Suala la Mkwawa kuwa mtoto au mjukuu lilichambulia
vizuri katika makala ya mwanahistoria wa Tanzania @Daniel Mbega mnamo mwaka
2012. Mwanahistoria huyo alifanya utafiti wa mambo mbalimbali kuhusu kabila la
Wahehe na mwanzo wa utawala wa Chifu Mkwawa katika ardhi hiyo.
MWANZO WA MUNYIGUMBA
Chifu Munyigumba Kilonge
Mwamuyinga ulidumu kwa muda wa miaka 19 tangu alipomuua kaka yake
Ngawonalupembe mwaka 1860.
Mtwa Munyigumba alifariki mwaka 1879 katika Kijiji cha
Lungemba akiwa amefanikiwa kuziunganisha koo zaidi ya 100 ambazo baadaye ndizo
zilizozaa kabila la Wahehe, wakati Munyigumba anafariki, Mtwa Mkwawa, ambaye ni
mtoto wake wa kwanza, alikuwa na umri wa miaka 24.
Kutokana na umri mdogo wa Mkwawa, ikabidi asikabidhiwe
kwanza uchifu kwa wakati huo, hivyo ukoo ukamteua mdogo wake Munyigumba, Mtwa
Mhalwike, aliyezaliwa na mke wa tatu wa Mtwa Kilonge, Mama Sekindole.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya Mtwa Munyigumba
kufariki na kutawazwa kwa Mhalwike, utawala huo ukapinduliwa na mmoja wa
wafuasi wake na pia mkwewe aliyekuwa amemuoa binti yake. Mtu huyo, Mwamubambe
Mwalunyungu, alikuwa anatokea eneo la Wassa na enzi za utawala wa Munyigumba
ndiye hasa aliyekuwa kitumwa kazi ndogo ndogo kiasi cha kupendwa na hatimaye
akapewa binti wa Chifu.
“Huyu Mwamubambe kwa nini mdogo wake Munyigumba
atawale? Nchi hii nitaichukua mimi mwenyewe,” alisimulia Malugala Mwamuyinga,
mjukuu wa Msengele Kilekamagana, ambaye ni mdogo wake Mkwawa.
Mwamuyinga alisema, Mwamubambe alimvizia Mhalwike
kichakani, akampiga na kumchinja katika eneo hilo la Lungemba. Alipomaliza kazi
yake hiyo haramu akaenda mahali ambako watu walikuwa wanakunywa pombe na
kusema: “Nchi hii ni yangu. Kama mnabisha nendeni kule kwenye miti mkamtazame
Mhalwike.” Walipokwenda huko wakakuta maiti ya Mhalwike ikiwa imechinjwa kama
kuku.
Wakati huo Mtwa Mkwawa alikuwa bado mdogo sana kupewa
madaraka na kwa vile tayari Mwamubambe alikuwa ameupindua utawala, wakahisi
Mtwa Mkwawa angeweza kuuawa kwa sababu ndiye mtoto mkubwa wa Munyigumba na
ndiye hasa aliyetarajiwa kutawala. Hivyo, ikabidi wamkimbize kwenda kumficha
Dodoma kwa Mtemi Mazengo wa Wagogo. Hii ndiyo sababu Wagogo wanawaita Wahehe
wajomba zao na wanaheshimiana mno.
MAPAMBANO YA MKWAWA
Wahehe hawakufurahishwa na
utawala wa Mwamubambe anayechukuliwa kama adui mkubwa zaidi katika historia ya
kabila hilo kuliko hata Wajerumani. Kwa hiyo basi, wakapanga mbinu za siri
kumrejesha Mtwa Mkwawa kutoka uhamishoni.
Mtwa Mkwawa, wakati huo akiwa amejifunza mbinu za juu
za kivita, akaamua kurejea na kuunda jeshi lake ili kupambana na Mwamubambe.
Hata hivyo, wapiganaji wengi wa Mtwa Mkwawa aliuawa na
Mwamubambe, mtu ambaye anadaiwa kuwa alikuwa akitumia zaidi mitishamba kushinda
vita nyingi kwa sababu hata dawa alizokuwa anatumia ndizo zilizokuwa zikitumiwa
na Mtwa Munyigumba, huku Mwamubambe mwenyewe ndiye akielekezwa kuzitafuta
porini.
