Wednesday, September 30, 2020

Jamii ipambane kuzuia watu Kujiua

 
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) takribani watu laki 8 hadi milioni 1 hujiua kila mwaka kwasababu mbalimbali. Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Kifungu cha 216 na 217: Kushawishi mtu Kujiua au Kujaribu Kujiua ni Kosa la Jinai.

Kifungu cha 216 kinafafanua: Mtu yeyote ambaye; (a) anasababisha mtu mwingine ajiuwe; au (b) anamshauri mtu mwingine ajiuwe na akamshawishi kufanya hivyo; au (c) anamsaidia mtu mwingine ajiuwe, atakuwa anatenda kosa na atahukumiwa kifungo cha maisha.

Kujaribu kujiua, kifungu cha 217 kinafafanua: Mtu yeyote anayejaribu kujiua ana hatia ya kosa.

Mwezi Septemba kila mwaka umekuwa maalum kwa ajili ya kampeni ya kuelimisha umma duniani kote kuhusu matukio haya ya kujiua. Nchini Tanzania mnamo mwaka 2018 ndani ya wiki moja matukio matatu ya askari polisi kujiua yaliripotiwa.

Kiujumla Matukio ya watu kujiua ni miongoni mwa mambo 10 yanayopelekea ukiukwaji wa Haki ya Kuishi Duniani. Sababu kuu ya askari hao kujiua ilitajwa kuwa Msongo wa Mawazo unaosababishwa na watu kushindwa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kijamii kama mahusiano au ndoa, pamoja na changamoto za kiuchumi. Matukio haya kwa jeshi la polisi yamekuwa ya kujirudia mara kwa mara lakini hata kwa watu wa kawaida.

Katika maisha yangu nimewahi kushuhudia mara tatu watu wa karibu wakijiua kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha. Mnamo mwaka 2008 nilishuhudia mdogo wangu akijiua, pia mwaka 2020 baba mdogo naye akichukua hatua hiyo ya kukatisha maisha yake.

Hata hivyo ukubwa wa tatizo unaonekana kuongezeka kwa kasi ambapo vifo vinavyotokea, ni katika kundi la vijana kati ya miaka 15 hadi 29. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na taarifa yake kuripotiwa Septemba 2019 uliweka bayana kuwa kujiua kunachukua nafasi ya pili baada ya matukio ya ajali.

Utafiti huo ulionyesha vijana wengi huwa ndio umri wa kubalehe na wanapitia changamoto nyingi, mara nyingi huwa wanajaribu vitu vingi sana katika maisha yao.

Familia na vijana mara nyingi huwa wanakuwa hawaelewi, malumbano mengi, hawana taarifa sahihi na kile kinaweza kutokea na wanataka kujaribu kila kitu kama vileo wakidhani vinaweza kuwa suluhisho katika kukabiliana na changamoto zao.

Aidha wanaume wanaweza kujiua mara tatu zaidi ya wanawake ambao huwa wanaishi na mawazo ya kutaka kujiua mara tatu zaidi ya wanaume. Wanaume wachache sana wanaojaribu kujiua na kupona, wengi huwa hawaponi.

WHO inasema kuwa tatizo hili halijazungumzwa vya kutosha miongoni mwa jamii za watu. Vitendo hivi huathiri watoto, wazazi, wenza na marafiki. Kila baada ya sekunde 40 mtu mmoja mahali fulani, wanajikatiza uhai duniani.

Wakati ambao mwezi huu wa tisa unamalizika ni vema jamii ikatambua kuwa matukio ya kujiua hayapaswi kuachiwa hivi hivi na ikaonekana ni mapenzi ya Mungu mwanadamu kufa. Inaeleweka kwamba hakuna atakayeishi milele katika dunia hii lakini kifo gani unachokufa ndio penye maswali mengi.

Katika mwezi huu wa kupinga vitendo vya kujitoa uhai, unawezaje kuzungumza na mtu anayefikiria kujiua. Lakini matukio haya hutokea zaidi kunapokuwa na mizozo, au nyakati ambazo watu wanakuwa na msongo wa mawazo, matatizo ya kifedha, kuvunjika kwa mahusiano, maradhi sugu na maumivu yasiyokwisha.

Idadi kubwa ya watu walio mjini hujiua, na makundi ya watu wanaokabiliwa na unyanyapaa. Sababu nyingine za matukio haya ya kujiua ni mizozo, majanga, machafuko, unyanyasaji, kupoteza wapendwa na kutengwa.

Jambo la msingi katika kupambana na changamoto hii ni jamii kuwa na uelewa wa namna ya kuzuia watu kujiua na sababu zinazosababisha mtu kufikia hatua hiyo. Elimu inaposambaa kwa jamii inapunguza visababishi vya mtu kufanya jaribio la kujiua.

0 Comments:

Post a Comment