Friday, July 10, 2020

Mwanamalundi: Mtu maarufu katika Historia ya Wasukuma

Jina halisi la Mwanamalundi ni Igulu Bugomola. Huyu alikuwa mcheza ngoma maarufu sana katika kabila la Wasukuma hapa nchini Tanzania. Matamashi ya Mwanamalundi yalikuja baadaye lakini Usukumani alikuwa akifahamika kwa jina la Ngw'anamalundi. 

Alizaliwa na kupewa jina la jina la Igulu Bugomola, Igulu ikiwa na maana ya Mbingu. Alizaliwa akiwa mtoto wa mwisho na wa pekee wa kiume kati ya watoto wanne wa familia ya mzee Bugomola na Ngolo Igulu. 

Ngw'anamalundi alizaliwa katika kijiji cha Mwakubunga Nera katika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza mnamo 1846 vyanzo vingine vinadai alizaliwa mnamo mwaka 1892 na kufariki dunia mnamo mwaka 1936 katika kijiji cha Ngalitu. Igulu (Ngw'anamalundi) alikua na tabia ya uzururaji na haikuwa rahisi kumkuta nyumbani.

Alikua mahiri wa kucheza ngoma, na mara nyingi alifuatwa na kundi la watoto kwa sababu hiyo.

Hali hii iliwachukiza wazazi wengi kutokana na kwamba watoto wao, ambao pia walikuwa wakiwategemea katika kuchunga mifugo, waliwatelekeza mifugo na kumfuata Igulu, hivyo mfugo ya watoto hao ilikuwa ikipotea mara kwa mara.

Walimkebehi kwa msemo wa “Mamirundi galyo lilihumbura bhana bhise” ikiwa na maana ya “mamiguu yake marefu linarubuni watoto wetu”: hatua hiyo ilifuta jina la Igulu na kuwa Ng’wanamalundi.

Mtu huyu aliutingisha utawala wa Wajerumani, alizaliwa katika ukoo wa kawaida akiwa mcheza ngoma mashuhuri.

Watu wengi wamekuwa wakimjadili kwa maoni tofauti, wengine wakimsifu kama shujaa huku wengine wakihusisha uwezo wake na nguvu za giza.

Mjukuu wake wa pili, Kishosha Sitta mnamo mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 80 huko Mwalugulu wilayani Kahama mkoani Shinyanga, alisimulia alivyomfahamu babu yake huyo.

Sitta alianza kueleza kuwa kadiri siku zilivyosonga mbele Ng’wanamalundi alizidi kujiimarisha katika kikundi chake cha ngoma ambayo ilivuta vijana wengi, pia baadaye ilitumika kama jeshi la kukodiwa na Watemi inapotokea vita.

Pamoja na wazazi kumchukia sana, lakini vijana walimpenda na kikundi chake kikubwa cha ngoma kilipendwa na kutumika katika sherehe mbalimbali kwenye familia za Kitemi za wakati huo.

Sitta alisema Ng’wanamalundi na wenzake wawili siku moja walikwenda kwa bibi kizee mmoja kutafuta dawa itakayowasaidia katika shughuli zao za kucheza ngoma, ambapo bibi kizee huyo alikubali kuwasaidia.

“Tujagi lolo ngh’wiporu bana bane akiwa na maana kwamba twendeni sasa porini watoto wangu. Mwanamalundi aliongozana na wenzake pamoja na kizee huyo mpaka porini.

“Walipofika porini bibi Kizee huyo alikamata vinyonga watatu na kuwaekea vichwani, kwa kila mmoja na kuendelea kusonga mbele porini, baada ya kufika katikati ya pori nene, kizee aliwaambia wote wasimame,”

Baada ya kusimama aliamuru kila mmoja achimbe shimo lenye urefu hadi kiunoni, na baada ya kukamilika kwa mashimo hayo aliwaambia wakusanye kuni na kuzitumbukiza.

Baada ya kazi hiyo kukamilika walitakiwa kupekecha moto na kuziwasha zile kuni na moto uliposhika kasi aliwachukua wale vinyonga watatu na kuwawekea dawa mdomoni na kisha aliwatupia ndani ya moto huo, wakateketea wote.

