Ron Davis (mwenye tai nyekundu), akiwa mjini Pretoria na Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela. Picha hiyo ilipigwa mwaka 1992 wakati Ron Davis alipozuru taifa hilo. |
DAR ES SALAAM, TANZANIA
Makala yaliyopita tulijikita kumfahamu kiundani kocha Ron
William Davis aliyemnoa mwanariadha aliyeipa medali ya kwanza Tanzania Filbert
Bayi.
Pia tuliangazia kwa kifupi kuhusu tukio la mwaka 1968 katika
michuano ya Olimpiki ambalo Tommie Smith na John Carlos baada ya kushinda mbio
jijini Mexico waliunga mkono mapambano dhidi ya ubaguzi wa mtu mweusi.
Haikutosha tulimuona Ron Davis akishindwa katika mbio za
kuwania kufuzu hivyo kushindwa kwenda kwenye michuano ya Olimpiki ya mwaka
1964.
Hata hivyo alipozwa machungu yake kwa kupewa ziara ya kuzuru
Afrika chini ya Goodwill.
Hapo ndipo kiini cha makala haya kuhusu Ron Davis ambaye ni
Mmarekani mzaliwa wa New York City aliyekulia Baltimore na Connecticut.
Leo tunaendelea katika sehemu ya pili ambayo Ron Davis
anasimulia namna alivyofika Afrika Kusini na kukutana na Nelson Mandela akiwa
ametoka jela la Robben Island.
ILIKUAWAJE?
Nelson Mandela enzi za uhai wake. |
Licha ya kushindwa kufuzu michuano ya Olimpiki mwaka 1964
Idara ya Michezo ya jimbo ilimteua kuwa miongoni mwa watakaozuru Afrika kwa
majuma sita katika nchi 20.
Nchi ya kwanza Ron Davis anasema ilikuwa Ghana na hapo ndipo
alipokutana na wanariadha wengi wa Afrika hivyo kuhamasika na programu za mbio
fupi za uwanja (Track & Field).
Tukio la kukutana na Nelson Mandela mpambanaji wa ubaguzi wa
rangi nchini Afrika Kusini lilitokea ikiwa ni miaka takribani 15 baada ya
kuhitimisha kibarua chake cha kuinoa Nigeria ambayo aliipa medali katika
michuano ya All Africa Games mwaka 1978.
Mwaka huo akiwa na kocha Lee Evans, Ron Davis waliweka
rekodi ya kuwa taifa la kwanza kuizabua Kenya kwa ushindi mwingi wa medali.
Hivyo Nigeria hadi sasa inashikilia rekodi ambayo
haitafutika kamwe kuwa taifa la kwanza kuitupa chini Kenya kwani hakukuwa na
taifa lolote barani Afrika ambalo lilikuwa na uwezo wa kuizidi Kenya kwa medali
na pointi.
Ron Davis alifanikiwa kufanya hayo kwa medali na hata pointi
akiipa Nigeria pointi 68 huku Kenya ikijiwekea kibindoni pointi 63.
Katika ukocha wake zaidi ya miaka 40 sasa hataweza kusahau
alipochaguliwa na Shirikisho la Kimataifa la mbio za Ridhaa (IAAF), kusimamia
na kuratibu timu ya Afrika ya mbio za kiwanja ili kupambana na Afrika Kusini
jijini Dakar, Senegal na Johannesburg, Afrika Kusini.
Alichokifanya Ron Davis anasema, " Niliwasiliana na ANC
ambao tulikubaliana kukutana na Nelson Mandela na wakati huo alikuwa akiwania
Urais wa kuliongoza taifa la Afrika Kusini."
Hafla ya usiku iliyopangwa
kukutana na Nelson Mandela ilifanikiwa. Usiku ule Ron Davis anasema
anaukumbuka kwani Mandela aliomba radhi kwa wanamichezo wa Afrika Kusini wenye
asili ya Afrika kwa michezo yote ukiwamo riadha kwa mgomo uliowafanya
wasishiriki michuano ya Olimpiki na michuano ya kimataifa.
Itakumbukwa miaka ile ya 1960 hadi 1980 kulikuwa na wimbi
kubwa la ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Mauaji ya watu 69 wakiwamo watoto 29 katika kituo cha polisi
kule Transvaal (ambayo sasa ni Gauteng) maarufu 'Sharpville Massacre' Machi 21,
1960 ilikuwa miongoni mwa matukio yaliyokuwa yakionyesha hali ya ubaguzi
ilivyokuwa nchini humo.
Kauli ya Mandela usiku ule kuomba radhi ilimpa kibali katika
uchaguzi. Ikumbukwe mwaka 1964
alihukumiwa miaka mitano jela na serikali ya kikaburu na baadaye walimtupa jela
ya Robben Island alikodumu hadi mwaka 1990.
Mchango wa Ron Davis katika kuirudisha Afrika Kusini katika
michuano ya kimataifa ilionekana michuano ya Olimpiki ya mwaka 1992 mjini
Barcelona, Hispania.
Afrika Kusini ilishiriki kwa mara ya kwanza tangu mwaka
1960, ikiwapeleka wanamichezo 93 wanaume 68 na wanawake 25 ambao walishiriki
matukio 87 kwenye michezo 19.
Afrika Kusini ilirudi na medali mbili za fedha. Mwanariadha
Elana Meyer alikuwa miongoni mwa waliopa medali ya fedha Afrika Kusini katika
mita 10,000 (10K) akitumia dakika 31:11.75
Pia Ron Davis anasema baada ya kumsoma kwa kina Nelson
Mandela aligundua masuala mbalimbali yenye kutia moyo katika medani ya michezo.
"Niliposoma nukuu za Nelson Mandela; aliposema Elimu ni
silaha yenye nguvu inayoweza kubadilisha dunia, pili aliposema Michezo ina
nguvu ya kubadilisha dunia ilinigusa sana."
USHAWISHI WA GRACA MACHEL KUKUTANA NA MANDELA
Kutokana na kufanana katika mapambano dhidi ya mtu mweusi
Ron Davis alijikuta akikutana na wapambanaji mbalimbali barani Afrika miongoni
mwa hao alikuwa Graca Machel ambaye alikuwa mke wa Rais wa zamani wa Msumbiji
Samora Machel na baadaye Nelson Mandela.
Ron Davis anasema alipata nafasi ya kuinoa Msumbiji ambayo
ilimpa nafasi ya kupenya na kukutana na Nelson Mandela.
Njia ilirahisishwa kutokana na uhusiano wa Graca Machel na
Nelson Mandela hivyo alipopewa majukumu ya kuandaa timu wakati ule alikuwa na
mawasiliano mazuri na Graca.
Makala haya yametayarishwa na Jabir Johnson ambaye alipata
fursa ya kuzungumza na Ron Davis masuala
mbalimbali ya maisha yake na medani ya riadha alipotua nchini Tanzania. Kwa
maoni ushauri barua pepe: jaizmela2010@gmail.com
0 Comments:
Post a Comment