Ramani ya Tanganyika, wakati wa Utawala wa Ujerumani; Tanganyika ilikuwa ikiitwa German East Africa (GEACO) |
Taifa la Tanganyika lilijipatia uhuru wake Desemba 9, 1961
kutoka kwenye makucha ya Uingereza. Historia yake inaanzia mbali, harakati za
kudai uhuru wa Tanganyika ambayo baadaye (1964) ilikuja kuungana na Zanzibar
kuunda inayoitwa sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwandishi wa harakati za uhuru wa Tanganyika Mohammed Said
katika kitabu chake cha “The Life and Times of Abdulwahiid Sykes,” anasema Julius Kambarage Nyerere alikuja Dar es Salaam
mwaka 1952 akiwa kama mwalimu wa shule ya St. Francis College, Pugu.
Nyerere alikuwa na Mwapachu huko Tabora katika mwaka 1945, na
Makerere College na baadaye nchini Uingereza wakichukua masomo ya juu.
Inawezekana kwamba Nyerere kufuatia harakati za chama cha
TAA, alisikia kuhusu Abdulwahid kupitia kwa Mwapachu alipokuwa bado yuko
Uingereza. Mwapachu na Nyerere walikuwa wanafunzi katika Chuo cha Makerere wakati
ambapo Kasella Bantu na Nyerere walifundisha katika shule moja, St. Mary's
School huko Tabora.
Uhuru wa Tanganyika huwezi kuuzungumzia bila kumzungumzia
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere namna alivyopita hadi kufikia kushika madaraka
makubwa ya kuliongoza taifa.
Nyerere alipata kusema kwamba, ilikuwa dhahiri yake
kufundisha kwa muda kisha aingie kwenye siasa. Hatimaye Nyerere alifanywa
kuukubali ule uongozi ambao Tanganyika Africans Association (TAA) ilimpa.
Shindano baina ya aliyekuwa rais, Abdulwahid na Mwalimu wa
shule asiyefahamika, Julius Nyerere, lilifanyika kwenye Ukumbi wa Arnatouglo Aprili
17, 1953. Ukumbi huu ukienda ofisi ndogo za Chama chsa Mapinduzi mtaa wa
Lumumba jijini Dar es Salaam utaonyeshwa tu.
Nje ya duara la uongozi wa TAA ambao ulimpendekeza kugombea,
Nyerere alikuwa mgeni kabisa kwa wote waliokuwa na haki ya kupiga kura.
Shughuli za kisiasa za Nyerere zilianza tangu siku hii. Hapa
alikuwepo Nyerere, mgeni na mtu aliyekuwa hana historia ya kuongoza mapambano
ya watu dhidi ya serkali ya kikoloni.
Familia ya Sykes ilikuwa imehusika na siasa za kienyeji mjini
Dar es Salaam kwa takribani robo ya karne wakianzisha na kuongoza vyote viwili
vyama vya African Association na Al Jamiatul Islamiyya.
Abdulwahid kama mtoto wa Kleist Sykes alikuwa mmoja wa
familia iliyojadili hadharani masuala ya kisiasa ya siku zile na kuyaandika
wakati mwingine wakiandikiana barua na mamlaka ya kikoloni.
Uchaguzi ulikuwa wa kuinua mikono. Phombeah aliyekuwa
mfawidhi wa Ukumbi wa Arnatouglo alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo. Phombeah
aliwaomba wote wawili Abdulwahid na Nyerere kutoka nje ya ukumbi ili uchaguzi
uanze.
Wiki nzima kabla ya uchaguzi Phombeah alikuwa akizunguuka
huku na kule akimfanyia kampeni Nyerere. Lakini hakukuwa na haja ya kufanya
hivyo, duara la ndani kabisa la TAA la Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz na Rupia
lilikuwa tayari limekwishaamua kumfanya Nyerere awe rais wa chama.
Uchaguzi ilikuwa kutimiza utaratibu tu. Baada ya Abdulwahid
na Nyerere kutoka nje upigaji kura ulianza Abdulwahid "alishindwa"
uchaguzi huo ikiwa ni mara yake ya kwanza katika maisha yake yote ya siasa.
Nyerere alishinda uchaguzi huo dhidi ya Abdulwahid aliyekuwa
rais wakati huo kwa kura chache sana. Huu ulikuwa ndio mwanzo na mwisho kwa
ushawishi wa familia ya Sykes katika chama cha TAA na mwanzo wa shughuli za
kisiasa za Nyerere. Tangu siku ile historia ya kisiasa ya Tanganyika kamwe haikuwa
ile ile tena.
Dossa Aziz alikuja kutoa taarifa kwamba Abdulwahid hakushindwa
katika uchaguzi ule,
"Hakukuwa na namna yoyote Nyerere angeweza kumshinda
Abdulwahid katika Dar es Salaam ya miaka ya 1950. Abdulwahid hakushindwa katika
uchaguzi ule. Sisi sote tulitaka iwe vile. Uongozi wa TAA tulimtaka Nyerere."
Abdulwahid alikuwa mwenye kuonekana mara kwa mara, kama rais
wa TAA aliifanya ofisi yake ipendeze. Alizoea kuwakaribisha watendaji wa TAA
nyumbani kwake kwa chakula cha mchana na usiku na hili liliongeza umaarufu
wake. Wakati huo wengi walidhani Nyerere asingefaa katika nafasi ile ya
Abdulwahid.
Marehemu Tewa Said alipata kueleza kwamba siku ile kabla ya
uchaguzi pale katika Ukumbi wa Arnatouglo, Abdulwahid alikwenda nyumbani kwake
jioni.
Wakati huo Tewa alikuwa akikaa mtaa wa Pemba si mbali sana
toka nyumbani kwa Abdulwahid. Abdulwahid alimwambia Tewa haya kuhusu mabadiliko
ya uongozi ambayo waliamua yafanyike kwenye chama cha TAA;
"Tewa, kesho tunakwenda kumpa huyu mtu, Nyerere, mamlaka
ya kuendesha nchi hii. Kuanzia hapo, mara tu tutakapomchagua kutuongoza hakuna
namna ya kumnyang'anya mamlaka hayo. Hatumfahamu vizuri sana lakini natumaini
kila kitu kitakwenda vizuri."
Tewa akikumbuka matukio yaliyopelekea Nyerere kuchaguliwa
kama rais wa TAA alisema; "Kitu pekee alichokuwa nacho Nyerere zaidi ya Abdulwahid
kilikuwa ile digrii ya chuo kikuu. Abdulwahid kwa takribani miaka minne tangu
akamate ofisi katika mwaka 1950, alikataa kuitisha mkutano wa wajumbe kwa
sababu moja au nyingine, mpaka alipokutana na Nyerere. Ninaamini kama
Abdulwahid angekwenda Makerere tungeunda chama cha TANU mapema zaidi, labda
kabla ya mwaka 1954 na Abdulwahid angekuwa rais, hata kama angeshindana na
Nyerere."
Haya ni miongoni mwa mambo yaliyokuwapo nyuma ya uhuru wa
Tanganyika ambayo mwaka 1919 sehemu kubwa ya koloni la Kijerumani ilikabidhiwa
rasmi mikononi mwa Uingereza kama eneo la kudhaminiwa chini ya mamlaka ya
Shirikisho la Mataifa kulingana na kifungo 22 cha mkataba wa Versailles.
Wajerumani walianza kushirikia eneo la Tanganyika tangu mwaka 1886 ikiwa ni
miaka miwili baada ya Mkutano wa Berlin mwaka 1884.
Ramani ya Afrika |
0 Comments:
Post a Comment