Nilipofika nilimkatisha muuzaji yule mazungumzo yake na mteja wake lakini nahisi walikuwa wakizungumza na mtu wanayefahamiana naye, kwa mbali walikuwa wakizungumzia suala la kubeti, kijana huyo alikuwa akishawishiwa na mwenzake kwamba jioni wakutane akamfundishe namna wanavyobeti.
Kilichonivutia zaidi ushawishi wa kijana yule aliyeonekana amezidiwa na kileo (harufu ya ‘kiroba’ ilikuwa ikimtoka) huku macho yakiwa mekundu kama ‘ugoro wa subiana’
Nikamuungisha muuza samaki kiasi ambacho niliona kitanitosha siku hiyo kwani ilikuwa yapata saa 8 mchana, wakati nataka kutoka nikawauliza wanafaidika vipi na ‘mikeka’?
Yule aliyekuwa akimshawishi alionekana kuwa na shauku ya kuongea akasema “hivi karibuni nimejishindia laki mbili hapo nyuma nilikuwa napoteza lakini nilipokuja kuujua mchezo nimekuwa nikifaidika hata baiskeli ya gia nimenunua.”
Ukweli ni kwamba ukipita maeneo mbalimbali utawaona vijana wengi wakiwa na peni na karatasi zenye mechi za siku husika.
Pia kinachostaajabisha ni kwamba vijana wanaotafuta maisha kwa biashara ndogondogo au unaweza kuwaita wajasiriamali katika mitaa mbalimbali nchini ndio waathirika wakubwa wa ‘mikeka’.
Kibaya zaidi unapoziona sare za shule katika maeneo ya ‘ku-beti’ ndio majanga zaidi, unapomwona kijana akitoroka vipindi vya darasani na kwenda ‘kushona mkeka’ au unapomwona kijana muuza maandazi na kashata anayomaliza mtaji wake ambao ‘unaliwa na mbuzi’ ndicho kinachotia simanzi.
Msingi wa makala haya ni kutaka kuangazia kama sheria kanuni na taratibu za michezo hii ya kubahatisha zinafuata na kusimamiwa kikamilifu, hususani kwa washiriki wa michezo hiyo. Hii inatokana na ukweli kwamba maendeleo makubwa ya simu yamekuwa makubwa ambapo mshiriki anaweza ku-beti hata akiwa nyumbani kwake, au kichochoroni.
Jambo la kuzingatia hapa ambalo litaufanya mjadala huu uendelee zaidi je, watanzania wanaelewa kuwa ‘mikeka’ ni maalumu kwa ‘leisure’ na ‘entertainment’ au wao wanaelewa nini kuhusu hili hususani kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18.
Pia majina ya wahusika yatahifadhiwa hususani wale walio chini ya umri wa miaka 18. Aidha kinachovutia zaidi ni kwamba hata serikali inatambua kuwa michezo ya kubahatisha ni chanzo kikubwa cha mapato.
Hadi sasa tumeona namna serikali na mamlaka zake inavyolichukulia suala hili la ku-beti, sheria za michezo hii ya kubahatisha kupitia Bodi ya Michezo ya Kubahatisha na namna ya utoaji wa leseni kwa maduka ya ku-beti ambapo Marekebisho ya Sheria ya Leseni (Business Licensing Act no. 25 of 1972) yaliyofanyika mwaka 2003 kupitia Finance Act No. 15 ya mwaka 2003, kifungu 5(1)(f), yaliondoa michezo ya kubahatisha katika orodha ya uhitaji wa leseni za biashara, isipokuwa leseni inayotolewa na Gaming Board.
Pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inavyopambana katika ukusanyaji wa kodi, kwa kuainisha kodi za aina mbili Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Tax)- Hii ni kodi anayotozwa mwendeshaji wa mchezo wa kubahatisha kutokana na mapato yake yatokanayo na michezo ya kubahatisha; na Kodi ya Michezo ya Kubahatisha kwenye Zawadi (Gaming Tax on Winnings), ambayo anatozwa mchezaji baada ya kushinda zawadi ya mchezo wa kubahatisha.
