Wednesday, September 23, 2020

'Ku-beti' kunatupeleka wapi?-1


Vijana wakifuatilia ratiba ya mechi kwa ajili ya ubashiri

Ubashiri katika michezo nchini umekuwa maarufu kwa jina la ‘mkeka’ au katika maeneo mengine umekuwa ukifahamika ‘Kwa Mhindi’; itakumbukwa kwamba mkeka ni kitu kama jamvi kinachoshonwa kutokana na kili na hutumika kwa kazi mbalimbali kama vile kukalia au kutandika kitandani.

‘Sports Betting’ iliitwa mikeka kutokana na karatasi zinazobandikwa katika ukuta wa matangazo katika kituo cha michezo ya kubahatisha ikionyesha mechi mbalimbali zinazotarajiwa kuchezwa. Lakini tangu mwaka 2013 ilipoanza kushika kasi michezo hiyo katika medani ya soka hadi sasa imekua kwa kiasi kikubwa. 

Hivyo ukisikia ‘Mbuzi kala mkeka’ au ‘ukisikia mhindi amenichania mkeka’ ujue mhusika aliyeweka pesa kwa ajili ya mchezo husika basi ndio ameshindwa kutabiri vizuri na pesa aliyoweka imekwenda na maji; 

Kwa sehemu kubwa ya watu duniani, michezo ya kubahatisha ni burudani maridhawa isiyo na madhara, yaani kwao ni njia moja ya kujifurahisha au kupitisha muda.

Msingi wa makala haya ni kutaka kuangazia kama sheria kanuni na taratibu za michezo hii ya kubahatisha zinafuata na kusimamiwa kikamilifu, hususani kwa washiriki wa michezo hiyo. Hii inatokana na ukweli kwamba maendeleo makubwa ya simu yamekuwa makubwa ambapo mshiriki anaweza ku-beti hata akiwa nyumbani kwake, au kichochoroni. 

Jambo la kuzingatia hapa ambalo litaufanya mjadala huu uendelee zaidi je, watanzania wanaelewa kuwa ‘mikeka’  ni maalumu kwa ‘leisure’ na ‘entertainment’ au wao wanaelewa nini kuhusu hili hususani kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18. 

Pia majina ya wahusika yatahifadhiwa hususani wale walio chini ya umri wa miaka 18. Aidha kinachovutia zaidi ni kwamba hata serikali inatambua kuwa michezo ya kubahatisha ni chanzo kikubwa cha mapato. 

MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA INAZUNGUMZIAJE ?

Katika taarifa yake kwa umma, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Maapto Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede anaweka bayana kuhusu namna ambavyo michezo hii ya kubahatisha inaongeza mapato, anasema, “kodi ya michezo ya kubahatisha ni

kodi inayotozwa kwenye mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha. Kodi hizi ni za aina mbili; Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Tax) - Hii ni kodi anayotozwa mwendeshaji wa mchezo wa kubahatisha kutokana na mapato yake yatokanayo na michezo ya kubahatisha.” 

Pia Dkt. Mhede anaongeza, “Kodi ya Michezo ya Kubahatisha kwenye Zawadi (Gaming Tax on Winnings), Hii ni kodi anayotozwa mchezaji baada ya kushinda zawadi ya mchezo wa kubahatisha.” 

Kwa mujibu wa TRA aina ya michezo inayotozwa kodi ya aina hiyo ni Kasino (Casino), Kasino ndogo (Mini Casino/Forty machines sites), Michezo ya Kubashiri Matokeo (Sports Betting), Michezo ya Machine (Slots machines/route operations), Bahati Nasibu ya Taifa (National lottery) na Bahati nasibu ya kutumia ujumbe mfupi wa simu.(SMS lottery)

BODI YA MICHEZO YA KUBAHATISHA TANZANIA INATOAJE LESENI?

