Wapo wanaodhani kujua saikolojia ni mpaka uingie dawati darasani kwa miaka kadhaa lakini bado ukweli uko pale pale kwamba wewe ni mwanasaikolojia. Hebu fikiria, ni mara ngapi umeweza kubaini kuwa mtu fulani hana furaha ama ana huzuni ama amekasirika na kadhalika? Umejuaje?
Unapoweza kujifunza kinachoendelea katika ufahamu wa mtu,
ukajua kinachosababisha awaze hivyo anavyowaza, ama awe na tabia hizo
alizonazo, basi unajihusisha moja kwa moja na elimu nafsi ama saikolojia katika
urahisi wake.
Kuna ukweli fulani kwamba tabia alizonazo mtu zimetokana na
mambo mengi. Tabia ni zao la muunganiko wa vibeba urithi kutoka kwa baba na
mama yako, vilivyobebwa katika mbegu na yai vilivyoungamana kukutengeneza wewe.
Pili, tabia ni zao la mwingiliano wako na mazingira yako.
Dhana ya mazingira inaanzia na watu unaoishi nao kwa karibu
mfano wazazi wako, yaya aliyekulea, watoto wenzio na kuendelea mpaka hata mambo
kadha wa kadha uliyokumbana nayo tangu ukiwa tumboni mwa mama yako. Vyote hivyo
katika ujumla wake, vimeshiriki katika kutengeneza tabia uliyonayo leo.
Kwa ufupi tabia na uwezo au haiba ya mtu inatokana na asili
(yaani nature ) na mazingira (yaani nurture). Kila binadamu anazaliwa na uwezo
fulani (potential) lakini ili uwezo huo ufikie kiwango chake cha juu (maximum
potential) basi lazima kuwepo na mazingira yanayoruhusu ukuaji huo.
Lakini pia asilia au mazingira huweza kuweka kipingamizi
(limitation) dhidi ya uwezo wa mtu. Kwa mfano hata mtu apate mazingira mazuri
namna gani kama hana asili ya urefu (yaani genes for tallness) mtu huyo hawezi
kuwa mrefu.
Sanaa ni ufundi wa kuwasilisha fikra na mawazo ya binadamu
kwa njia aidha ya kuchora, kuchonga, ufinyanzi, uimbaji, uigizaji na vitu
vingine vifananavyo na hivi.
Maana nyingine ya Sanaa ni uzuri wa umbo lililosanifiwa na
likasanifika na kuleta maana kwa jamii. Na anayefanya kazi hiyo ni msanii.
Unaweza kuzaliwa ukawa na haiba ya kuwa msanii na ukaendelea kusimama nayo
maisha yako hadi unapofikia mwisho wa maisha yako duniani.
Miongoni mwa watu ambao huwezi kupinga au kwenda kinyume na
hili ni Chifu Athumani Omary Mwariko ‘Mhelamwana’.
Chifu Mwariko amekuwa maarufu sana katika mitandao ya kijamii
katika siku za hivi karibuni kutokana na maoni aliyoyatoa kuhusu masuala
mbalimbali wakati wa upigaji wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi
(CCM) mjini Moshi zilizofanyika Julai 20, mwaka huu.
Chifu Mwariko alikuwa miongoni mwa watu waliotia nia ya
kuwania kuteuliwa ubunge ndani ya chama hicho kwa ajili ya kupeperusha bendera
ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao kwa jimbo la Moshi Mjini. Ukumbi ulizizima kwa
shangwe wakati Chifu Mwariko alipoingia katika ukumbi kwa ajili ya kuomba
ridhaa kwa wapiga kura kwa wajumbe wa mkutano wa chama hicho.
Mwariko aliweka bayana kuhusu haiba yake kuwa yeye ni
mchangamfu na pia ni mtu wa Sanaa lakini kabla ya hapo alipendekeza kuwapo kwa
noti ya shilingi 50,000 au shilingi 100,000 ambayo itakuwa na picha ya Rais wa
awamu ya Tano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutokana kazi alizozifanya.