“Ng’wanamalundi na wenzake wakiwa bado wanashangaa vinyonga hao kuungua, ghafla alitokea kifaru kwenye moto huo na kuanza kuwakimbiza hovyo na wote wakasambaritika na bibi kizee wao,”

Ngw’anamalundi alikimbia akapanda juu ya mti, kifaru alifika kwenye shina la mti na kuanza kuliparua kwa hasira na baadaye aliondoka kabla hajafika mbali alimuona yule bibi kizee akikutana na faru huyo.”

Ng’wanamalundi alishuhudia kifaru akimrarua rarua bibi kizee mpaka akafa, kisha kifaru alitoweka kusikojulikana huku akimuacha Ng’wanamalundi asijue la kufanya juu ya mti.

 “Ng’wanamalundi baada ya muda alishuka juu ya mti na kwenda kwenye maiti ya yule bibi kizee, akaamua aibebe mgongoni airejeshe nyumbani, lakini kabla hajafika mbali alisikia sauti ikisema, “Igulu bajahe abiyo akiwa na maana Igulu wenzako wamekwenda wapi”.

Sauti hiyo ilimshtua Ng’wanamalundi ambaye alimshusha bibi kizee mgongoni mwake na akashangaa kumuona akiwa hai asiyekuwa na jeraha lolote, kama alivyokuwa baada ya kushambuliwa na faru.

“Igulu tujage ahante ugo waliwalinaga, akiwa na maana Igulu twende kwenye mti uliokuwa umepanda, Ng’wanamalundi aliongozana na bibi kizee huyo mpaka kwenye ule mti aliyachukua magamba ya mti yaliyokuwa yameparuliwa na faru,”

Baada ya zoezi hilo kukamilika bibi kizee huyo alimtengenezea dawa aliyokuwa akihitaji, na kisha Mwanamalundi alirejea kwao kuendelea na shughuli zake za ngoma aina ya Kahena, ambayo mpaka leo inaendelea kwa jina lingine la Wigashe.

Ng’wanamalundi akiwa katika harakati zake za kujiimarisha katika masuala ya dawa zake za ngoma, alienda kuchimba kwenye pori la Mwandutu huko wilayani Maswa sasa ni Wilaya ya Kishapu, ambalo lilikuwa katika milki ya Mtemi Chalya.

Inaelezwa kuwa baada ya kufika katika pori hilo akiwa na wafuasi wake wakiendelea kuchimba dawa, ghafla alitokea Mtemi Chalya na kumuuliza; “Ubebe nani wakuwilaga kwiza ngh’wiporu lyane” akiwa na maana; “Wewe nani amekuambia kuja kwenye pori langu?”

Mwanamalundi alimjibu; “ Ubebe ulintemi wa banhu pye nu nene nding’wenekele wa maporu pyee.” Akiwa na maana “Wewe ni Mtemi wa watu wote na mimi ni mmiliki wa mapori yote”. Kauli hiyo ilimuudhi Mtemi Chalya.

Kutokana na kauli hiyo Mtemi Chalya aliita jeshi lake kwa lengo la kuja kumkamata, lakini walishangaa baada ya kufika katika eneo waliloelezwa na Mtemi wao kuwa Ng’wanamalundi anatakiwa kukamatwa na kuuawa, lakini walishindwa baada ya kukuta simba wengi sana.

Jeshi hilo na Mtemi ilibidi kukimbia kujiokoa kwani simba hao walianza kuwashambulia, wengine walitawanyika ovyo na baadhi yao wachache tu ndiyo walionusurika.

Lakini cha kushangaza walipofika walimkuta Ng’wanamalundi na wafuasi wake wakimalizia kula chakula nyumbani kwa Mtemi Chalya, ambaye hata yeye alichanganyikiwa na kushindwa kuongea lolote.

Ng’wanamalundi baada ya kumaliza kula chakula kwa Mtemi Chalya aliondoka na wafuasi wake na akapitia kwenye lile pori akachimba dawa zake na kuondoka kwenda kuendelea na maisha yake.

“Katika ngoma zake; Ng’wanamalundi alikuwa na tabia ya kuwatahadharisha mashabiki wake kuacha kwenda wakiwa wamejipaka dawa yoyote ile, anasema. Aliwaambia: “Bing’we akwiziza munho wibilaga bugota bosebose ulu kutora akotora henaha,ulo nsabo akupandika heneha.”

