meje Generali
Rwigyema alikuwa na mkakati mkubwa ambao ungewawezesha kufanya vizuri katika
kuuondoa utawala wa Habyarimana.
Wakati mapambano yakiendelea Meja Paul Kagame
alikuwa nchini Marekani ambako alikuwa
amepelekwa na UPDF kwa mafunzo zaidi. Ilikuwa ikieleweka kwamba Kagame alikuwa
akiunga mkono mkakati wa Rwigyema.
Baada ya taarifa za kifo chake na maofisa wengine
wa juu wa RPF kilimfanya Kagame asitishe mkakati wa kuipindua Kigali na kurudi
msituni kutengeneza jeshi ambalo ndilo lililoleta kile kinachofamika kama
Mauaji ya Kimbari 1994 yaliyotekelezwa na majeshi ya Habyarimana.
Watutsi wapatao 800,000 walpoteza maisha na
wachache walikuwa Wahutu baada ya kifo cha Habyarimana aliyefariki kwa ajali ya
ndege wakati akirudi kutoka Tanzania alikuwapo kwa ajili ya mazungumzo ya
amani.
Inaaminika kwamba kuangushwa kwa ndege hiyo
kulifanywa na missile iliyotupwa na majeshi ya ukombozi ya Kagame. Inasemekana
kwamba mauaji hayo yalifanywa ili kumwingiza madarakani Paul Kagame.
KILA MMOJA ALIKUWA NA NDOTO
Museveni na Kagame wote wawili walikuwa na ndoto
ya kutaka kuwa viongozi wa mataifa hayo. Vita baridi baina ya mataifa hayo
kuhusu vikwazo vya kiuchumi ni mwendelezo wa kuhofia siasa na usalama wao
katika siasa.
Kuna wakati utakumbuka majeshi ya mataifa haya
mawili yalipigana katika ardhi ya DRC bila kuonyesha kuhusika kwa mataifa haya.
Mataifa haya yanakiri kuwa yamekuwa yakipeleka majeshi yao Mashariki mwa taifa
la DRC.
Wakati Rwanda wakiendeleza harakati la kulimaliza
kundi la Habyarimana la Wahutu wa Interahamwe, Uganda nako wamekuwa
wakiendeleza juhudi zao za kulifuta kundi la waasi Allied Democratic Forces
(ADF), ambalo limekuwa na wapiganaji wengi wa Kiislamu ambao wanataka kuifanya
Uganda ya Kiislamu ambayo itaongozwa na sharia za Kiislamu.
Mji wa Kisangani ambao ni wa tatu kwa ukubwa
nchini DRC umekuwa kitovu cha majeshi hayo, kutokana na uwepo wa Uwanja wa
Ndege, pia amadini kama dhahabu, coltan na almasi na mataifa hayo yakitokwa na
udenda wa utajiri huo katika ardhi ya DRC.
Miongo kadhaa sasa ya migongano nchini DRC utabe
baina ya Kampala na Kigali bado haujafikia kikomo licha ya juhudi za
kidiplomasia kuendelea kufanyika na kila upande ukiona kuwa uko sahihi.
Lawama hizo zimekuwa zikienda mbali zaidi ya hapo
ambapo mwaka 2019 vyombo vya habari nchini Rwanda navyo vikiingia katika mtafaruku
huo ambapo viliinyooshea kidole cha lawama Uganda kuwa imewakamata wanahabari
wa Rwanda katika kituo cha Polisi cha Nalufenya katika mji wa kusini wa viwanda
wa Jinja pia mjini humo bila kificho kuna watu wengine wenye vyeo vya juu wa
Rwanda wamezuiliwa.
Taarifa hiyo ilitolewa maelezo na Museveni wakati alipokuwa akifanya uzinduzi mmoja huko
Rwakitura magharibi mwa Uganda ambako alitangaza kuwasamehe waandishi hao wa habari.
Raia wengi wa Uganda na Wanyarwanda ni jamii ya
watu ambao huwezi kuwatenganisha nchini Uganda.
Kwa upande mwingine Wanyarwanda nao, Uganda ni nyumbani.
Hiyo inatokana na wazazi wao kuzaliwa katika
ardhi ya pande hizo mbili. Mwanahabari mmoja mkongwe nchini Uganda aliwahi
kukaririwa akisema hakuna uhusiano mbaya baina ya watu wa Uganda na
Wanyarwanda. Tatizo lipo kwa Museveni na Kagame kutokana ubinafsi wao.
Wakati Museveni akijipona kuwa yeye ni mwamba wa
ukanda huo, Kagame anataka Museveni atambue kwamba yeye ni Rais wa taifa huru
lenye mamlaka yake.
0 Comments:
Post a Comment