“Mimi ni msanii katika sehemu ya Utamaduni na Sanaa,
nilizungumza nikasema mkinichagua nitashirikiana na Mhe; Rais Dkt. Magufuli
kutokana na kazi kubwa alizozifanya kwa kipindi chake cha miaka minne, sasa
kitu cha kumzawadia tunaomba kuanzia sasa itengenezwe noti mpya ya sh 50,000 ya
magufuli au ya 100,000.
Katika suala linalohusu Sanaa Chifu Mwariko aliweka
kinagaubaga kuhusu utamaduni wa Mtanzania. Chifu Mwariko alisema kabla ya
kuwapo kwa wazungu katika ardhi ya Afrika, kama wenyeji wa bara hili kulikuwa
na namna ya maisha waliyokuwa wakiishi.
Aidha ujio wa wazungu ulizifanya mila na desturi zikose mvuto
lakini Chifu Mwariko alisisitiza kuwa atakapopata ridhaa ya kuteuliwa
atapendekeza mila hizo zirudi katika mstari miongoni mwa hizo ni matumizi ya
njia za asili kutibu matatizo badala ya kusubiri dawa za kisasa ambazo kuna
wakati zimeshindwa ikiwamo kina mama kuwa wagumba.
“Jambo la pili nitakwenda kuwatetea akina mama waliokuwa
wagumba kupitia wizara ya utamaduni, na kupitia wizara hii tutafanya kila
namna,” alisisitiza Chifu Mwariko.
MLIMA KILIMANJARO KUWEKWA PAZIA
Wakati wa kuomba kura hiyo Chifu Mwariko aliwastaajabisha wengi pale aliposema Mlima mrefu kuliko yote barani Afrika Mlima Kilimanjaro ambao una mita 5895 atapambana kuuwekea pazia ili anayetaka kuuona aweze kufunguliwa hivyo kuiiingizia mapato serikali ya Tanzania.
“Mkinipa kura wizara ya utamaduni, Mlima Kilimanjaro tutauwekea pazia ili kila anayetaka kuuona hata kama hawezi kupanda mlima huo aweze kulipia ili kuongeza mapato ya nchi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla. Haiwezekani watu wanatoka nje na kuja kuuona mlima bila hata ya kulipia ni vyema ukafunikwa na pazia ili atakayetaka kuuona aweze kulipia kwanza kisha pazia linafunuliwa tayari ameshaingizia mapato serikali,” alisema Chifu Mwariko.
Chifu Mwariko aliongeza kuwa Watu wamekuwa wakitoka majumbani mwao na kuuona mlima bila hata ya kuupanda “Hii tunapoteza fedha nyingi na kuishia kulalamika kwamba mzunguko wa fedha hakuna, fedha zitapatikanaje wakati mtu anauona tu mlima bila kulipia? Endapo kama mtanipa ridhaa ya kuwa mwakilishi wenu Bungeni nitakwenda kupigania jambo hili ili huu mlima lazima uwekewe pazia kubwa ili uchumi wa wanakilimanjaro uweze kukua.”
Kwa ufupi ni kwamba Chifu Mwariko ndiye aliyetengeneza kifimbo cha baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1922-1999) na kukabidhi kwa ajili ya uongozi wa taifa hili. Licha ya kwamba kwenye kura hizo aliambulia kura moja lakini ni mtu wa muhimu katika jamii ya Watanzania kutokana na haiba yake hususani Sanaa yake ya kuwakusanya watu na kuzungumza nao.
Pia Chifu Mwariko ndiye aliyependekeza Chama cha Hakimiliki cha Tanzania (COSOTA) kirudishwe katika Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ambapo hapo awali ilikuwa Wizara ya Viwanda na Biashara. Hivyo unapomzungumzia Chifu Mwariko au maarufu Mhelamwana basi unamzungumzia mtu muhimu na urithi ambao unapaswa kulindwa na kupewa kipaumbele.
0 Comments:
Post a Comment