Kauli hiyo ilikuwa na maana nyie asije mtu amejipaka dawa yoyote hapa kama ni kuoa, ataoa hapahapa kama ni mali atapata hapahapa, hata hivyo kuna wale walipuuza kauli hiyo kwa kuja wamejipaka dawa kwa lengo la kujipima uwezo wa dawa zao. Lakini hawakufanikiwa na badala yake walikufa.

Akiwa anaendelea na ngoma yake siku moja wananchi wa Kijiji cha Sekke waliibiwa ng’ombe wengi sana na watu kutoka Kabila la Wamasai ambao walienda kuwahifadhi katika Pori la Mwanima karibu na Kijiji cha Bubiki.

Ng’wanamalundi na kikosi chake waliondoka Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na kuelekea Sekke wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa lengo la kusaidia kuzikomboa ng’ombe zilizoibwa.

Hata hivyo kabla hawajafika uwanja wa vita, Ng’wanamalundi alifanya utabiri wake uliotokana na nguvu ambazo alizipata kutoka kwa Bibi Kizee wa porini. Aliwaambia kuwa kabla ya vita, itatokea mvua kubwa sana na ikikatika watakuja ndege hai aina ya mwewe watakaokuwa wanazungukazunguka kwenye zile ng’ombe na hapo sasa wafuasi wake wakate miti mifupi mifupi (Lubugu).

Utabiri huo ulitimia, kwani mvua ilinyesha kubwa sana na baada ya kukatika wale mwewe walijitokeza wengi sana wakawa wanazunguka kwenye zile ng’ombe na ndipo yale mapigano ya Wamasai na wafuasi wake yalipoanza.

Aliwaeleza kuwa baada ya kuwa na fimbo ya Lubugu wale wenye upinde na mishale watakaa nyuma na kazi yao watakuwa wanazipiga zile ngao za Kimasai na zikidondoka chini ndipo wenye pinde na mishale waanze kushambulia.

Mwanamalundi alipigana hiyo vita ya Wamasai mpaka akazirejesha zile ng’ombe na aliwakimbiza Wamasai hadi kwenye mpaka wa Mto Manonga unaotenganisha Tinde Shinyanga na Nzega mkoani Tabora.

Hapo ndipo ilibainika Wamasai hao walikuwa wametumwa kuiba ng’ombe Usukumani na Mtemi Tinginya wa Busongo Nzega, ambapo baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi na kundi lake walirudi Sekke na kupewa jina la Kishosha Mang’ombe tafsiri ikiwa ni Mrudisha Ng’ombe. Baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi alirudi nyumbani kwao wilayani Kwimba kuoa, lakini bahati mbaya ilimkuta, kwani kila mke aliyejifungua, mtoto alikufa.

Baba yake Bugomola akaenda Ntuzu kwa sasa Bariadi kufanyiwa tambiko kuhusu uzazi kwa mwanaye. Akiwa huko Ntuzu, Bugomola alielezwa mwanaye Ng’wanamalundi hatapata mtoto kwa wake zake alionao.

Hivyo aoe msichana atakayempata upande wa Mashariki ambaye atakuwa akiitwa Nkamba na atazaa watoto watatu; wa kwanza ataitwa Sitta, wa pili Ngassa na wa tatu Marieta. Baada ya kurudi Bugomola, haikumchukua muda mwanaye Ng’wanamalundi akapata msichana akaoa na akaendelea na shughuli yake ya kuendesha kikundi cha ngoma.

Ng’wanamalundi kuwekwa kizuizini akiwa anaendelea na ngoma zake katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, siku moja yeye na kikundi chake walipokuwa wakiburudisha katika maeneo ya Bukumbi mkoani Mwanza, wafuasi wake walipumzika kwenye mti mkubwa ambapo pia kilikuwa Kituo cha Wajerumani, Ng’wanamalundi aliwaambia wafuasi wake waondoke waende kwenye ngoma, wafuasi wake waligoma wakadai wanapumzika kwenye kivuli hicho ili wavute sigara.

Baada ya kuwabembeleza vya kutosha akabaini hawataki kumsikiliza ndipo alipounyooshea kidole ule mti akisema “Ngh’walemelaga hanti gunugo aliyo gumaga,” akiwa na maana “Mmekatalia kwenye mti huo huku ukiwa umekauka.” Ghafla mti huo wote ulikauka.

