Saturday, July 4, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: John Adams ni nani?

Julai 4, 1826 alifariki dunia Rais wa pili na miongoni mwa waanzilishi wa taifa la Marekani John Adams. Mpambanaji huyo ambaye alikuwa mwanasheria, mwanadiplomasia, mwandishi alishikilia uongozi wa taifa hilo kutoka mwaka 1797 hadi 1801.

Kabla ya kushika Urais wa taifa hilo Adams alikuwa kiongozi wa Mapinduzi ya Marekani ambapo walijipatia uhuru wao kutoka kwa Waingereza na yeye kuwa Makamu wa Rais wa kwanza wa Marekani.

Adams alikuwa na watu muhimu katika historia ya mwanzo ya taifa hilo ambalo walimsaidia kwa kila hali akiwamo mkewe na mshauri Abigail Adams na Thomas Jefferson.

Akiwa mwanasheria na mwanaharakati  wa kisiasa Adams alikuwa muhamasishaji mkuu wa mapinduzi ya taifa hilo. Pia Adams alisimamia kikamilifu kuwatetea askari wa Uingereza dhidi ya mauaji katika ghasia za Boston mnamo Machi 5, 1770.

Adams kama mzaliwa wa Massachussets alishiriki kikamilifu katika kuandika Katiba ya Massachusetts mnamo mwaka 1780 ambayo ilisaidia pakubwa Katiba ya Marekani ambayo iliipa uhalali wa uhuru wa mwaka 1776 baada ya kupata suluhisho la Bunge la Jimbo la North Carolina.  

Akiwa kama mwanadiplomasia alisaidia kupatikana kwa Mkataba wa Paris mnamo Septemba 3, 1783 ambao ulihitimisha safari ndefu ya vita vya ukombozi nchini Marekani.  Mkataba huo uliweka mipaka baina ya Dola la Uingereza na Muungano wa Shirikisho la Marekani.

Adams alichaguliwa kuwa makamu wa Rais chini ya Rais George Washington. Pia Adams alikuwa rais wa kwanza na pekee kuchaguliwa chini ya chama cha Federalist. Adams alizaliwa Oktoba 30, 1735 kwa wazazi John Adams Sr. na Susanna Boylston.

Baada ya kustaafu kuongoza taifa hilo alirudi zake huko Peacefield ambako alijikita katika masuala ya kilimo. Pia alimuunga mkono James Madison Jr. wakati akiwania Urais wa taifa hilo ambapo mwaka 1812 alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani.

Adams aliunga mkono vita ya mwaka 1812 baina ya Marekani na majeshi ya Uingereza na washirika wake ambayo ilipiganwa katika bahari ya Pasifiki na Atlantiki pia Mashariki na katikati ya Marekani.

Abigail alifariki kwa typhoid mnamo Oktoba 28, 1818  katika nyumba ya Quincy huko Peacefield. Adams alifariki dunia katika maadhimisho ya miaka 50 ya Azimio la Uhuru. Alifariki dunia saa 12:20 jioni.

Maneno yake ya mwisho kabla ya kifo chake yalihusisha pia shukrani zake kwa rafiki wake wa siku nyingi na mpinzani Thomas Jefferson. Adams hakuwa na taarifa kwamba Jefferson alikuwa amefariki dunia saa chache kabla. Jefferson alifariki siku hiyo hiyo majira ya 6:50 mchana akiwa na umri wa miaka 83 huko Virginia.

Akiwa na umri wa miaka 90 Adams aliweka rekodi ya Rais aliyeiongoza Marekani kuishi muda mrefu kabla ya Rais Ronald Reagan kuivunja mnamo mwaka 2001. Reagan ambaye ni Rais wa  40 wa Marekani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 93 mnamo Juni 4, 2004 huko Los Angeles, California

0 Comments:

Post a Comment