Chama cha TLP
kimeendelea kusisitiza hatua yake ya kumteua Rais John Pombe Magufuli kuwania
urais licha ya kunyoshewa kidole cha lawama na watu mbalimbali kuhusu uamuzi
wake kilichoamua kupitia halmashauri kuu ya chama hicho mnamo Julai 2019 huku
kikikazia mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyevuliwa uanachama wa Bernard
Membe kuwa hapaswi kupata kura zaidi ya 10 katika kinyang’anyiro hicho mwaka
huu.
Mbali na hilo chama hicho kimedai kuwa upinzani nchini haujaenda likizo upo imara na kukanusha taarifa mbalimbali zinazoelekezwa kwao kuhusu hatua ya kumuunga mkono Magufuli kuwa wao ni vibaraka wa CCM.
Hayo yalijiri wakati
Mwenyekiti wa TLP taifa Dkt. Augustino Lyatonga Mrema alipokuwa akitangaza azma
ya chama chake kuingia katika uchaguzi wa mwaka huu kushindana na vyama vingine
kwenye ngazi ya udiwani wa Moshi Mjini.
Mrema alisema wao
kama TLP sio vibaraka katika kuamua hivyo katika nafasi ya urais isipokuwa
uzalendo ndilo jambo kubwa lililowasukuma kufanya hivyo baada ya kuona kazi
zinazofanywa na Rais John Pombe Magufuli.
“Tulichukua ilani ya
TLP tukaona serikali ya Magufuli imetekeleza, sio kwamba hatuna mgombea tunaye.
Lakini Magufuli hana mbadala tukakubaliana kidemokrasia, sasa wengine
wanafikiri kwasababu Mheshimiwa Rais alinipa uenyekiti wa bodi ya Parole eti
kwamba mimi nalipa fadhila. Jamani mnanionea,” alisema Mrema.
Aidha Mrema
aliwataka wana CCM wasimame kidete kulinda kura zao na wao kama TLP watahakikisha CCM haipotezi kura yake endapo
Membe ataingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwani ni miongoni mwa watu ambao
wamekuwa na kiburi kutokana na fedha walizonazo hali ambayo inaweza kuyumbisha
demokrasia ya Tanzania akipewa nafasi ya kuongoza nchi.
“Membe kwanini apate
kura hata kama ni kumi, CCM lazima watuambie imekuwaje Membe apate hizo?
Nasikia kuna pesa zinakuja Tanzania kupitia Kenya kwa njia za siri kwa ajili ya uchaguzi huu, hizo
zitayumbisha demokrasia ya nchi yetu, Tunataka upinzania ambao utakuwa ukikosoa
serikali bila kutukana,” alisisitiza.
Mbali na hilo Mrema
alisema katika kata 21 moja za Moshi Mjini wamesimamisha madiwani 11 katika
kata ili kuonyesha kwamba wao wanaweza kufanya vizuri kama vyama vingine
kutokana na wagombea wake.
“Wapinzani wako
hawajaenda likizo na sio kwamba Magufuli atapita kirahisi, katika ngazi za udiwani
tunasimama imara kushindana ipasavyo,” aliongeza Mrema.
Kata ambazo TLP
imesimamisha wagombea kwa tiketi ya chama hicho ni Njoro, Mji Mpya, Ng’ambo,
Kiboriloni, Bondeni, Boma Mbuzi, Pasua, Nganga Mfumuni, Majengo, Miembeni na
Longuo.
Katika mkutano wake
na wanahabari Mrema aliwakaribisha wanachama waliokimbia Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) na kuwania udiwani kwa tiketi ya TLP ambao ni Thomas
Senzige (Mji Mpya), Petro Mbonea Mbwambwo (Bondeni), Severin Jacob Dafi (Njoro
Sokoni) na Rajab Yassin Magema (Ng’ambo).
Aidha Mrema
aliwasisitizia wagombea wake kuwa ushindi wao unaanza na mwonekano wao na ilani
ya uchaguzi ya chama na namna chama kilivyojipanga kifedha ndio sababu ya
ushindi wao.
0 Comments:
Post a Comment