Kuona hivyo wafuasi wake wakaondoka wote kwenye huo mti wakaenda kuendelea na ngoma yao ambayo walicheza katika eneo la Bukumbi na Busagara karibu na Mji wa Mwanza na walipomaliza walirejea Kwimba.

Akiwa Kwimba alicheza ngoma moja na Gindu Nkima, ngoma hiyo ilikuwa ngumu kwake ilichezwa sehemu za Mwanagwa. Baada ya kuwa amezidiwa Ng’wanamalundi, wapishi wake walimfuata na kumtaka awasaidie namna ya kupata kuni za kupikia.

Kutokana na uharaka aliokuwa nao Ng’wanamalundi alielekeza kidole chake kwenye miti ya minyaa iliyokuwa mbele yake huku akisema “Batemagi pye abenababa mkazugile,” akiwa na maana “Yakateni yote haya mkapikie.”

Baada ya kauli hiyo minyaa yote ilikauka na kuwa kuni na wafuasi wake walikata wakaenda kupikia chakula. Akiwa katika ngoma hiyo wakati huo barabara ya kutoka Shinyanga kwenda Mwanza ilikuwa inachongwa na manamba waliokuwa wakikamatwa na Wajerumani kwa ajili ya kazi hiyo, Gavana wa Kijerumani wa eneo la Mwanza alipita eneo hilo akiwa amepanda punda alikuta kazi imesimama, alipohoji kwanini kazi imesimama alielezwa wananchi wote wamekwenda kwenye ngoma ya Ng’wanamalundi.

Kitendo hicho kilimchukiza sana Mjerumani huyo, ambaye aliondoka akaenda Mwanza na baada ya siku mbili walikuja askari waliomkamata Ng’wanamalundi na kumfunga mnyororo na watuhumiwa wengine walipelekwa Mwanza na kuwekwa gerezani.

Kosa hilo kwa utawala wa Ujerumani lilihesabiwa kuwa ni uhaini wa kupinga utawala wao hivyo alitakiwa kupewa adhabu ya kunyongwa. Kabla hajapelekwa Mwanza, kwa kuwa ilikuwa ni safari ya kwenda kunyogwa, alipelekwa nyumbani kwa wazazi wake kuaga. Alipofika nyumbani kwao alimpa mama yake shoka aliloliweka pembezoni mwa ukuta chumbani na maziwa, huku akitoa maelekezo. “Mayu imbasa yeneye ulu yulina ng’wigulya mumhonatwalwa ulu yika hase mumhonashoka amabele genaya ulu guganda mumhonacha, ulu gita lububhi mumhonasata.”

Akiwa na maana hii shoka ikipanda juu basi nitakuwa nimepelekwa ikishuka chini nitakuwa nimerudishwa.”

Ng’wanamalundi aliendelea kumpa maelekezo mama yake kuwa haya maziwa yakiganda atakuwa amekufa na pindi yakipata utando atakuwa anaumwa, baada ya maelezo hayo Ng’wanamalundi alipelekwa Mwanza gerezani ambako alikutana na Mtemi Makongoro wa Mwanza.

Siku iliyofuata walitolewa wote ambapo walikutana pia na mganga aliyemtabiria kuzaa watoto watatu ambaye naye alikuwa amekamatwa kwa kosa la kupiga ramli iliyosababisha mauaji ya kishirikina.

Asubuhi kila mmoja alisomewa mashtaka yake ambapo Ng’wanamalundi alisomewa mashtaka matatu, shtaka la kwanza kuukausha mti uliokuwa ukitumiwa na maofisa wa utawala wa Wajerumani kama kituo cha kupumzikia huko Bukumbi Mwanza.

Shtaka la pili kuwatungia na kuwaimbia nyimbo mbaya Wajerumani na la tatu ni kukwamisha ujenzi wa Barabara ya Mwanza kwenda Shinyanga. Ng’wanamalundi alidaiwa kuchezesha ngoma eneo la Mwanangwa hali iliyosababisha wafanyakazi wa manamba waliokuwa wakilima barabara hiyo kuacha na kwenda kuangalia ngoma yake hali iliyowachukiza Wajerumani.

0 Comments:

Post a Comment