Julai 1, 1999 alifariki dunia mwanamuziki wa reggae
raia wa Jamaika Dennis Emmanuel Brown. Alikuwa msanii wa reggae katika lovers
rock. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 42. Alizikwa Julai 17, 1999 jijini
Kingston. Enzi za uhai wake alirekodi zaidi ya santuri 75 na kuwa miongoni mwa
nyota wa reggae ulimwenguni.
Mwishoni mwa miaka ya 1990 afya ya Brown ilianza
kutetereka. Alikuwa akisumbuliwa kwenye mfumo wa upumuaji huenda ilitokana na
kuwa mraibu wa dawa za kulevya aina ya cocaine. Matatizo hayo yalimfanya apate
homa kali Mei 1999 wakati wa ziara yake ya muziki nchini Brazil akiwa na
wanamuziki wengine wa reggae.
Akiwa huko alipatwa na kichomi, baada ya kumaliza
ziara hiyo alirudi Kingston na jioni ya Juni 30, 1999 alikimbizwa katika
hospitali ya Chuo Kikuu cha Kingston kutokana na kupata shambulio la moyo.
Brown alifariki dunia siku iliyofuata na taarifa rasmi ilisema nyota huyo wa
muziki alifariki dunia kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mapafu yalishindwa
kufanya kazi.
Wakati huo Kaimu waziri Mkuu P. J Patterson na waziri
mkuu wa zamani wa Jamaika iliyokuwa mikononi mwa kiongozi wa upinzani Edward
Seaga wa chama cha Labour walizungumza katika mazishi yake yaliyofanyika Kingston.
Ibada ya mazishi ilichukua takribani saa tatu ambayo
ilikwenda sambamba na uimbaji wa wasanii Maxi Pries, Shaggy na watoto watatu wa
kiume wa Brown. Alizikwa katika makaburi ya Mashujaa wa Taifa hilo jijini
Kingston. Wakati anafariki dunia alikuwa ameacha mke mmoja Yvonne na watoto 10.
Waziri Mkuu Patterson alitoa salamu zake za rambirambi
na kusema, “Kwa miaka mingi, Dennis Brown alijipambanua yeye mwenyewe kuwa
miongoni mwa wasanii wazuri na wenye kipaji katika zama zetu. Alikuwa akijiita
Crown Prince (mwanamfalme) wa Reggae. Ametuacha na nyimbo nyingi ambazo
zitaendelea kuhuisha mioyo na akili zetu na kwa vizazi vijavyo.”
Uimbaji wake umekuwa chachu ya kuwapo kwa wasanii
wengi wa reggae miaka ya 1970 hadi 2000 wakiwamo Barrington Levy, Junior Reid,
Frankie Paul, Luciano, Bushman, na Richie Stephens.
Mnamo Julai 1999 kundi la wanamuziki nchini Uingereza
likiwa na waimbaji waliokuwa wakifanya kazi chini ya jina la The Bristish
Reggae All Stars wakiwamo Mafia & Fluxy, Carlton "Bubblers"
Ogilvie, Peter Hunnigale, Louisa Mark, Nerious Joseph, na Sylvia Tella
walitengeneza wimbo wa pamoja ikiwa ni salamu za rambirambi kwa mwanamuziki
huyo.
0 Comments:
Post a Comment