NA JABIR
JOHNSON
Siddharth
Katragadda ni mwandishi, mtengenezaji wa filamu, msanii na mwana ushairi mwenye
asili ya India aliyezaliwa mwaka 1972 aliwahi kusema katika mojawapo ya nukuu
zake aliwahi kusema, “Ukubwa wa utamaduni
fulani unaweza kuupata katika matamasha.”
Nukuu hiyo
inaweza kushabihiana na kilichojiri katika tamasha la 37 mjini Bagamoyo mwaka
huu. Tamasha hilo kongwe nchini lilianza kurindima Oktoba 20 na kuhitimishwa
Oktoba 27 mwaka huu.
Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe alifungua tamasha
hilo huku Naibu wake katika wizara hiyo Juliana Shonza alifunga. Tamasha hili
lilizidi kuwanufaisha wenyeji wa Bagamoyo kwani madereva wa pikipiki ‘bodaboda
na bajaji’ walipata wateja wengi kutokana na tamasha kumalizika nyakati za
usiku.
Biashara ya
bidhaa za madukani na masokoni mzunguko wake uliongezeka hali kadhalika katika
mahoteli na nyumba mbalimbali za wageni. Katika siku ya ufunguzi uwepo wa
mabalozi wa Palestina, India, Msumbiji na Nigeria.
Mtendaji
Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dkt. Herbert Makoye
alisisitiza umuhimu wa udhamini katika tamasha hilo ili kuendeleza dhima ya
uanzishwaji wa Bagamoyo International Festival.
Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Dkt Herbert Makoye |
SIMANZI KIFO
CHA MPONDA
Machi 22,
2018 alifariki Mwalimu na gwiji la Sanaa John Mponda. Dakika moja katika siku
ya ufunguzi ukumbi ulikaa kimya kumkumbuka mhamasishaji mkuu wa tamasha hilo
kwa miaka mingi Mwalimu Mponda.
Mtazamaji
aliyetambulisha kwa jina la Farida Sengu akibubujikwa na machozi alisema,
“Tamasha limekuwa doro kweli angekuwapo Mwalimu Mponda ungependa…”
VIKUNDI 100
VYA BURUDANI
Vikundi 65
kutoka Bagamoyo na vingine kutoka nje ya mkoa wa Pwani kikiwamo kile cha ngoma
ya Kisonge TPS-Moshi. Pia katika burudani hiyo kulikuwa na kikundi cha wasanii
kutoka Munich nchini Ujerumani ambacho kilionyesha muziki wake kwa watazamaji.
Uimbaji wa
mwanadada Sonja Lachenmayr, na wapiga vyombo Felix Renner, Simon Mack, Vincent
Crusius, Anne Buter na Hugo Siegmeth uliwagusa wengi.
Kikundi cha Ngoma cha Wakufunzi wa TaSUBa wakionyesha umahiri wao jukwaani katika tamasha hilo |
WARSHA NA
SEMINA KWA WASANII
Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Bagamoyo na Kituo cha
Ushauri Nasaha cha Life and Hope Rehabilitation vilipata fursa ya kupeleka
elimu kuhusu masuala ya rushwa na uraibu wa dawa za kulevya unaowakumba vijana
ambao ni nguvu kazi ya taifa.
KIKUNDI CHA
WALIMU TaSUBa
Kilitisha
sana tangu ufunguzi hadi kufunga pale kilipopewa nafasi ya kupanda jukwaani
kuonyesha umahiri katika ngoma na maigizo.
Ilionyesha
wazi kuwa hawakukosea kuwa walimu na kutengeneza picha ya wanafunzi watakaokuwa
wakitoka hapo watakuwa manguli wa Sanaa.
Kina dada watatu kutoka Harare Zimbabwe wanaounda bendi ya Weutonga kutoka kushoto ni Nancy, Beauty na Edith wakihitimisha mojawapo ya wimbo katika tamasha hilo. |
Mwanamke
aliyekuwa akishikilia gitaa la bass, Edith Weutonga hakika alikonga nyoyo za
watazamaji waliofika kutokana na umahiri wake wa kuimba na kupiga gita hilo kwa
ustadi mkubwa.
Hata kama
walikuwa wakiimba lugha ya Kichewa lakini muziki ni muziki tu, kelele, vifijo
na nderemo havikuzuilika ukumbini hapo.
