Katibu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres aliyeshika nafasi hiyo kutoka mwaka 2017 hadi sasa. Guterres alipokea mikoba kutoka kwa Ban Kimoon.
Mnamo mwaka 1945, mataifa yalikuwa magofu. Vita vya pili vya
dunia vilikwisha na ulimwengu ulihitaji
amani. Mataifa 51 yalikusanyika huko San Francisco mwaka 1945 kutia saini hati
ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.
Sudan Kusini ndiyo nchi ya mwisho kujiunga na Umoja wa Mataifa mwaka 2011 baada ya Montenegro (2006) , Uswisi na Timor-Leste (2002), Yugoslavia na Tuvalu (2000).
Hati hii ilikuwa ni mkataba, ukiunda shirika jipya ambalo si jingine bali ni Umoja wa Mataifa. Mwaka 2020 ni miaka 75 tangu kuanzishwa Umoja wa Mataifa unaendelea kudumisha amani na usalama wa kimataifa.
Umoja wa Mataifa unakuza maendeleo na kupatia wahitaji misaada ya kibinadamu. Umoja wa Mataifa unatetea sheria ya kimataifa, unalinda haki za binadamu, na kukuza demokrasia.
Na kwa sasa, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinafanya kazi pamoja kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Umoja wa mataifa unasaidia kujenga ulimwengu bora kama vile ambavyo waanzilishi wake walivyotamani miaka 75 iliyopita.
Lugha rasmi za Umoja wa Mataifa ni sita ambazo ni Kiarabu, Kichina, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza na Kirusi.
Kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni mjumbe wa Baraza Kuu. Mataifa yanakubaliwa kuwa wanachama wa UM kwa uamuzi wa Baraza Kuu baada ya kupendekezwa na Baraza la Usalama.
Vyombo vikuu vya vya Umoja wa Mataifa ni Baraza Kuu, Baraza la Usalama, Baraza la Uchumi na Jamii, Baraza la Udhamini, Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Sekretarieti. Vyote hivi viliundwa mwaka 1945 wakati Umoja wa Mataifa ulianzishwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni alama ya maadili ya shirika na msemaji mkuu wa shirika kwa maslahi ya watu wa ulimwenguni, hususan maskini na wale walio hatarini zaidi kudhuriwa.
Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa, na ambaye ni wa tisa (9) kushika wa waadhifa huu ni António Guterres kutoka nchini Ureno.
Alichukua mamlaka mnamo Januari 1, 2017. Mkataba wa Umoja wa Mataifa humweleza Katibu Mkuu kama ‘Ofisa Mkuu Tawala’ wa shirika.
Sekretarieti, mojawapo wa kiungo muhimu cha Umoja wa Mataifa, imepangiliwa kwa misingi ya idara, kila idara au ofisi ikiwa na eneo la utendaji na jukumu dhahiri. Ofisi na idara huratibiana kuhakikisha kuna uwiano zinapotekeleza kazi za kila siku za shirika katika ofisi na vituo vya kazi kote duniani. Kiongozi wa Sekretarieti ya Umaja wa Mataifa ni Katibu Mkuu.
Mfumo wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana rasmi kama ‘‘familia ya UN’’umeundwa na Umoja wa Mataifa wenyewe na programu zingine zinazohusiana, fedha na mashirika maalumu zote zikiwa na uanachama wao, uongozi na bajeti.
Programu na fedha hufadhiliwa kwa njia ya kujitolea kinyume na michango kadiriwa. Mashirika Maalumu na mashirika huru ya kimataifa yanafadhiliwa kwa njia ya kujitolea na michango iliyokadiriwa.
Katika makala haya tutaangazia kipengele cha mabadiliko ya tabianchi na namna Umoja wa Mataifa unavyopambana kukabiliana na changamoto hiyo.
Taarifa ya mwaka 2020 imepembua kuhusu, hali ya kiwango cha Maji duniani, Bahari, Kiwango cha maji yaliyoganda kwenye uso wa dunia, hali halisi ya ardhi duniani, kiwango cha maji ya Bahari pamoja na usafi na usalama wa hali ya hewa duniani.
Guterres anasema, maeneo yote haya ni muhimu ili kuweza kutoa taarifa kamili ya uelewa wa mabadiliko ya tabianchi kisayansi.
Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yametoa taarifa ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi kwa mwaka 2020 “The United in Science 2020 Report” na Karibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres kuandika dibaji yake.
Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO, limeratibu taarifa za Mashirika ya: Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, UNESCO-IOC, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, Global Carbon Project, GCP, Intergorrmental Panel On Climate Change, IPCC.
Kila Shirika liliweza kutoa taarifa yake ya kisayansi na zote kwa pamoja zikahaririwa na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO.
Guterres katika dibaji ya taarifa hii anasema kwamba, janga la homa kali ya mapafu inayosabishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limeleta madhara makubwa katika maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia.
Guterres ana matumaini makubwa, kwamba, Serikali na viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Kimataifa wataweza kutumia tafiti hizi za kisayansi, ili kuweza kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, ili kujenga mazingira salama sanjari na kuendelea kujikita katika maendeleo fungamani ya binadamu kwa ajili ya mafao ya wengi.
Wakati huo huo, kumekuwepo na ongezeko kubwa la nyuzi joto duniani hali ambayo imepelekea athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi.
Majanga ya moto yameongezeka maradufu, kumekuwepo na ongezeko la kina cha bahari, mafuriko na kwa upande mwingine kumekuwepo na ukame wa kutisha. Barafu inaendelea kuyeyuka kwa kasi kubwa kiasi cha kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi. Haya yote yamekuwa ni madhara makubwa kwa watu na mali zao.
Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa, hali inayotishia Jumuiya ya Kimataifa kutoweza kufikia lengo lake la kudhibiti ongezeko la nyuzi joto duniani hadi kufikia nyuzi joto 1.5 kipimo cha sentigrade kama njia ya kutekeleza kwa vitendo makubaliano.
Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 ulifanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12 2015.
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. wa Makao makuu ya Kanisa Katoliki dunia huko
Vatican katika makala yake ya Septemba 2020 alitoa ushauri wake kwa Umoja wa
Mataifa katika mapambano ya Mabadiliko Tabianchi kuwa viongozi wa Serikali
mbalimbali duniani wanapaswa kujifunga kibwebwe, ili waweze kushirikiana kwa
ukaribu zaidi na wanasayansi, ili kuibua sera na mikakati endelevu na hatimaye,
waweze kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, ili kuweza kukabiliana na
changamoto mamboleo.
0 Comments:
Post a Comment