RIPOTI ya Chama cha Michezo ya Kubahatisha cha
Marekani (AGA) mnamo mwaka 2017 kilikadiria kuwa kubeti kulikuwa kukiingiza
mapato katika taifa hilo kati ya kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 100 na
400 kwa mwaka.
Mwanahistoria wa Ufaransa Georges Vigarello anasema
wakati wa utawala wa dola mbalimbali zilizopita suala la kamari lilikuwa ni
jambo la muhimu na lilikuwa likifanyika katika mifumo miwili ama kwa kubeti au
kupata zawadi baada ushindi.
Vigarello anaongeza kuwa kubeti kulikuwa kukifanyika
baina ya watu waliopo katika tabaka moja; wakulima au matajiri. Michezo
iliyokuwa ikishirikisha zawadi ilikuwa ikifanyika katika matukio muhimu kama
kuzaliwa au harusi.
Hadi karne ya 19 kubeti kulianza kuangaziwa kama
miongoni mwa mambo katika michezo. Utamkumbuka Baron Pierre de Coubertin,
ambaye mnamo mwaka 1887 alianzisha Muungano wa Vyama vya Michezo nchini
Ufaransa ambapo neno mchezo ‘Sport’ lilipoanza kutumika badala ya lile ya
‘Games’.
Wakati wa Mapinduzi ya Viwanda nchini Uingereza Mbio
za Farasi ambazo ni maarufu sana katika ardhi hiyo; katika karne ya 16 na 17
zilifanya kubeti kuwe maarufu. Hata hivyo kubeti kuliruhusiwa kwa watu wenye
uwezo hususani wamiliki wa farasi na wenye maduka ya vinywaji.
Miongoni mwa mbio za farasi ilikuwa ile ya mwaka 1870
iliyozinduliwa na Earl wa 12 wa Derby Edward Smith-Stanley. Pia Charles II
ambaye alikuwa akipenda sana mchezo huo alivuta umati mkubwa wa watu kushiriki
kwa kiasi kikubwa ikiwamo kubeti na kiasi kikubwa cha fedha kilipatikana
kupitia mbio hizo.
MATOKEO YA
KU-BETI
Kubeti kumekuwa na matokeo chanya na hasi hata hivyo
katika michezo kwa upande hasi kashfa za upangaji wa matokeo katika matukio
mbalimbali ya michezo yamerikodiwa. Katika
mashindano ya baseball nchini Marekani mnamo mwaka 1919 ambapo fainali ilikuwa
baina ya mabingwa wa Ligi ya Marekani Chicago White Sox dhidi ya Mabingwa wa
Taifa Cincinnati Reds ambapo Cincinnati Reds waliibanjua White Sox kwa 5-3.
Mashindano hayo yalisifiwa sana kwa kuweka rekodi ya kuingiza
mapato katika fainali za baseball zilizowahi kufanyika katika karne ya 20.Mapato
mengi yakipatikana kupitia kubeti. Hata hivyo mchezo huo uliingia doa mnamo mwaka
1989 wakati huo Pete Rose alikuwa kocha wa Cincinnati Reds ambaye alikutwa na
kashfa ya kupanga matokeo wakati akiwa mchezaji na kocha wa mabingwa hao wa
1919 World Series.
Matokeo yake Rose aliondolewa katika Jumba la Wakongwe
wa Baseball mnamo mwaka 1991. Rose alikiri kwa kinywa chake mnamo mwaka 2004
kuwa alibeti akiwa mchezaji na kocha wa Cincinnati Reds. Rose aliwahi kutumikia
Reds mara mbili (1963-1978 na 1984-1989).
Katika mchezo wa kikapu mwamuzi wa NBA Tim Donaghy
alikutwa na kashfa kwenye michuano ya NBA mnamo mwaka 2002. Donaghy alikutwa na
hatia ya kubeti katika mechi zote alizokuwa akichezesha. Donaghy alichezesha
misimu 13 ya Ligi ya NBA kutoka mwaka 1994 hadi 2007; mechi 772 na mechi 20 za
mtoano (playoffs).
Donaghy alijiuzulu kuchezesha mechi za NBA Julai 9,
2007 baada ya ripoti zake kuifikia Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI)
kuhusu upangaji wa matokeo kwa misimu miwili. Mnamo Agosti 15, 2007 Donaghy
alikutwa na hatia na Julai 29, 2008 alihukumiwa kwenda jela miezi 15.
Alitumikia miezi 11 katika jela ya Pensacola, Florida na miezi iliyobaki
alimalizia kifungo cha nyumbani.
Donaghy alirudishwa tena jela mnamo Agosti baada ya
kukiuka matakwa ya sheria ya kuachiwa. Novemba 4, 2009 aliachiwa baada ya
kumaliza kifungo chake. Baada ya kashfa hiyo mchezo wa sita wa fainali za NBA
Ukanda wa Magharibi mwaka 2002 uliingia doa kutokana na Donaghy kubeti
isivyotakiwa.
