Monday, September 21, 2020

Ya Lamine Diack kulikuta Shirikisho la Riadha Tanzania?

Mashindano ya Riadha ya Tanzania mnamo mwaka 2020 yaliyofanyika katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Aliyekuwa rais wa Chama cha Kimataifa cha Mashirikisho ya Michezo (IAAF), Lamine Diack amehukumiwa kifungo cha miaka minne gerezani, huku miwili ikisitishwa, kwa kosa la kuwaficha wanamichezo wa Russia waliokuwa wakitumia dawa za kusisimua misuli. 

Diack ambaye ni raia wa Senegal alikabiliwa na mashitaka ya ufisadi na mengineyo. Mahakama moja nchini Ufaransa hivi karibuni iliamua kwamba Diack aliomba au kupokea euro zipatazo milioni 3.2 au takriban dola milioni 3.8 ili kuwaficha wanamichezo kutoka katika ardhi ya Urusi waliokuwa wakitumia dawa za kusisimua misuli. 

Pia kiongozi huyo wa zamani alitozwa kutozwa faini dola 590,000 za Kimarekani. Jaji aliyeendesha kesi hiyo alisema hatua za Diack “zilidunisha maadili ya michezo na vita dhidi ya dawa za kusisimua misuli.” 

Kijana wa kiume wa Diack Papa Massata Diack aliyekabiliwa na mashitaka sawia alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani na kutozwa faini ya euro milioni moja au takriban dola milioni 1.2. Kijana huyo alisalia nchini Senegal, na hakuwa mahakamani wakati hukumu ikitolewa. 

Aidha waendesha mashitaka wa Ufaransa wanachunguza ikiwa uhamishaji wa dola milioni mbili kutoka kwa kamati ya kutoa maombi ya Olimpiki ya Tokyo hadi kwa kampuni moja ya Singapore ulikuwa sawia na ufisadi. Kampuni hiyo inaaminika kuwa na uhusiano na mwanaye wa kiume Papa Massata. 

Taarifa za kuwajibishwa mbele ya vyombo vya dola kkwa kiongozi huyo mkubwa ndio hoja kuu ambayo imeushtua ulimwengu wa wapenda michezo hususani riadha ambao mara kadhaa wamekuwa wakilia na hali zao ili waweze kusonga mbele. 

Hata hivyo kinachostaajabisha na kuacha maswali tele ni pale Russia ambayo ni taifa kubwa na lenye historia kubwa duniani katika kila nyanja linapoingia katika kashfa ya jinsi hiyo. Pia kupitia kashfa hiyo ya Diack mwenye umri wa miaka 87 inatoa somo kwenye mashirikisho mengi ya riadha katika nchi kujipima kama yanatosha na yanadhibiti ubora wa riadha katika mataifa yao. 

Septemba 12-13 mwaka huu nchini hapa kulifanyika mashindano ya Riadha ya Taifa ambayo yalikusanya wanariadha kutoka mikoa zaidi ya 20 ya Tanzania huku mikoa mitatu ikishindwa kushiriki. 

Katika mashindano hayo yaliyofadhiliwa na Olympic Solidarity kwa uangalizi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kwa namna fulani yalitufumbua macho kuona ni kwa namna gani tutachelewa kuifikisha riadha katika kiwango cha kimataifa kama hali itaendelea kama ilivyo. Mosi, mashindano hayo ya taifa yalikuwa yakifanyika kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano kwani kwa mara ya mwisho ilikuwa mnamo mwaka 2015. 

Swali la msingi Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) muda wote huo lilikuwa likifanya nini kuhakikisha wanatengenezwa wanariadha wa kuiwakilisha Tanzania kimataifa. 

Pili, macho ya viongozi wa riadha kuanzia mikoani hadi taifa yalikuwa katika fedha iliyotolewa na TOC kiasi cha shilingi milioni 45 za uratibu wa mashindano hayo, ukiwasikia, kila mmoja alikuwa akizungumza la kwake kuonyesha kuwa kuna dalili ya upigaji wa hiyo fedha, sasa unajiuliza mmesaidiwa bado mnalalamika nini maana yake? Je tutafika tunakotaka kwenda kwa staili hiyo ya kila mtu kutaka fedha iwe upande wake? 

Tatu, Kutokana na kila mmoja kuangalia fedha ndio suluhisho hata maandalizi yalifanyika kwa kulipua kwa maana hiyo hata viwango vya ubora kwa wanariadha haviwezi kuwa vya kimataifa kutokana na maandalizi duni ambayo hayawezi kumpa fursa mwanariadha kutoa ushindani wa kweli. 

Kumeshuhudiwa wanariadha katika mashindano hayo ya kitaifa wakikimbia bila viatu huku wengine wakisema hawajazoea kuvaa viatu kwenye maeneo ya joto, pia wengine wakikosa fedha za kununulia viatu au vifaa kwa ujumla mahsusi kwa ajili ya mbio za uwanjani (Track & Field). 

Mikoa mingi haikuendesha mashindano yao ya mikoa ili kuchagua wawakilishi wao watakaoshiriki mashindano hayo kwa ustadi mkubwa sasa unategemea nini?

Nimefuatilia kwa karibu mashindano ya taifa la China yaliyofanyika sambamba na haya ya Tanzania kwa kweli ni mashariki na magharibi, unaona wenzetu wako ‘serious’ kuhakikisha wanaendelea kuweka rekodi murua kitaifa na kimataifa, wote wana vifaa vya kila tukio la riadha. 

Ninachoweza kusema ni kwamba dunia bado inaendelea kupambana na dawa za kusisimua misuli ambayo ni changamoto kubwa kwa sasa lakini medani ya riadha nchini ikiendelea kwa mwendo huu uliopo sasa wa maslahi binafsi inawezekana baadaye likazaliwa tatizo kubwa zaidi. 

Viongozi mliopo sasa jifunzeni kwa Diack ambaye baada ya kustaafu kwake mwaka 2015 alikokalia kwa miaka 16 ndipo sasa mkururu wa mambo aliyoyafanya wakati akiwa madarakani ulipoanza kushika kasi, hatimaye tumeshuhudia akikutwa na hatia ya rushwa na ufisadi. 

Jitafakarini nafasi mlizoshika kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na taifa je, zinawatosha kama ni kwa maslahi binafsi ni vema mkaziachia nafasi hizo hili washike wengine kwani kiama chaja ambacho kitatenda haki kwa kila mmoja wenu.


0 Comments:

Post a Comment