Bodi ya michezo ya kubahatisha Tanzania (Gaming Board of Tanzania), inatoa maelekezo ya utoaji wa leseni kuwa leseni/vibali vya kuendesha shughuli za michezo ya kubahatisha hutolewa na gaming board of tanzania baada ya mwombaji kukidhi vigezo vilivyoainishwa kisheria ikiwa ni pamoja na kufanyiwa upekuzi wa kina (background check). 

Marekebisho ya Sheria ya Leseni (Business Licensing Act no. 25 of 1972) yaliyofanyika mwaka 2003 kupitia Finance Act No. 15 ya mwaka 2003, kifungu 5(1)(f), yaliondoa michezo ya kubahatisha katika orodha ya uhitaji wa leseni za biashara, isipokuwa leseni inayotolewa na Gaming Board. 

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO TANZANIA INACHUKULIAJE MICHEZO YA KUBAHATISHA?

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja katika taarifa yake kwa umma aliweka bayana ongezeko la maduka ya michezo ya kubahatisha na namna inavyoongeza pato la taifa. 

“Serikali imetolea ufafanuzi juu ya suala la michezo ya kubahatisha kuwa ni moja ya shughuli za kiuchumi, zinazoendeshwa kwa mujibu wa sheria kama shughuli zingine. Michezo yote ya kubahatisha ikiwemo Kamari (slots machines) inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Namba 4 ya mwaka 2003, Sura 41 pamoja na Kanuni zake,” alisema Mwaipaja. 

Katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, aliwahi kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Asha Abdullah Juma, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kudhibiti michezo ya kubahatisha ambao alisema umekuwa ukiwakosesha amani wazazi na jamii nzima, kwa kuchangia uvunjifu wa maadili na nguvu kazi ya vijana inayopotea kwa kucheza michezo hiyo badala ya kushiriki katika uzalishaji. 

Dkt. Kijaji alisema sheria inakataza watoto wenye umri chini wa miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au kuzururazurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha. 

“Mtu yeyote atakaye ruhusu mtoto chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la Mchezo wa Kubahatisha, anahesabika kafanya kosa na anastahili kulipia faini ya shilingi 500,000/- au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote kwa pamoja” aliongeza Dkt. Kijaji 

“Endapo kosa hilo litafanywa na mwendesha mchezo wa kubahatisha, Bodi ina mamlaka kisheria kumfutia leseni. Hivyo basi, wajibu wa Serikali ni kuzuia watoto na vijana walio chini ya miaka 18 kucheza michezo ya kubahatisha. Natoa rai kwa wazazi na walezi kuwazuia wao kucheza michezo hiyo” alisisitiza Dkt. Kijaji 

 

VIJANA CHINI YA UMRI WA MIAKA 18

Mnamo mwaka 2015 katika kupitapita kwangu nilikutana na kijana huyu aliyejitambulisha kwa jina Justin ukimuangalia ana umbo la miaka 18 lakini katika uhalisia wake ana miaka 16 hivi. Nilijuaje? 

Nilimuuliza swali hili, ulizaliwa lini akakataa kuniambia, nikabadilisha swali umesoma hadi kidato cha ngapi? Justin akasema ameishia darasa la saba. 

Nikaongeza swali jingine, lini ulimaliza darasa la saba akasema 2013 na hakufanikiwa kwenda sekondari kutokana na ugumu wa maisha ikabidi aendelee kufanya kazi mbalimbali za kujitafutia kipato. 

Justin ambaye kazi yake kubwa wakati huo ilikuwa ni kuuza maandazi na chai majira ya asubuhi katika maeneo ya Zakheim, jijini Dar es Salaam aliniambia kuwa ‘ku-beti’ yaani kucheza mikeka hakujamsaidia kwani tangu aanze kujiingiza katika suala hilo ameshinda mara mbili. 

Kwa uchungu mwingi kijana huyo alisema kwamba ametumia kiasi kikubwa cha fedha kuwekeza ili atoke kimaisha  kwani aliwaona wenzake wakijishindia zaidi ya shilingi 100,000/= za Tanzania. 

