Tuesday, July 7, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Alfredo di Stefano ni nani?

Julai 7, 2014 alifariki dunia mchezaji wa soka na kocha wa Kimataifa wa Argentina na Hispania Alfredo di Stefano. Jina lake la ukoo ni Laulhe alizaliwa jijini Buenos Aires, Argentina mnamo Julai 4, 1926.

Di Stefano kama ambavyo alikuwa akifahamika na wengi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 88 jijini  Madrid nchini Hispania ambako alikuwa akiishi hadi kifo chake. Mnamo Novemba 5, 2000 alitunukiwa Urais wa Heshima wa klabu ya Real Madrid.

Akiwa na umri wa miaka 79 Di Stefano alikutwa na shambulio la moyo hiyo ilikuwa Desemba 24, 2005. Mnamo Mei 9, 2006 Uwanja wa Alfredo di Stefano ulizinduliwa katika jiji la Madrid. Uwanja huo ndio uwanja wa mazoezi wa klabu yake ya Real Madrid.

Katika uzinduzi huo kulichezwa mechi  baina ya Real Madrid na Stade de Reims ikiwa ni mechi nyingine ya ukumbusho baada ya kukutana kwenye fainali ya Kombe la Ulaya ambalo Real Madrid ilishinda mnamo mwaka 1956.

Mechi hiyo ya uzinduzi wa uwanja huo matokeo ni kwamba Real Madrid ilishinda kwa mabao 6-1. Mabao yalifungwa na Sergio Ramos, Antonio Cassano ambaye alifunga mawili, Roberto Soldado alifunga mawili na Jose Manuel Jurado.

Mnamo Julai 5, 2014 Di Stefano alipata shambulio la moyo kwa mara nyingine hivyo ikabidi akimbizwe katika hospitali ya Gregorio Marañón iliyopo jiji Madrid ambao alifariki dunia. Julai 8, 2014 jeneza lake liliweka hadharani katika dimba la Santiago Bernabeu.

Rais wa klabu hiyo Florentino Perez na nahodha wa klabu hiyo wakati huo Iker Casillas walikuwa miongoni mwa waliohudhuria tukio hilo. Kutokana na kifo cha nyota huyo watu mbalimbali walitoa salamu zao za rambirambi wakiwamo Alex Ferguson, Johan Cruyff, Pelé, Cristiano Ronaldo, Diego Maradona  na Bobby Charlton.

Katika mchezo wa Kombe la Dunia hatua ya nusu fainali mnamo Julai 9, 2014 baina ya Argentina na Uholanzi Di Stefano alipewa heshima ya dakika moja ya ukimya huku wachezaji wa Argentina wakivaa vitambaa vya rangi nyeusi ikiwa ni kuonyesha heshima.

Klabu ya River Plate ya nchini Argentina na Millonarios ya Colombia ziliratibu mechi ya kirafiki kwa ajili ya kutoa heshima kwa nyota huyo ambaye aliwahi kuzitumikia timu hizo. Mechi hiyo ilichezwa Julai 16, 2014 katika dimba la Millonarios El Campin.

Di Stefano alipendwa sana alipokuwa nchini Hispania baada ya kufungiwa kuitumikia timu ya Argentina na ndio sababu iliyomfanya atimkie nchini Hispania kwa ajili ya kuendeleza soka lake.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) lilikataa kumwekea vikwazo Di Stefano baada ya nyota huyo kupata uraia wa Hispania mnamo mwaka 1956 licha ya shinikizo kutoka kwa Chama cha Soka cha Hispania.

Mechi ya kwanza nchini Hispania alicheza Januari 30, 1957 ambayo ilikuwa ya kirafiki. Ilichezwa jijini Madrid ambapo Di Stefano alifunga hat trick katika ushindi wa mabao 5-1 hivyo akawa mchezaji wa kwanza kuzaliwa nje ya Hispania kucheza kikosi cha kwanza cha timu ya taifa.

Mechi yake ya kwanza ya kimataifa kabla ya kutimkia nchini Hispania ilikuwa Desemba 4, 1947 akiwa katika jezi ya Argentina alicheza dhidi ya Bolivia. Mchezo ulichezwa katika dimba la George Capwell huko Ecuador kwenye michuano ya Bara la Amerika Kusini sasa Copa America.

Alifunga bao lake la kwanza la kimataifa katika mchezo huo kwenye ushindi wa mabao 7-0. Di Stefano alifunga mabao mengine matano katika katika michuano hiyo ya mwaka 1947 ikiwamo hat trick dhidi ya Colombia.

Argentina ilifanikiwa mwaka huo kutetea taji hilo ambalo ilishinda mwaka mmoja nyuma katika ardhi ya nyumbani. Mechi sita tu zilitosha kuwa Di Stefano zilionyesha dhahiri kuwa muhimu katika timu ya taifa.

Sasa balaa lilijitokeza katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia la mwaka 1950 dhidi ya Brazil mnamo mwaka 1949 baada ya Di Stefano kugombana kwenye mechi hizo ambazo ziliifanya Argentina kujitoa kwenye mechi hizo za kufuzu. Ilikuja tena kwenye michuano ya mwaka 1953 ya Amerika Kusini.

Katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia mnamo mwaka 1954 FIFA ilimfungia Di Stefano kuhudumu katika timu ya taifa ya Argentina. Mafanikio makubwa ngazi ya klabu aliyapata akiwa na Real Madrid sambamba na Francisco Gento na José María Zárraga waliisaidia Los Blancos kutwaa mataji matano ya Ulaya ngazi ya klabu (Ligi ya Mabingwa).

Akiwa na Los Blancos alipewa jina la Saeta rubia kutokana na uwezo mkubwa, nguvu, akili ya mpira, ubunifu, stamina, mbinu za mpira na macho ya mpira zaidi ya yote Di Stefano alikuwa na uwezo wa kucheza nafasi yoyote uwanjani. Katika La Liga alifunga mabao 216 katika mechi 282 kati ya mwaka 1953 na 1964.

Akiwa sambamba ya Cristiano Ronaldo, Di Stefano anakuwa mfungaji bora katika mechi za El Clasico.

Alianza maisha yake ya soka akiwa na umri wa miaka 17 mnamo mwaka 1943 katika klabu ya River Plate. Alitunukiwa tuzo ya Ballon d’Or kwa mchezaji bora wa Ulaya wa mwaka mnamo mwaka 1957 na 1959.

Alipotoka Real Madrid alienda kumalizia soka lake huko Espanyol mnamo mwaka 1964 akiwa na umri wa miaka 40. 

0 Comments:

Post a Comment