Maelfu ya watu wa Afrika Mashariki walishtushwa na taarifa majuma kadhaa yaliyopita pale jina la Thomas Lubanga Dyilo, lilipokuwa likitajwa na wenyeji wa Mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ambao walimpokea kwa furaha na shangwe baada ya kumalizika kifungo cha takribani miaka 15 jela na kurudi kwao Ituri.
Ilikuwa hivi; Baada ya kukaa jela kwa kipindi cha
zaidi ya miaka 16 kutumikia adhabu ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC),
kiongozi wa zamani wa waasi wa UPC, Thomas Lubanga, alirejea nyumbani na kupokelewa
na maelfu ya raia.
Maelfu ya watu walijjitokeza mjini Bunia kumpokea Lubanga,
ambaye baadhi ya watu wa kabila lake la Bahema walimbatiza jina la Nelson
Mandela wa Ituri.
Édouard Unwanga Balladur, mmoja wa wazee wa busara wa
kabila la Alur, aliiambia DW kwamba Lubanga "alipatishwa tabu ya bure na
ilhali alikuwa akifanya jambo kwa manufaa ya wakaazi wa Ituri", alipokuwa
kiongozi wa kundi la waasi wa Muungano wa Wazalendo wa Congo, UPC.
Lubanga, aliyewasili Bunia baada ya kuwa gerezani
nchini Uholanzi kwa muda wa miaka 14, sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha
kuyapatanisha makabila ya Bahema na Lendu, kufuatia mauaji yanayoendelea katika
wilaya ya Djugu.
Mauaji hayo yanayofanywa na waasi wa CODECO wanaotokea
kabila la Walendu na yanayowalenga watu wa kabila la Bahema hayajatajwa hadi
sasa kuwa ni mauaji ya kikabila.
Kuwasili kwa Lubanga kumesadifiana pia na kipindi cha
maombolezo kwa watu wa Ituri kufuatia mauaji ya wenzao wapatao 50 yaliyofanywa
na waasi wa kundi la ADF katika vijiji vya Belu, Payipayi na Katanga, katika
wilaya ya Irumu, kusini mashariki ya Bunia, wilaya inayopakana na wilaya ya
Beni katika mkoa jirani wa Kivu ya Kaskazini.
Waasi wa ADF, wamekuwa wakifanya mauaji kila kukicha
katika wilaya ya Beni, kwa sasa wanafanya mauaji hayo hayo katika vijiji
mbalimbali vya mkoa wa Ituri.
Lubanga alikutwa na hatia Machi 14, 2012 na Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi kutokana na makosa ya kivita yaliyoorodheshwa
likiwamo la kuwatumikisha watoto chini ya umri wa miaka 15 kama askari wa
kivita na kuwajumuisha katika uhasama huko Mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo (DRC). Alihukumiwa Julai 10, 2012 na kutupwa jela kwa jumla ya miaka
14.Mnamo Desemba 1, 2014 ilithibitishwa na mahakama kuhusu makosa yake ambapo
Desemba 19, 2015 Lubanga aliendelea kusalia jela za DRC.
Lubanga alizaliwa Desemba 29, 1960 huko Djiba katika
Jimbo la Ituri wakati huo ikiitwa Jamhuri ya Kongo au Leopoldville. Alikuwa
miongoni mwa watu kabila la Hema-Gegere. Alisoma elimu yake katika Chuo Kikuu
cha Kisangani shahada ya Saikolojia . Alioa na akajaliwa kuwa na watoto saba.
Thomas Lubanga wakati akiwa kiongozi wa kundi la UPC |
Wakati wa Vita vya Pili vya Kongo ambavyo vilianza mnamo mwaka 1998 Lubanga alikuwa Kamanda wa Kijeshi na Waziri wa Ulinzi wa Vuguvugu la RCD-ML. Mnamo Julai 2001 alianzisha kundi jingine ambalo aliliita UPC. Mapema mwaka 2002 Lubanga aliondolewa katika vuguvugu la RCD-ML hivyo akaamua kuanzisha kundi jingine la waasisi. Mnamo Septemba akawa Rais wa kundi hilo la UPC ambapo alianzisha tawi la kijeshi la FPLC.
Human Rights Watch ililishtaki kundi la UPC chini ya
amri za Lubanga kwa kufanya mauaji ya kikabila, mateso, ubakaji na kuwajumuisha watoto kuwa askari wa
kijeshi. Kati ya Novemba 2002 na June 2003 inaelezwa kuwa UPC iliwaua raia
wasio na hatia 800 kwa kigezo cha ukabila katika machimbo ya dhahabu katika
eneo la Mongbwalu. Kati ya Februari 18 na Machi 3, 2003 kundi la UPC lilitoa
taarifa kuwa limeharibu vijiji 26 na kuua takribani watu 350 na wengine 60,000
kuyakimbia makazi yao.
