Thursday, July 9, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Zachary Taylor ni nani?

Julai 9, 1850 alifariki dunia mwanasiasa wa Marekani Zachary Taylor. Huyu alikuwa Rais wa 12 wa taifa hilo. Alikuwa akifahamika zaidi kwa jina la utani kama ‘Old Rough and Ready’. Alihudumu katika nafasi hiyo kutoka Machi 4, 1849 – Julai 9, 1850. Alifariki dunia katika jengo la Ikulu ya White House jijini Washington D.C Alizaliwa Novemba 24, 1784 huko Barboursville, Virginia.

Kabla hajaingia katika nafasi hiyo alikuwa jeshini akifikia kuwa na cheo cha Meja Jenerali na alikuwa miongoni mwa mashujaa wa taifa hilo kutokana na ushindi walioupata katika vita vyao dhidi ya Wamexico vilivyodumu kwa miaka miwli kutoka mwaka 1846 hadi 1848.

Julai 4, 1850 Taylor alikula kiasi kikubwa cha matunda na maziwa mgando wakati akihudhuria tukio la kuchangia katika jengo la Washington Monument wakati huo likiwa bado katika ujenzi. Baada ya siku chache alipatwa na homa kali ya tumbo.

Daktari wake aliweka bayana kwamba Taylor alikuwa amepatwa na kipindupindu (ugonjwa wakati wa zama za Taylor ulikuwa ukisumbua sana) kitaalamu Cholera morbus.

Utata uliibuka katika maradhi hayo lakini baadaye hata wasaidizi wake katika baraza lake walikuja kupatwa na maradhi hayo. Homa aliyokuwa nayo Taylor ilikuwa ni vigumu kupona.

Taylor alisema maneno haya kabla ya kifo chake, “I should not be surprised if this were to terminate in my death. I did not expect to encounter what has beset me since my elevation to the Presidency. God knows I have endeavored to fulfill what I conceived to be an honest duty. But I have been mistaken. My motives have been misconstrued, and my feelings most grossly outraged.”

Taylor alifariki dunia saa 4:35 usiku wa Julai 9, 1850 akiwa na umri wa miaka 65. Hivyo makamu wa Rais Millard Fillmore alikalia kiti chake hadi muhula ulipomalizika Machi 4, 1853.

Taylor alizaliwa katika familia ya watu wenye uwezo, wamiliki wa mashamba huko Virginia. Baadaye walitoka huko na kwenda zao Louisville, Kentucky.

Akiwa jeshini aliansa kuwa Ofisa wa jeshi mnamo mwaka 1808 na baada ya kazi ya ziada alitunukiwa cheo cha Captain mnamo wakati wa vita vya mwaka 1812.

Alipanda vyeo haraka baada ya kufanya kazi nzuri alipokuwa na jeshi katika mapambano yaliyokuwepo Mto Mississippi na mnamo mwaka 1832 katika vita vya Black Hawk alitunukiwa kuwa Kanali. Kazi nzuri katika vita vya Pili vya Seminole huko Florida kati ya mwaka 1835 hadi 1842 alijikuta akipewa jina la utani ‘Old Rough and Ready’.

Mnamo mwaka 1845 wakati jimbo la Texas lilipokuwa likijiunga katika serikali ya Shirikisho Rais James K. Polk alimpeleka kwa kazi maalum huko Rio Grande  kwa ajili ya kupata suluhu ya mzozo dhidi ya Wamexico kwenye mpaka wa Texas na Mexico.

Hata hivyo Aprili 1846 vita ilianza na Taylor akiwa kiongozi wa majeshi katika battalion yake aliyaadhibu vikali majeshi ya Wamexico yaliyokuwa chini ya amri ya Pedro de Ampudia katika vita vya Monterrey. 

Pia Taylor alifanya kwa ushupavu mapambano mengine ya kivita huko Buena Vista ambako upande wa kusini alipata usumbufu kiasi kutoka kwa  Antonio Lopez de Santa Anna. Baada ya hapo Meja Jenerali Winfield Scott alipokea kijiti hicho cha Taylor  lakini umaarufu wake haukutoweka hata kidogo.

Bila hiyana chama cha Whig kikamteua Taylor kupeperusha bendera kwa ajili ya uchaguzi wa Rais mnamo mwaka 1848 licha ya kwamba hakuwa anapendelea sana masuala ya siasa alikubali kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi huo.

0 Comments:

Post a Comment