Thursday, July 9, 2020

Ifahamu Historia ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)


Kwa mujibu wa vyanzo ndani ya KKKT inaelezwa kuwa Mwaka 1887 kazi ya Injili kwa Kanisa la Kilutheri ilianzishwa nchini Tanganyika (baadaye Tanzania) na Chama cha “Misioni cha Berlin III” au “Evangelical Missionary Society for East Africa” (EMS) kutoka Ujerumani. Kituo cha kwanza cha misheni kilikuwa ni Kigamboni, Dar es Salaam.


Chama cha pili, yaani “Chama cha Misioni Berlin I”, nacho kutoka Ujerumani, kiliingia Tanganyika kikitokea Afrika ya Kusini na kuanza kazi Nyanda za Juu Kusini mwaka 1891 kilipoanzisha kituo cha misheni sehemu iitwayo Ipagika au Pipagika (Wangemannshöhe) katika Dayosisi ya Konde.


Mwaka 1890 “Chama cha Berlin III” kilibadilika na kuchukua sura mpya baada ya kubadili sera yake na kujulikana kwa jina la “Bethel” au “Misioni ya Bethel”. Misioni hii ikafika Tanga na kuanza kazi eneo la Mbuyukenda. Baadaye Misioni ya Bethel iliamua kufkisha Injili ya Kristo nje ya mipaka ya Tanganyika.


Wamisioari waliohusika walipanga kwenda Rwanda kupitia Bukoba. Walipofika Bukoba mwaka 1910 wakashawishika kufungua kituo Bukoba na ile nia ya kuanzisha kazi ya misioni Rwanda ikawa imesitishwa. Chama cha tatu kufka Tanganyika ni “Chama cha Misioni cha Leipzig” (nacho kilitokea Ujerumani).


Kiliingia nchini mwaka 1893 na kuanza kazi ya misioni Kaskazini ya nchi kwa kuweka kituo cha misheni Kidia, Old Moshi.


Kutokana na vyama hivyo vitatu kijiti cha kueneza Injili  ilipokelewa na wenyeji toka kwa wamisionari wa Ujerumani.


Na vyama vingine vya misioni vilivyofka baadaye kutoka Ulaya na Marekani navyo vilieneza Injili kwa kufundisha Neno la Mungu kwa upendo na kwa usahihi, hasa baada ya Vita ya I ya Dunia (1914 - 1918) na Vita ya II ya Dunia (1939 - 1945).


Pamoja na kueneza Injili, Kanisa lilianza kutoa huduma mbalimbali za kijamii na diakonia kwa lengo la kumhudumia mwanadamu kikamilifu – kimwili, kiroho na kiakili. Makanisa saba yanayojitegemea ambayo baadaye yaliungana na kuunda Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Tanganyika yalianzishwa.


Mnamo Juni 1963 Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanganyika (KKKT) likaundwa. Baada ya KKKT kuanzishwa Kanisa la Ubena-Konde (eneo la Nyanda za Juu Kusini) likaitwa Dayosisi ya Kusini; Kanisa la Uzaramo-Uluguru likaitwa Dayosisi Mashariki na Pwani; Kanisa la Usambara-Digo likaitwa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki; Kanisa la Kaskazini likaitwa Dayosisiya Kaskazini; Kanisa la Mbulu likaitwa Dayosisi ya Mbulu; Kanisa la IrambaTuru likaitwa Dayosisi ya Kati na Kanisa la Kaskazini Magharibi likaitwa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi.


Yapo maeneo nchini ambayo yalikuwa yanafanya kazi ya Injili kama misheni nayo ni: Mkoani Mara, Mashariki ya Ziwa Victoria, Ruvuma, Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Kusini Mashariki ambayo sasa ni Dayosisi.


Dayosisi za mwanzo nazo kwa kutegemea vigezo vya kikatiba na historia zikaendelea kugawanyika na hadi 2014 KKKT ikawa na Dayosisi 24 kama ifuatavyo: Dayosisi ya Kusini, Dayosisi ya Konde; Dayosisi ya Iringa; Dayosisi ya Kusini Kati; Dayosisi ya Kusini Magharibi; Dayosisi Mashariki na Pwani; Dayosisi ya UlangaKilombero;  Dayosisi ya Morogoro na Dayosisi ya Dodoma. Nyingine ni Dayosisi ya Kaskazini Mashariki; Dayosisi ya Kaskazini; Dayosisi ya Kaskazini Kati; Dayosisi ya Pare; Dayosisi ya Meru; Dayosisi ya Mbulu, Dayosisi Mkoani Mara; Dayosisi ya Kati; Dayosisi ya Kaskazini Magharibi; Dayosisi ya Karagwe; Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria; Dayosisi ya Ruvuma; Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria; Dayosisi ya Kusini Mashariki na Dayosisi ya Ziwa Tanganyika.

Pamoja na KKKT kuwa na Dayosisi 24 bado kuna maeneo machache nchini ambayo ni ya misheni. Maeneo ya Misioni ndani ya nchi ni: Zanzibar, Kigoma na Tabora.


Pia KKKT imekuwa ikifanya kazi ya umisheni katika nchi jirani kwa kushirikiana kwa hali na mali na makanisa dada na mashirika ya misheni kutoka ng’ambo. Katika misheni hizo watumishi hutumwa kuanzisha kazi ya misheni lakini pia washarika wa KKKT wamekuwa chachu ya kuanzishwa misioni nchi jirani.


Juhudi za kazi ya misioni ya nje zimesaidia kuzaa makanisa katika nchi jirani ambayo yanalelewa na KKKT. Misioni ya KKKT nje ya nchini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Kongo (DRC), Kenya, Zambia, Msumbiji, Rwanda, Burundi na Uganda.

0 Comments:

Post a Comment