Sasa leo tunaendelea na namna wazazi au walezi au watu wenye familia wanavyolichukulia suala la ku-beti. Kinachoonekana ni kwamba wanaume ambao wamekuwa wakiona kwa idadi kubwa katika maduka ya ku-beti wengi wao wana familia zao au wazazi kwa maana wana watoto; hivyo wamekuwa wakiwadanganya hata wenza wao, watoto wa mjini wanasema ‘wanaingiza mjini’ kwa kujifanya hawana fedha za matumizi au nauli lakini ukweli wa mambo ni kwamba wanataka fedha za michezo hizo baada ya wengine kupoteza kila wanapobeti.
“Unajua ndugu kama ni ulevi basi ku-beti we acha tu, yaani hata kujinasua nashindwa, kuna wakati namdanganya hata mke wangu kwamba pesa niliyonayo ni kidogo ili nika-beti baadhi ya mechi,” anasema mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 42 ambaye ana familia ya mke na watoto wawili.
Aliongeza kusema mwanaume huyo ambaye anaonekana kupenda mchezo wa soka, “ Awali wakati naanza niliona kawaida tu kutokana na ushawishi ambayo baadhi ya marafiki zangu waliufanya kwamba ni mojawapo ya chanzo cha mapato.”
Aidha mwanaume huyo anayefanya kazi ya ufundi mekanika katika gereji moja ya mtaani alisema watanzania wengi wameuchukulia kama sehemu ya kutoka kimaisha na ndio maana watu wa chini ndio wanaonekana kwa wingi katika vituo vya ku-beti.
Hata hivyo alitoa ushauri kwa familia ambazo zimekuwa sugu katika suala la ku-beti kujitahidi kuzijali badala ya kuzipunja huduma muhimu pia kupanga ratiba ya kwenda ku-beti na sio kila wakati kwani wengi hupendelea ‘live betting’ ambayo huweza kusababisha kurudi usiku wa manane hali ambayo ndoa zao zimeingia matatani.
Mzazi mmoja wa maeneo ya Soweto mjini Moshi mkoani Kilimanjaro aliyejitambulisha kwa jina Baba Sophia anasema, “ Mimi nilikuwa mtu wa ku-beti nikafikia mahali nikaacha kwani nilipata ushauri kutoka kwa rafiki yangu mmoja Mombasa, Kenya kuhusu madhara ya ku-beti nikamwelea lakini sio rahisi kuacha, alichofanya alikuwa akinisisitiza kusoma vitabu mbalimbali vyenye maudhui ya kujitambua wewe ni nani; ndugu mwandishi vimenisaidia sana na uraibu wa ku-beti.”
Alipoulizwa kuhusu namna ya kuwasaidia watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambao wamejikita katika ku-beti anasema, “Bado jamii ina kazi kubwa ya kufanya kuhusu rika hilo kwani maadili kwa sasa yamekuwa chini sana kuanzia kwa wazazi wenyewe jambo ambalo linaweka ugumu wa kuwadhibiti, serikali haiwezi kufanya peke yake kudhibiti watoto hao lazima elimu kuhusu malezi bora ipite katika familia zetu, bila hivyo itakuwa kutwanga maji kwenye kinu.”
Kwa upande wake mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Flora ambaye ni mama wa watoto watatu anatoa ushuhuda wa kijana wake wa kiume, “ Mwanangu mimi ana umri wa miaka 15, nilimfuma siku moja akiwa na simu ndipo nilipoanza kujua kitu gani anachokifanya kwenye simu. Awali nilijua labda ni mambo ya mapenzi si unajua umri wa kubalehe huo lakini nikastaajabu kuona ana-beti japokuwa sikuwa na ufahamu sana nikampata kichapo ndipo aliposema nini ambacho huwa anafanya kwa kutumia simu hiyo.”
Bi. Flora anaongeza kuwa baada ya kumbana zaidi alijua mtu aliyempa simu kwani yeye kama mzazi hakuwa kumnunulia simu mwanaye hivyo akamfuata na kumwelekeza kuwa asimharibie kijana wake kwani anahangaika kumlea.
“Ku-beti huku kwa vijana wetu kunawaharibu hata kama serikali inachukua mapato lakini inapaswa kuliangalia kwa kina, wakiwa kwenye maeneo yao wanaweza kujifunza tabia mbaya, watakuwa ni watu wasiopenda kufanya kazi za maana ili kufanikiwa. Naona wengi wanaona ku-beti ni kama mlango wa mafanikio, kitu ambacho mimi nakataa kabisa,” anaongeza Bi. Flora
MAKALA NYINGINE ZA SPORTS BETTING au KU-BETI
0 Comments:
Post a Comment