Aidha Human Rights Watch ilidai kuwa Lubanga
aliwaajiri watoto 3,000 kuwa wanajeshi ambapo watoto hao walikuwa na umri kati
ya miaka 8 na 15. Lubanga aliwahi kusema kuwa aliitaka kila familia katika eneo
lake kumsaidia katika vita hiyo kwa kuchangia kitu kama fedha, ng’ombe au
watoto kujiunga na jeshi ili kuzuia uonezi wa vikundi vya waasi kutoka nje
vinavyoimezea ardhi yao.
NELSON MANDELA ALIKUWA MTU WA NAMNA GANI?
Nelson Mandela enzi za uhai wake |
Juni 12, 1964 Nelson Mandela, mwanasiasa maarufu nchini Afrika Kusini na duniani kwa ujumla ambaye alikuwa mtu muhimu katika kuutokomeza ubaguzi wa rangi nchini humo alihukumiwa kifungo cha maisha kutokana na harakati hizo. Kwa ufupi ni kwamba alianza kutumikia kifungo cha miaka 27 jela.
Mandela alikuwa mtoto wa Chifu wa kabila la Tembu,
Chifu Henry Mandela. Mandela alizaliwa katika kijiji cha Mveso kwenye mji mdogo
wa Transkei, Julai 18, 1918.
Mandela alikamatwa, akatiwa hatiani na kuhukumiwa
kifungo cha maisha gerezani kuanzia mwaka 1964 hadi 1990, ambapo maisha yake
kama kiongozi wa harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi yakajulikana dunia
nzima. Kama mfungwa wa dhamiri, Mandela mara kwa mara alikataa kuachiwa kwa
masharti.
Mwaka 1990, akiwa amekaa jela kwa miaka 27 na akiwa na
umri wa miaka 71, iliachiwa huru bila masharti yoyote baada ya utawala wa
kibaguzi kushinikizwa na jumuiya ya kimataifa.
Mwaka 1944, alijiunga na chama cha siasa cha African
National Congress (ANC), kilichoundwa kwa lengo la kukabiliana na sera za
ubaguzi wa rangi za serikali ya wachache ya nchini Afrika Kusini iliyoongozwa
na watu weupe.
Na baadaye, mfumo huu ukabadilika na kuwa mapambano ya
muda mrefu dhidi ya ubaguzi yaliyoongozwa na Mandela. Nelson Mandela aliunda
tawi la kijeshi ndani ya ANC lililojulikana kama "Umkhonto we Sizwe"
au "Mkuki wa taifa" ili kukabiliana na serikali iliyoko mamlakani na
sera zao za ubaguzi wa rangi.
Alishitakiwa kwa hujuma na kupanga njama za kuipindua
serikali mnamo mwaka 1964, na ndipo alipofungwa kifungo cha maisha katika
gereza lililopo kwenye kisiwa cha Robben.
Mandela alikivutia kizazi cha Afrika Kusini kwa kuwa
ingawa alikuwa kifungoni kwa muda mrefu, utu wake na mtizamo wake juu ya
ulimwengu ulipenya hadi nje ya kuta za gereza.
Miongo kadhaa aliyotumikia kifungo haikumvunja nguvu,
bali ilimjengea mchango wake wa kihistoria katika mapambano ya kusaka uhuru wa
taifa hilo.
Baadhi ya nyimbo za kupinga ubaguzi wa rangi zilitoa
mwito wa kuachiwa huru kwa Nelson Mandela, na miongoni mwa nyimbo hizo ni ule
wa Johnny Clegg na Savuka ulioitwa, "Asimbonanga" ukiwa na maana
"Hatujamuona". Alifariki dunia jijini Johannesburg, Afrika Kusini
Desemba 5, 2013.
Hivyo basi huenda watu wa Bunia na Ituri kwa ujumla
wake wanamuona Lubanga kurandana kiasi na Mandela licha ya kuonekana kuwa na
makosa ambayo yalimfanya atupwe jela. Hata hivyo wanasalia kuamini kuwa mtazamo
wake juu ya watu wa ardhi yake ni mzuri hata kama haupendezi kwenye macho ya
walio nje ya hapo.
0 Comments:
Post a Comment