Kutokana na wapiganaji wengi kuuawa na Mwamubambe,
wapiganaji wengine walikuwa wakilia na kupiga kelele; “Hee Hee Hee! Mtwa
tuisila!” wakimaanisha; “Hee Hee Hee! Mtwa tunakwisha!” Hapa hasa ndipo
lilipoanza jina la kabila la Wahehe kutokana na kelele walizokuwa wakizipiga.
“Wafuasi wake walikuwa wanakufa sana. Siku moja Mkwawa
akajiwa kwenye ndoto na baba yake Munyigumba ambaye alimwambia kwamba hilo jitu
hawataliweza. Lilikuwa likichomwa mikuki linachomoa na kuwarushia wao na
kuwaua,” anasema Malugala Mwamuyinga.
Inaelezwa kwamba, Munyigumba alipomtokea Mkwawa kwenye
ndoto akamwambia, roho ya Mwamubambe iko kwenye kidole au kwenye kisigino. Hata
wakifanya namna gani hawawezi kumuua. Hivyo akamtaka amtafute Mkimayena
Mwakinyaga amwambie akamchome Mwamubambe kwenye kisigino au kidole.
Mwamubambe alikuwa na jeshi kubwa na wafuasi wengi
wenye uwezo wa vita, Mtwa Mkwawa akalazimika kujipanga upya ili kuwapiga na
kuyarejesha maeneo yote yaliyokuwa yametwaliwa na Mwamubambe.
Mapambano makali kabisa ya Mkwawa na wafuasi ya
Mwamubambe yaliianzia eneo ambalo leo hii linafahamika kama Lundamatwe (Lundika
Vichwa), lakini yapata kilometa mbili kutoka Barabara Kuu ya Tanzam upande wa
kusini.
Hapa palikuwa nyumbani kwa mganga Ngondo Kimamula
Mbugi, pembezoni mwa Mto Ruaha. Inaelezwa kwamba, mganga huyo aliamua kuchukua
jukumu la kuwaandaa wapiganaji wa Mkwawa kukabiliana na maadui zake.
Wapiganaji wa Mkwawa baada ya kuganguliwa wakaondoka
kupambana na Mwamubambe na wafuasi wake ambapo waliwapiga na kuwaua zaidi ya
wapiganaji 1,000.
Mwamubambe alipona mambo yamemzidia akatimua mbio,
lakini wapiganaji wa Mkwawa wakaanza kumfukuza.
Kwa vile Mkwawa alikuwa ameelekezwa na baba yake
ndotoni kuhusiana na Mwamubambe, akaamua kumtuma Mukimayena Mwakinyaga, ambaye
alikuwa mganga wa kienyeji, ili akamuue.
Mwakinyaga akaenda na kumkuta Mwamubambe anakunywa
pombe. Mbele ya umati wa watu, akamchoma mkuki kwenye kidole. Mwamubambe
akadondoka chini na kuanza kutapatapa bila kukata roho.
“Mwamubambe akamuuliza Mwakinyaga, ‘Umenifanya nini?’
Mwakinyaga akasema, ‘Aah ni mikuki tu’. Basi alipoona mambo yamekuwa magumu,
akamwambia; ‘Kaniitie Mkwawa aje’. Mkwawa alipofika Mwamubambe akamwambia;
‘Wakorofi kama mimi wapo wengi ndani ya utawala wako, kwa hiyo sasa ukazane’.
“Kwenye ndoto, baba yake alikuwa amemwambia Mkwawa
kwamba akishafika aukite mkuki wake chini. Basi Mkwawa akaukita mkuki chini.
Ndipo Mwamubambe akakata roho,” anaeleza Mwamuyinga.
Mwamuyinga anasema kwamba, kwa vile Mwamubambe alikuwa
amewatesa na kuwaua Wahehe wengi, baada ya kufa ikabidi, kwa hasira, wananchi
wale wamkatekate vipande vipande na kuila nyama yake ili lisiwepo kabisa
kumbukumbu lake.
0 Comments:
Post a Comment