Thursday, November 29, 2018

LHRC: Mwezeshaji wa Haki za Binadamu Tanzania


NA JABIR JOHNSON
johnsonjabir@gmail.com
Waandishi wa Habari walioshiriki mafunzo ya siku tatu yaliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kati ya Oktoba 30 hadi Novemba 2, 2018 mjini Morogoro katika picha ya pamoja. (Picha na Jabir Johnson)

Mwandishi Dkt. Helen Kijo-Bisimba katika kitabu chake ‘Mwongozo wa Haki za Binadamu’ cha mwaka 2014 anatoa tafsiri ya Haki za Binadamu kuwa ni zile haki ambazo kila mwanadamu anazo au anastahili kuwa nazo kwa kuwa tu yeye ni binadamu.

Pia katika tafsiri hiyo kwenye ukurasa wa 13 anaandika Haki  za  binadamu  hazitegemei au kutolewa  na  hati  ya  kisheria.  Haki  hizi  ni  za  asili, binadamu huzaliwa nazo na hivyo inabidi zitambuliwe na kuheshimiwa.

HISTORIA YA HAKI ZA BINADAMU
Katika  historia  ya  binadamu  imebainika  kuwa  jamii  nyingi  zilitambua  na  kuthamini  utu  wa haki za Binadamu. Hii ni kabla ya hata haki hizi kuandikwa au kutamkwa katika mikataba au sheria  za  nchi  mbalimbali. 

Kwa upande  mwingine,  vitendo  vya  uonevu,  dhuluma  na  vya kinyama  vilikuwepo  katika  jamii  nyingi  duniani.  Na hii ilifanya  baadhi  ya  jamii  kuinuka  na kudai haki za binadamu pale zilipokuwa zinakiukwa au kutotekelezwa.

Historia inaonyesha  jitihada  za  mwanzo  zilizofanywa  na  baadhi  ya  jamii  mbalimbali katika kuzinadi haki za binadamu ili kuweza kutekelezwa ipasavyo.

Jitihada hizi, ndizo  zimekuwa  chimbuko  la  kuandikwa  kwa  mikataba  mbalimbali  ya  haki  za binadamu.

Hati ya Magna Carta kwa mara ya kwanza iliandikwa mwaka 1215 na Mfalme John wa England akiwa na wenzake Stephen Langton Bishop Mkuu wa Canterbury.

Hata hivyo kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945 ndio kulileta changamoto rasmi ya kulinda na kuheshimu haki za bianadamu karibu duniani kote.

Hii ni baada ya watu wengi kuteseka, kufa na pia kunyanyaswa katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Hapo ndipo jumuiya ya Kimataifa ilianza kukubali, kuthamini na kulinda haki za binadamu
Asasi zisizo za kiserikali kwa kiwango kikubwa zimekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa elimu  na  mafunzo  ya  haki  za  binadamu  katika  nchi  nyingi.

KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU (LHRC)
Nchini Tanzania Kituo cha Sheria  na  Haki  za  Binadamu  kimekuwa  kikiendelea  mafunzo  mbalimbali  ya  haki za binadamu tangu mwaka 1995.

Mafunzo haya yamekuwa yakitolewa kwa makundi na watu mbalimbali kama vile  viongozi  na  watendaji  wa  serikali    mfano, wabunge,  madiwani, mahakimu  askari  polisi,  viongozi  wa  serikali  za  vijiji  na  wananchi  kwa  ujumla  hasa  walio vijijini.
 
Mafunzo   hayo daima   yamekuwa   yakilenga   katika   kuisaidia   jamii   nzima   ya watanzania walio mijini na vijijini kuelewa maana ya haki za binadamu katika maisha yao ya kila siku.

Kujua manufaa  ya  haki  za  binadamu  na kuchukua jukumu la  kuheshimu, kutetea, kulinda na kuendeleza haki za binadamu kwa manufaa ya watanzania wote.

Oktoba 30 hadi Novemba 2 mwaka huu LHRC iliendeleza shauku yake ya kutoa elimu katika makundi mbalimbali na safari hii ilikuwa zamu ya waandishi wa habari nchini ambao walikutana mjini Morogoro kwa ajili ya kupeana uzoefu na ufafanuzi katika baadhi ya maeneo yanayohusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika.