Katika mchezo wa soka kukutwa na kashfa ya kupanga
matokeo kupitia kubeti imezikuta ligi nyingi ikiwamo ile ya Uturuki mnamo mwaka
2011 huku klabu ya Fenerbahce ikinyoshewa kidole cha lawama ambapo mnamo mwaka
2015 ilipanda katika mahakama ya rufaa kutaka kulipwa kwa uharibifu na usumbufu
uliojitokeza ikitaka kiasi cha euro milioni 135 kutoka shirikisho la soka la
Ulaya (UEFA) na lile la Uturuki (TFF).
Aidha katika kashfa hiyo ya mwaka 2011 nchini Uturuki
ilidaiwa kuwa mechi 19 za soka nchini humo zilibetiwa isivyo ambapo Julai
10,mwaka huo huo watu 61 wakiwamo makocha wa soka walikamatwa kwa kupanga
matokeo (kubeti) wakiwamo wachezaji wa timu ya taifa ya Uturuki.
Kupanga matokeo hakuishia hapo mnamo mwaka 2015 Soka
la Italia liliingia doa baada ya kukutwa na kashfa ya kupanga matokeo kupitia
kubeti isivyo. Msimu wa 2014-15 klabu ya Calcio Catania iliingia katika kashfa
hiyo ambapo Mei 19, 2015 takribani watu 50 walikamatwa kutokana na kupanga
matokeo. Catania inaonesha ilipanga matokeo mechi tano ili iweze kusalia Serie
B. Juni 23, 2015 Rais wa Klabu hiyo Antonio Pulvirenti na wengine sita
walikamatwa kutokana na kupanga matokeo. Siku sita baadaye mwaka huo huo Pulvirenti alilipa pauni 71,000 sawa na shilingi
milioni 212 za Tanzania kutokana na kupanga matokeo ya mechi tano.
Shirikisho la Soka la Italia mnamo Agosti 20, 2015;
lilitangaza rasmi kuishusha daraja klabu ya Catania hadi ligi daraja la tatu na
kunyang’anywa pointi 12 na faini ya euro
150,000 sawa na shilingi milioni 400 za Tanzania ikiwa ni adhabu mbaya kuwahi
kutolewa kwa klabu yoyote nchini Italia.
Timu nyingine zilizoingia kwenye kashfa hiyo ni Savona
na Torres ambazo zilipata adhabu ya kushushwa hadi ligi daraja la nne (Serie
D). Teramo ilinyimwa nafasi ya kupanda daraja la pili (Serie B) msimu wa 2015-16 na kunyang’anywa
ubingwa wa Lega-Pro msimu wa 2014—15.
Hata hivyo haitasahulika kashfa ya kupanga matokeo ya
mwaka 1877 ya Louisville Grays katika mchezo wa baseball; katika kashfa hii
baadhi ya wachezaji wa baseball wa timu ya Louisville Grays walipokea kitita
cha fedha ili waweze kupoteza mechi zao. Wachezaji hao Bill Craver, Jim Devlin,
George Hall na Al Nichols baadaye walikutwa na hatia ambapo walizuia kufanya
shughuli yoyote inayohusu mchezo wa baseball maisha yao yote.
Hayo ni matokeo ya kubeti katika michezo ambayo
yamepoteza ajira za wengi, yameathiri mienendo ya klabu mbalimbali za michezo
kufikia malengo zilizojiwekea kutokana na kubeti.
Akizungumza na LaJiji mdau wa michezo nchini Tanzania
Michael Mbughi anasema, “Kubeti kunaweza kuleta athari chanya na hasi kwa
wakati mmoja, upande wa hasi ndio unaoumiza hebu fikiria umechukua ubingwa wa
Ligi Kuu Tanzania Bara halafu unakutikana ulibeti michezo tuseme miwili halafu
unashushwa hadi daraja la nne na faini juu hapo ni majanga tu.”
Hata hivyo Mbughi anasisitiza ulazima wa elimu
kuendelea kutolewa kwa jamii na wale wanaobeti kuzingatia sheria zilizowekwa
ili kuondokana na matokeo hasi ambayo yanaweza kuleta usumbufu usio wa lazima.
“Kwa upande wa wazazi na walezi wanapaswa kuwaelekeza
watoto wao kuhusu michezo hii ya kubeti kuwa inapaswa kufanywa kwa kiasi
kinachoonekana sasa watu hawataki kufanya kazi wanategemea kubeti hapo kutakuwa
hakuna tofauti na mraibu wa dawa za kulevya,” anaongeza Mbughi.
MAKALA NYINGINE ZA SPORTS BETTING au KU-BETI
0 Comments:
Post a Comment