Familia ni kikundi cha watu wanaokaa pamoja kama baba,
mama na watoto. Kikundi hicho mara yingi ni sehemu ya kundi kubwa zaidi la ukoo
unaounganisha watu wenye asili katika uzazi wa pamoja.
Aina za familia zinatofautiana duniani kutokana na
utamaduni na hali ya jamii. Katika nchi nyingi za Afrika familia ndogo ya baba,
mama na watoto kwa kawaida ni sehemu tu ya familia kubwa zaidi pamoja na ndugu
wa baba na mama, akina babu na bibi na kadhalika.
Lakini hata Afrika kuna taratibu tofauti tofauti kama
ni ndugu wa baba au ndugu wa mama wanaotazamiwa kuwa karibu zaidi kwa watoto wa
familia ndogo. Vilevile kuna tofauti kama muundo wa kawaida ni mume mmoja na
wake wengi na kila mmoja akiwa na watoto wake tena.
Katika jamii za nchi zilizopita kwenye mapinduzi ya
viwandani kama Ulaya na Marekani familia inamaanisha hasa familia ndogo inayokaa
pamoja katika nyumba. Ukoo haujapotea lakini umuhimu wake umepungua sana na
mara nyingi ni chaguo la watu ndani ya ukoo kama wanapenda kujumuiana na ndugu
zao au la.
Katika mazingira ya miji mikubwa au pale ambako koo za
kale zimeporomoka na kuachana kuna jumuiya ndogo sana kama mama na watoto ambao
ni familia bila baba au wanaume. Aina hii ya familia yenye mzazi mmoja tu
imepatikana pia kama familia ya baba na watoto kama utamaduni unamruhusu baba
peke yake kulea watoto.
Nchini Tanzania suala la kuifahamu historia ya familia
husika linaweza kuwa jambo gumu kutokana na familia nyingi kutawanyika kutokana
na mabadiliko makubwa ya kimaisha ambayo yametokea tangu mwanzoni mwa karne ya
21, pia ufuatiliaji wa wanafamilia wenyewe kuhusu walikotoka ni jambo ambalo
halijazoeleka.
Kwa asili mwezi Oktoba ni mwezi wa nane katika
mtiririko wa Kalenda ya Kirumi. Asili ya neno Oktoba imetoka katika lugha ya
kilatini ‘Octo’ ikiwa na maana ya ‘Nane’.
Baada ya kalenda za Julian na Gregori kuanza kutumika
ukawa ni mwezi wa kumi. Oktoba ni miongoni mwa miezi sita kati ya saba ambao
una siku 31. Oktoba ulikuwa ni mwezi wa nane wakati wa utawala wa kirumi wa
Romulus mnamo mwaka 759 K.K Baadaye Oktoba ukawa mwezi wa kumi baada ya
kuongeza miezi ya Januari na Februari katika kalenda hiyo.
Wakazi wa Saxons ambao walikuwa wakiishi katika pwani
ya bahari ya Kaskazini ambayo kwa sasa ni Ujerumani Oktoba walikuwa wakiuita
‘Wintirfyllith’ kutokana na kwamba mwezi huo ulikuwa na mbalamwezi na mwanzo wa
baridi kali.
Hata hivyo kumekuwa na matukio ambayo yamekuwa
yakiadhimishwa kila mwaka katika mwezi huu wa 10 kwa kalenda ya sasa ya
Gregori, miongoni mwa matukio ni ‘Ufahamu kuhusu Historia ya Familia yako’
ikiwa na madhumuni ya kuhamasisha watu mbalimbali kuzifahamu na kuzitunza
historia za familia zao kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya; Rubetina
Meena anasema watanzania walio wengi wanafahamu historia kwa kiasi kidogo.
“Utakuta mtu anafahamu mwisho kwa babu yake tu,
familia yake ilikotoka hadi hapo alipo hana ufahamunayo ila anaweza kukwambia
kuhusu kabila lake lilipotoka; nafikiri changamoto kubwa ni familia nyingi
hazikuwa na utaratibu wa kutunza kumbukumbu kwa maandishi,” anasema Bi.
Rubetina.
Mfuatiliaji wa masuala ya Kijamii Adam Damian anasema
kutunza kumbukumbu kwa mdomo kumesababisha kumbukumbu nyingi kupotea au
kupoteza mantiki iliyokusudiwa za familia husika jambo ambalo linapelekea watu
wengi kushindwa kuzifahamu historia zao.
“Unapopitia kurasa za mitandao mbalimbali duniani
historia za familia za kiafrika huwezi kuzikuta kwa wingi, sio kwamba hazipo
bali nadhani ni ukosefu wa kujizoeza
kutunza kumbuka kwa kufanya ufuatiliaji huo na kama tunatunza basi ni kwa mdomo
jambo ambalo linaweza kupotea mtu husika mwenye historia hiyo anapofariki
dunia. Watu muhimu wameaga dunia wakiwa na vitu muhimu kwa ajili ya familia
zetu lakini kwasababu hawajawahi kutuambia ndio basi tena,” anasema Damian
Baadhi ya watu waliofanikiwa kuanza kufanya utafiti wa
familia zao wamefanikiwa kuanzisha mikutano ya wanafamilia hao kwa ajili ya
kufahamiana zaidi jambo ambalo linatia hamasa katika kutunza historia za
familia.
Kwa mujibu wa mtafiti Adam Alphonce Kivenule wa Kidamali,
Iringa katika mojawapo ya tafiti zake alifuatilia ukoo wa Kivenule ulipoanzia
na kuandika haya, ninanukuu; “Ukoo wa Kivenule ni mmojawapo wa koo nyingi kubwa
zilizopo katika Himaya ya Uhehe katika Mkoa wa Iringa. Ukoo wa Kivenule ulianza
kutambulika toka Karne ya 18. Historia inaonesha kuwa Ukoo huu asili yake ni
kutoka kwa Wabena-Manga, waliopo Kusini mwa Mji wa Iringa; yaani maeneo ya
Mufindi na Njombe. Ni mchanganyiko wa Wahehe na Wabena wanaojulikana kama
Wabena-Manga.”
Kivenule anaongeza kuwa kwa Asili, ukoo wa Kivenule ni
maarufu kama Wapiganaji wa Vita. Ukoo wa Kivenule ulikuwa hodari sana katika
vita vya msituni ambavyo viliwahusisha babu zao akina Tagumtwa ambapo madhumuni
makubwa ya vita hizo katika himaya ya Uhehe ilikuwa kupata mali, mifugo na
heshima.
“Babu Tagumtwa Balama (Kivenule) ndiye aliyewazaa Babu
Tavimyenda Kivenule na Babu Kalasi Kivenule. Ikumbukwe kuwa, jina halisi la
ukoo wa Kivenule ni Balama…” anasema Kivenule
Je, una shauku ya kuifahamu historia ya familia yako?
Basi tumia mwezi huu wa Oktoba japo kuandika kurasa 10 za maelezo kuhusu
familia yenu, muulize mama, baba, bibi, babu, mjomba, shangazi au walezi wako
kuhusu wewe na familia yako. Hiyo itasaidia kujizoeza kutunza kumbukumbu za
familia ambayo itakuwa msaada wa kizazi kijacho.
0 Comments:
Post a Comment