UMUHIMU WA WANAHABARI
Wanahabari kutoka mikoa mbalimbali walioshiriki mafunzo ya siku tatu yaliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kati ya Oktoba 30 hadi Novemba 2, 2018 mjini Morogoro katika picha ya pamoja. (Picha na Jabir Johnson)
Wanahabari ni kiungo muhimu katika makundi yote katika jamii katika kufikisha ujumbe kwa jamii kuliko muhimili wowote na ndio sababu mhimili huo unapewa jina la ‘Muhimili wa Nne usioonekana’.

Mtu yuko radhi asitoe taarifa zake katika uongozi wa kiserikali au chama akatoa kwa waandishi wa habari akiamini kuwa ujumbe wake utawafikia mamia kwa maelfu.

Licha ya uzuri huo lakini kumekuwapo na changamoto mbalimbali ndani ya medani hiyo hali ambayo imekuwa ikitishia hata uhuru wa utoaji wa taarifa.

Sheria mbalimbali zimekuwa zikitungwa kwa ajili ya kuminya au kuwapendelea zaidi watawala kuliko wanahabari hali ambayo ni hatari kwa jamii ambayo imekuwa ikitegemea msaada mkubwa kutoka kwa muhimili huo.

SHERIA KANDAMIZI ZA UPASHANAJI WA HABARI
Kila nchi ina utaratibu na kanuni zake katika upashanaji wa habari lakini hizo zote zinapaswa kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na zile za kimataifa kutokana na ukweli kwamba walio wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) walikubaliana kuwapo na usimamizi mzuri wa haki za binadamu.

Hali ya upashanaji wa habari nchini Tanzania, imekuwa ikikua siku baada ya siku licha ya changamoto za hapa na pale.

Mwanasheria wa LHRC William Kahale ambaye alikuwa miongoni mwa wawezeshaji katika semina hiyo alisema, “Kuna maendeleo makubwa kwa maana ya utoaji wa taarifa. Hapo awali kabla kwa kiasi kikubwa hakukuwa na sheria ukiacha katiba ya Jamhuri ya Muungano (Tanzania) katika ibara ya 18 inatoa uhuru wa kupokea, kutoa taarifa lakini kuna sheria  ambazo zilikuwa zikiupoka uhuru huo."

Kwa kifupi Katiba  ya  Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania  ya  mwaka  1977  (kama  ilivyorekebishwa) inalinda haki za kiraia na kisiasa, na haki za kiuchumi, kijamii, na kiutamaduni.

Licha ya kulinda kwake kuna sheria kandamizi kwa vyombo vya habari Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Takwimu ya mwaka 2016, Sheria ya Utoaji wa Taarifa, Sheria ya Uhalifu Mitandaoni na ile ya Maudhui ya Mitandaoni.

Hizi zote zina nia ya kuvibana vyombo vya habari hali ambayo inabana uhuru wa kujieleza na kuwasilisha taarifa mbalimbali.

UHURU WA HABARI NA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
Kahale alisema serikali ya awamu ya tano ya Dkt. John Magufuli imejipambanua kuwa inapambana na rushwa waziwazi.

Endapo jamii haitakuwa huru katika utoaji wa taarifa zake na mapambano ya rushwa hayatakuwa na maana yoyote kwani vita dhidi ya rushwa haiwezi kufanywa na serikali peke yake bila kuhusisha wananchi wake.

Kuviminya vyombo vya habari ni njia mojawapo ya kufanya mapambano ya rushwa kuwa magumu kwani watu watakuwa wakiogopa.

TANZANIA YA VIWANDA NA UHURU WA HABARI
Katika nukuu za Papa Francis wa Kanisa Katoliki anasema (katika tafsiri isiyo fasaha), “Haki za Binadamu hazikiukwi na ugaidi pekee, au ukandamizaji au mauaji bali kuwa na mifumo ya kiuchumi isiyostahili husababisha pengo la usawa kuwa kubwa.” 

Hivyo basi katika maendeleo ya taifa la Tanzania yatategemea sana usimamizi mzuri wa haki za binadamu hususani katika ‘Tanzania ya Viwanda Tunayoitaka.’

Kahale alisema, Tanzania ya viwanda inategemea namna ambavyo wananchi wanabadilisha taarifa za kiuchumi kuhusu bidhaa zao, sasa kama Sheria ikiwamo ya takwimu itabana uhuru wa takwimu za kiuchumi kufanyika watu wataogopa kuwekeza hivyo itakuwa ndoto kufikia malengo.

Makala hii imetayarishwa na Jabir Johnson, aliyekuwa Morogoro katika semina iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Kwa maoni na ushauri barua pepe: jaizmela2010@gmail.com

0 Comments:

Post a Comment