Chama Kikuu cha Ushirika mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) kimekubali ushauri uliotolewa na serikali wa kupata mwekezaji mpya katika Shamba la Lerongo lenye ekari 541.
Haya yalijiri baada ya ziara ya siku moja hivi karibuni katika shamba hilo lililopo katika kijiji cha Wiri wilayani humo iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Onesmo Buswelu na uongozi wa KNCU.
Katika taarifa yake Meneja wa KNCU Godfrey Massawe alisema mwekezaji waliyemtimua Ottaru Manufacturing and Trading Ltd waliingia naye mkataba mwaka 2004 kwa makubaliano ya kuliendeleza katika Kilimo cha Kahawa, ufugaji na baadhi ya mazao ya msimu kwa makubaliano ya kulipa kiasi cha dola za Kimarekani 23,520 ambazo zilifika hadi 29,000 kwa mwaka.
“Kodi hii aliendelea kulipa hadi ilipofika mwaka 2016 ambapo mwekezaji alianza kusuasua kulipa, na taratibu za kumchukulia hatua zilifanyika akawa anatumia mgongo wa mahakama kukwamisha jitihada zetu, lakini hatimaye haki ilipatikana na ilipofika tarehe 27 Desemba 2019 tulimwondoa mwekezaji huyu katika shamba kwa kutumia madalali wa mahakama ikiwa ni pamoja na kumpa notisi ya kuvunja mkataba,” alisema Massawe.
Aidha Massawe aliongeza kuwa wakati wakivunja mkataba naye deni kwa mwekezaji huyo lilikuwa dola za Kimarekani 109,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 250 za Tanzania hatua ambayo imeliacha shamba hilo kuwa pori na kahawa kufunikwa na majani nyemelezi.
Massawe alisisitiza kuwa kusalia pori na mikahawa kumezwa na majani nyemelezi haina maana ya kubadili matumizi ya shamba hilo nje ya kilimo bali mikahawa hiyo inaweza kurudi katika hali yake na uzalishaji ukaendelea kama kawaida.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya alisema katika ziara hiyo walichokikuta ni kitu cha ovyo kutokana kwamba shamba kama hilo kusalia kama pori ni jambo lisilokubalika isitoshe lina rutuba ya kutosha.
“KNCU kama watashindwa watuambie tubadili matumizi ya shamba hili la Lerongo, hebu fikiria ardhi kama hii yenye rutuba Tanzania ingekuwa na wawekezaji wanaoshindwa kuendeleza kusingekuwa na maendeleo yoyote, tunawapa siku 45 kuanzia Julai 6 mwaka huu wawe wameanza kuweka matangazo rasmi ya wanaotaka kuwekeza kujitokeza,” alisema Buswelu.
Buswelu alisema mwekezaji akiwepo maisha ya wanakijiji ambao ni watanzania yanabadilika kwani kitendo cha Ottaru kukacha kuliendeleza shamba hilo kumepoteza ajira zaidi ya 100 za wafanyakazi waliokuwapo hapo hivyo maisha ya familia zao kuyumba.
“Nimesikia suala la usalama limekuwa tete kwa wanakijiji kutokana na kugeuka pori kwani tembo wamekuwa wakivamia makazi na mashamba yaliyo jirani sasa hiyo haifai tutafuta mwekezaji la sivyo linaweza kubadilishwa matumizi likawa hata gereza la kilimo na wafungwa wakawa wanawekwa huku kwa manufaa ya taifa letu,” aliongeza Buswelu.
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa KNCU Kandata Kimaro aliihakikishia serikali kuwa agizo litatekelezwa ipasavyo kwani mpaka wamefikia hapo juhudi kubwa za serikali zimefanyika hadi kumwondoa mwekezaji huyo na kwamba hali ya usalama kwa sasa imekuwa shwari na wanaendelea kujipanga kupata mwekezaji mpya.
KNCU (1984) LTD inahudumia wakulima wadogo wa kahawa katika kanda za Siha, Hai, Moshi Vijijini na Rombo ambapo vyama 92 vya ushirika vinakamilisha chama kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro.
0 Comments:
Post a Comment