Sunday, July 26, 2020

Samuel Ndetaramo Shao: Mwanahabari aliyejitosa kutia nia kura za maoni CCM Mwika Kaskazini

Oktoba mwaka huu Watanzania wanatarajia kuwa na uchaguzi mkuu wa Urais, Wabunge na Madiwani, kuchagua viongozi au kuchaguliwa kuwa kiongozi ni moja kati ya haki ya Kikatiba ambazo zinakuwa ndani ya Kikatiba  ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu shughuli za utawala wa nchi.

Licha ya kwamba Serikali inpata madaraka yake kutoka kwa wananchi kwa njia ya Uchaguzi, pia wananchi wanapata haki ya kushiriki katika shughuli za serikali kwa njia ya uchaguzi. Kwa hiyo uchaguzi  ndio njia pekee ya kushiriki shughuli za serikali moja kwa moja au kwa njia ya uwakilishi.

Katika Makala hii leo tutajikita zaidi  kwenye nafasi ya Udiwani katika maendeleo ya nchi hususan kwenye ngazi ya chini kabisa ambayo inaanzia ngazi ya kata, kijiji , mtaa ama kitongoji.

Ibara ya 21 ya Katiba ya nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile Ibara ndogo ya kwanza (1) imeweka bayana kuwa kila raia wa Tanzania mwenye sifa stahiki anaweza kushiriki katika masuala ya shughuli za utawala wa nchi kwa kuchaguliwa, kuteua au  kuteuliwa.

Ushiriki huo unaweza kuwa moja kwa moja kwa njia ya kuchaguliwa kuwa kiongozi au ushiriki unaweza kuwa wa uwakilishi, kwa raia wanaweza kuchagua viongozi wenye sifa ili watuwakilishe katika vyombo vinavyochukua maamuzi ya kiutawala kwa niaba ya watu wengine.

Ukiwa diwani wa kata fulani na ushiriki wako kwa mujibu Katiba ya nchi ni kwa niaba ya wananchi wenzako waliokuchagua ili ukashiriki kufanya maamuzi juu ya mambo yanayowahusu wao na wewe kwa pamoja juu ya mustakabali wa maisha ya wale wote unaowawakilisha  pamoja na wewe bila kujisahau.

Uchaguzi wa Rais ni njia ya kuiweka Serikali madarakani kwa njia ya Kikatiba, Serikali ya nchi yetu imegatua madaraka yake kwenda kwenye Serikali za Mitaa, ambazo zinaundwa na halmashauri za miji, wilaya na Manispaa, ambapo kuna ushiriki wa wananchi.

Madiwani wana uwezo mkubwa kuchochea maendeleo ya wananchi moja kwa moja na kwa ukaribu zaidi kuzidi wabunge kwa sababu ya ukaribu baina ya wananchi na madiwani kwenye Kata wanazoziwakilisha.

Madiwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanasaidia kupunguza  umasikini kwa kuchochea wananchi kufanya biashara kwenye sekta za huduma kama vile viwanda na kilimo.

Julai 25 mwaka huu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakwenda kufanya chaguzi zake kwa wagombea wa udiwani walio tia nia ya kuomba nafasi hizo kuchaguliwa .

Katika Makala haya inamwangazia Samuel Ndetaramo Shao, ambaye Kitaaluma ni Mwalimu na Mwandishi wa habari aliyetia nia ya kugombea Udiwani katika Kata ya Mwika Kaskazini Mkoani Kilimanjaro.

Shao anaeleza safari yake ya maisha ilianza akiwa shule ya msingi Kaloleni Mkoani Morogoro, na kufuatiwa na elimu ya Sekondari Vunjo.

Anasena baada ya elimu yake ya sekondari alijiunga na elimu ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Mombo na baada ya kuhitimu elimu yake hiyo alijiunga na Chuo cha Uandishi wa habari (Royal College Of Journalist). 