Kibaya zaidi Justin alisema kiwango alichoshinda kilikuwa ni shilingi 2,000/= akilinganisha na kiasi cha fedha zaidi ya shilingi 30,000/= alichotumia katika ‘ku-beti’. 

Alipoulizwa anakozitoa fedha hizo Justin hakutaka kuweka bayana lakini kwa uchunguzi wa haraka haraka nikagundua kuwa amekuwa akitumia mtaji wake wa maandazi na chai kwenda kucheza. Mambo hayo!

Bado niliendelea kuzunguka zunguka katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam mnamo mwaka 2018 wakati wa Kombe la Dunia lililofanyika Russia nilishuhudia jinsi ambavyo vijana wakichakarika ‘Ku-beti’ nani ataibuka mshindi wa mchezo huu na ule na hata bingwa wa fainali hizo ambayo ilikuwa ni timu ya taifa ya Ufaransa likiwa ni taji lake la pili baada ya lile la mwaka 1998. 

Nilikuwa nikiishi Tandale kwa Tumbo, duka la ‘Ku-beti’ halikuwa mbali sana na nilipokuwa nikiishi umbali wa mita 300 hivi tukiwa katika duka hilo kila mtu alikuwa bize na kutazama mechi zitakazochezwa huku akiwa na kikaratasi na peni, binafsi nilikuwa sichezi ila nilikuwa maarufu sana eneo hilo wakiiniita ‘Jeshi la Mtu Mmoja’ 

Sababu ya kuniita ‘Jeshi la Mtu Mmoja’ ni kutokana na uwezo wa kubashiri matokeo ya mechi husika ya Kombe la Dunia, sasa nikajifunza jambo mara baada ya kijana mmoja mwenye umri wa miaka 17 kunifuata na kuniambia, “Kaka yaani leo umenipiga tafu kwelikweli, ilikuwa nife pale yaani Mhindi angenichania mkeka wangu, usingetabiri mechi zile mbili yaani buku tano langu lingeniuma hatari. We bro jeshi la mtu mmoja.” 

Nilicheka sana baada ya maneno ya kijana yule nikamuuliza, “Una umri wa miaka mingapi? Usinifiche.” Kijana yule akawa na wasiwasi mkubwa kwamba ninaweza kumharibia, nikamtia moyo kuwa sitaweza kufanya hivyo, akasema, “Ukweli bro mimi nina miaka 17 mimi nilizaliwa mwaka 2001…” 

Kijana yule wa kiume akasema, “Ku-beti mi alinifundisha rafiki yangu mmoja wa kitaa ambaye yeye alikuwa mzoefu wa ku-beti, nilikuwa nikimuona akiwa na fedha kibao, lakini kuna siku unamkuta hana akienda ku-beti ana mpunga wa elfu 20, au zaidi kulingana na mechi alizobeti.”

“Nimekuwa nikishinda sio mara kwa mara lakini naona inanisaidia kinyama, si unajua tena familia zetu bila hela mambo hayaendi, shuleni utaendaje wakati mzazi kila siku anakwambia hana hela, so lazima utafute namna ya kupata pesa sasa ku-ti licha ya kwamba sio rahisi inategemea na bahati yako lazima uvumilie kwa hali zozote zile,” alisema.

Je, wazazi wanasemaje kuhusu michezo hii ya kubahatisha maarufu kama ‘Ku-beti’. Tutaendelea katika makala yajayo.

Imetayarishwa na Jabir Johnson, mwandishi wa habari nchini Tanzania. Baruapepe: jabirjohnson2020@gmail.com

MAKALA ZINAZOHUSU SPORTS BETTING au KU-BETI

Ku-beti kunatupeleka wapi?-2

Ku-beti kunatupeleka wapi?-3

Ku-beti kunatupeleka wapi?-4


0 Comments:

Post a Comment