Edith hakuwa
peke yake alikuwa na wenzake Beauty, Nancy, Ishe, Richard, Farai, Givemore na
Aaron.
UWEPO WA
MATOVOLWA
Kuonekana
kwa Lumole Matovolwa maarufu BIG au Tupatupa katika maigizo ya majukwaani
kulivutia sana watazamaji ambao wengine walikuwa wakitazama kwa hisia maigizo
yao likiwamo la ‘Bibi Titi Mohamed’.
Akizungumza
Matovolwa alisema inapaswa watanzania kukumbuka na kutilia mkazo maigizo ya
majukwaani ili kuendeleza utamaduni wa watanzania kwani kwa sasa wengi
wamesahau na wengine hawajui kutokana na uzito mdogo yanayopewa maigizo hayo.
“Tamthilia za nje zimeua sana maigizo ya majukwaani…” alisema Matovolwa.
KIKUNDI CHA
NIHICHILILA
Kikundi hiki
kutoka Nanyumbu kilitisha sana kutokana na kuwa na asilimia kubwa ya wachezaji
wake ni wenye umri usiopungua miaka 45. Umahiri
katika kutikisa makalio ulivutia sana kwa wenyeji hao kutoka Kusini mwa
Tanzania.
MAONYESHO YA
SANAA ZA UCHONGAJI, UCHORAJI NA USANIFU
Msanii wa Akili Arts & Crafts akitoa maelezo ya kazi yake ya sanaa kwa Katibu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Suzana Mlawi alipozuru tamasha hilo |
Kusanifu ni
kuumba, kufanya jambo au kitu kwa kutumia ufundi au ustadi ili kuvutia watu kwa
uzuri wake. Mtu hueleza hisia zinazomgusa kwa kutumia umbo fulani ambalo
limesanifiwa.
Hivyo kazi
yoyote ya sanaa inategemewa ioneshe ufundi wa hali ya juu ili iwe na mvuto kwa
hadhira yake. Tukiwa Bagamoyo tuliweza kujionea kazi ya sanaa kupitia tanzu za
fasihi, uchoraji, ususi, ufumaji, utarizi, uchongaji, ufinyanzi na kadhalika. Katika
ukumbi wa Flexible wasanii walikuwapo humo kuonyesha kazi zao.
MADHAIFU YA
TAMASHA LA 37
Vikundi
dhaifu, Mfumo wa sauti haukuwa mzuri sana, Jukwaa la Nje lina umuhimu wake
lililopo la Mwembeni halifai kwa maendeleo ya kizazi cha sasa, Mfumo wa Kamera
za kutembea unapaswa kutiliwa mkazo ili kuendana na sayansi na teknolojia,
Uwepo wa washereheshaji butu, pia vipaza sauti vichache vilikuwa pungufu
ikilinganishwa na hali ya sasa.
Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo - TaSUBa |
USHAURI KWA
WAANDAJI NA WASANII
Kuhakiki
vikundi ni vema kuwa na vichache ambavyo vitashibisha kiu za washiriki na
watazamaji kuna wakati ilifikia ukumbi unakuwa umepoza licha ya wasanii kuwapo
jukwaani.
Haya ni
matamasha ya burudani kuwapandisha jukwaani washereheshaji wa mikutano ya ndani
sio sawa, Kwani MC ana mchango mkubwa wa kulifanya jukwaa lisimame au lilale.
Kwa upande
wa wasanii wenyewe kwa upande wenu sio kila tamasha unapaswa kupanda jukwaani
wakati mwingine ni vema kujipima ukiona uwezo wako bado ni mdogo usipande
jukwaani kupoteza muda wa watu wengine, jipange kwa wakati mwingine.
Wadhamini
jitokeze kwa nguvu kudhamini tamasha la 38 ili liweze kuvuta zaidi kwani ni
nafasi pekee haiwezekani mtu afunge safari kutoka Ulaya ajigharamie zaidi ya
shilingi milioni 15 halafu mfanyabiashara wa Tanzania unashindwa kuchangamkia
fursa hii kwa shilingi milioni tano kwenda mbele.
TaSUBa
hoyeeeeee! Bagamoyo International Festival juuuu!
Watazamaji wakifuatilia kwa makini kinachoendelea katika jukwaa wakati wa tamasha la 37 la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo |
0 Comments:
Post a Comment