Thursday, July 2, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Nostradamus ni nani?

Julai 2, 1566 alifariki dunia mnajimu wa Ufaransa Michel de Nostredame maarufu Nostradamus. Mnajimu huyu anajulikana sana kutokana na kazi zake za utabiri ambazo alizifanya wakati huo kwa matukio yajayo.

Mashairi 942 aliyaandika kuhusu siku zijazo na kujichotea umaarufu mkubwa hususani kupitia kitabu cha Les Propheties. Kitabu hicho kilichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1555 na baada ya kufa kwake kilianza kupatikana kwa shida. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 62 huko Salon-de-Provence nchini Ufaransa.

Nostradamus alifariki dunia kwa maradhi ya gauti yaliyogeuka na kuwa edema (kuvimba miguu, miguu kujaa maji). Maumivu makali kutokana na gauti yalimfanya Nostradamus ashindwe kutembea. Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huo, Nostradamus alimwita mwanasheria wake kuhusu mali zake kwa wanafamilia na kumpa maelekezo.

Julai 1, 1566 alimwambia Katibu Muhtasi wake Jean de Chavigny “Hutaniona nikiwa hai kutakapokucha.” Siku ya pili yake ilitangazwa kwamba Nostradamus amefariki dunia akiwa amelala sakafuni pembeni ya kitanda chake na kochi la kukalia.

Nostradamus alizikwa katika kanisa la Wafransiska huko Salon na baada ya mapinduzi ya Ufaransa eneo hilo liliwekwa Chuo kinachofahamika kama Saint-Laurent ambako kaburi lake lipo hadi leo.

Mnamo mwaka 1531 Nostradamus alialikwa huko Agen na Jules-Cesar Scaliger ambaye alikuwa msomi na daktari wa Kiitaliano aliyekuwa akifanya kazi zake nchini Ufaransa. Akiwa huko ndiko alikopata mke ambaye hakufahamika jina lake mara moja huenda ni Henriette d’Encausse ambaye walizaa naye watoto wawili.

Mnamo mwaka 1534 mkewe huyo na watoto walikufa na inadaiwa kwa maradhi ya tauni. Baada ya vifo aliendelea kusafiri huko na huko nchini Ufaransa na baadaye nchini Italia. Alirudi nchini Ufaransa mnamo mwaka 1545 akiwa na tabibu mahiri Louis Serre ambaye alifahamika kutokana na mapambano yake dhidi ya ugonjwa wa tauni jijini Marseille, baadaye alisaidia kwenye mji aliozaliwa Nostradamus wa Salon-de-Provence na mji mkuu wa Ufaransa Paris.

Hatimaye mnamo mwaka 1547 aliamua kusalia Salon-de-Provence katika nyumba ambayo ipo mpaka leo. Akiwa hapo alimwoa mama mmoja mjane tajiri aliyefahamika kwa jina la Anne Ponsarde. Akiwa na mwanamke huyo walizaa watoto sita (wa kike watatu na wa kiume watatu).

Kati ya mwaka 1556 na 1567 Nostradamus na mkewe walipata theluthi moja ya hisa katika mradi mmoja mkubwa ulioratibiwa na Adam de Craponne ambao ulikuwa umejikita katika utengenezaji wa mfumo wa umwagiliaji wa Canal de Caponne ili kumwagilia eneo lililokuwa halina maji la Salon-de-Provence. Nostradamus alizaliwa kati ya Desemba 14 au 21  mwaka 1503.

Nostradamus alikuwa miongoni mwa watoto tisa wa mzee Jaume (Jacques) de Nostredame na mama yake aliyefahamika kwa jina la Reyniere mjukuu wa Pierre de Saint-Remy ambaye alikuwa daktari huko Saint-Remy. Kwa asili familia ya Jaume ni Wayahudi.

0 Comments:

Post a Comment