Monday, July 27, 2020

Mwandishi wa habari Shao aongoza kura za maoni CCM Mwika Kaskazini

Mwandishi wa habari na mtangazaji wa Redio Sauti ya Injili Samwel Shao amekuwa miongoni mwa wanahabari wa kwanza mkoani Kilimanjaro kuongoza kura ya maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao kwenye ngazi ya udiwani.

Hayo yanajiri ikiwa ni siku chache baada ya kauli ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mkajanga kusema waandishi wa habari watapaswa kuacha kazi yao ya habari endapo wataenda kuwania nafasi za kisiasa ili kutopoteza misingi ya habari kwa ujumla.

Shao ameiongoza kura za maoni katika Kata ya Mwika Kaskazini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro akipata kura 26 kati ya 78 zilizofanyika Julai 25 mwaka huu na kutangazwa na Msimamizi wa Kura za Maoni wa chama hicho Bariki Moses Kimaro.

Aliyemfuata mwanahabari huyo ni Merry Shao aliyepata kura 17 akifungamana na Wilbard Shao aliyepata kura 17. Nafasi ya Nne imeshikwa na Hubert Mariki aliyepata kura 7, Harold Kimaro kura 6, Monyaichi Mlaki kura 5, Daniel Mgase kura 1 na Meja Jesse Jeremia akiambulia patupu katika kura hizo za maoni. Mtia nia aliyefahamika kwa jina la Nelson Eliya Massawe hakuonekana katika kura hizo za maoni.

Mwenyekiti wa kikao hicho cha kata cha kura za maoni ndani ya CCM Wilbard William Shao ambaye ni Mwenyekiti wa Tawi la Mlimbouwo alisimamia kikao hicho ambapo alisema watia nia walikuwa 9 lakini waliothibitisha ushiriki wao ni 8.

Katibu Kata wa CCM Mwika Kaskazini Leonard Mlaki alisema kumalizika kwa kura hiyo ya maoni haimaanishi aliyeongoza ndiye ameshinda isipokuwa amewataka wajumbe wa mkutano huo kusubiri uamuzi wa chama kama ilivyotangazwa mpaka jina litakaporudi ili kupambana na vyama vingine katika uchaguzi wa mwaka huu.

Awali uchaguzi huo ulianza na uandikishaji wa wajumbe wa mkutano huo ulitawaliwa na uwazi na utulivu wa hali ya juu hadi akidi ilipotosha ndipo zoezi zima lilianza kufanyika kwa watia nia kujinadi.

Wajumbe wa mkutano huo walisimama kwa dakika moja kuomboleza kifo cha Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania Hayati Benjamini William Mkapa kilichotokea Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam.

Kura ya maoni ya kuchagua majina yatakayokwenda katika Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya kwa kata ya Mwika Kaskazini ilifanyika kuanzia saa 4 asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari ya Mwika ambapo Mkuu wa Shule hiyo Damian Petro  alifungua mkutano huo kwa kuwakaribisha na kuwatakia kila la kheri katika mchakato mzima wa kura ya maoni.

Wakati wa muda wa Kampeni ulipofika kila mtia nia alipata nafasi ya kuzungumzia atawafanyia jambo gani wakazi wa Mwika Kaskazini ambapo mwandishi wa habari Shao alisisitiza ulazima wa kutetea shughuli za kimaendeleo ikiwamo suala la maji na barabara katika kata hiyo.

Wanahabari wengine mkoani Kilimanjaro walioingia katika kinyang’anyiro cha kura za maoni ndani ya CCM ni Nakajumo James (Mabogini), Gift Mongi (Mwika Kusini) na Venance Maleli (Rombo).










0 Comments:

Post a Comment