Shao anasema safari yake ya kuwania Udiwani ilianza mwaka 2015 ambapo ligombea na alishindwa na mwaka 2020 hajakata tamaa tena amejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Anasema Kata ya Mwika Kaskazini imekaa upinzani kwa muda mrefu hivyo mtu sahihi ambaye anaweza kuwaletea maendeleo kwa sasa ni yeye  huku akiwa na Kauli mbiu yake “Mwika Kaskazini Mpya ya Kijani Inawezekana”.

Samuel Ndetaramo Shao, ametia nia ya kugombea Udiwani katika Kata ya Mwika Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) anasema kama atafanikiwa kuchaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Mwika Kaskazini yako mambo Matano ambayo ameyapa kipaumbele kwake, kama vile, kuwa na Zahanati ,Maji Safi na Salama, Kituo cha polisi, soko la mazao na ajira kwa vijana na wanawake.

Anasema jambo la kwanza endapo atachaguliwa kuwa Diwani wa Kata hiyo, atahakikisha kwamba anakwenda kutokomeza uhalifu uliokithiri ndani ya kata hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na Kituo cha Polisi, miundombinu ya barabara ndani ya kata hiyo ambazo katika kipindi cha mvua barabara hizo hazipitiki.

“Kata ya Mwika Kaskazini ndio yenye vyanzo vingi vya maji lakini wakazi wa kata hiyo hawana maji safi na salama, wanatumia maji ya mifereji hivyo endapo watampa ridhaa ya kuwa diwani kipaumbele chake cha kwanza ni kwenda kuwatua ndoo maji akina mama ambao wameteseka kwa kipindi kirefu kutafuta maji,”anasema Shao.

Pia jambo lingine ni kuhakikisha kuwa wakazi wa kata hiyo wanakuwa na soko la uhakika kwa ajili ya kuuzia mazao yao ikiwemo soko la ndizi na parachichi hivyo anawaomba wakazi wa kata hiyo kumtuma kijana wao ili aweze kuwaletea maendeleo ya haraka ambayo waliyakosa kwa kipindi kirefu.

MAJUKUMU NA KAZI ZA DIWANI

Diwani huwakilisha wakazi wote wa Kata yake hivyo anatakiwa kuwa karibu na wapiga kura wake na kufikisha mbele ya Halmashauri na Kamati zake vipaumbele vya wananchi ili vijadiliwe na kutolewa maamuzi, kuhamasisha wananchi katika kulipa kodi na ushuru wa Halmashauri, kusimamia matumizi ya Fedha za Halmashauri.

Diwani anatakiwa kuhakikisha Fedha za Halmashauri zinatumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na sio vinginevyo, kuwa kiungo kati ya Halmashauri na ngazi za msingi za Serikali za Mitaa, Pia Diwani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata, anapaswa atumie mamlaka hayo kuwasilisha kwenye Halmashauri maamuzi ya Kata yake na vile vile kuwasilisha kwenye Kata maamuzi ya Halmashauri.

Majukumu mengine ya Diwani  ni kuhamasisha wananchi kuhusu vita dhidi ya umaskini, katika kulitekeleza hili ni lazima ajue kwa ufasaha hali ya kiuchumi na kijamii inayowakabili wananchi wake na kushirikiana nao ili kupanga mipango endelevu ya kujikwamua.

Kazi nyingine ya Diwani ni kufuatilia utekelezaji wa mipango yote ya wananchi na ya Halmashauri, ili kutimiza jukumu hili ipasavyo, Diwani anatakiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi yote ndani ya Kata yake ambalo ni jimbo lake la uchaguzi bila kudai malipo yoyote toka kwenye Halmashauri au wadau wengine. Kimsingi hii ndiyo kazi ambayo Diwani aliahidi kuitekeleza wakati wa kampeni.

Kutetea Maamuzi ya Halmashauri, wakati wa majadiliano ndani ya Halmashauri, Diwani ataelekeza na kutetea maoni yake au ya wakazi wa eneo lake. Hata hivyo, iwapo uamuzi utakaofikiwa na wengi utakuwa kinyume na matarajio yake atalazimika kuunga mkono maamuzi ya wengi yaliyofikiwa kidemokrasia. Kuzingatia misingi yote ya Utawala Bora wakati wa kutekeleza majukumu yote ya Udiwani.



 

0 Comments:

Post a Comment