Thursday, October 29, 2020

SIKU YA INTANETI: Intaneti itumike kujenga Tanzania ya Viwanda

Mnamo mwaka 2019 Bunge la taifa la Urusi maarufu Duma lilipitisha mswada ambao ulidhamiria taifa hilo kuwa mfumo wake pekee wa mtandao wa intaneti ambao utalifanya taifa hilo kutotegemea intaneti inayotumika duniani.

Muswada huo ambao ulipitishwa kwa kura nyingi za wabunge 307 huku 68 wakipiga kura kuupinga. Mmoja wa waandishi wa mswada huo Andrei Klishas alikaririwa akisema kwamba hawana shaka Marekani ina uwezo wa kiufundi wa kuizimia Urusi huduma za intaneti wakati wowote wakipenda kwa hivyo na wao wanajiandaa kiufundi kuhakikisha wanajilinda dhidi ya mashambulizi hayo.

Intaneti imekuwa maarufu sana duniani kote sasa hivi kutokana na huduma kadhaa ambazo zinaweza kupatikana kupitia njia hiyo.

Watu wengi wanaitumia  intaneti kupeleka na kupokea barua-umeme au barua pepe (‘e-mail’). Barua pepe ni njia moja maarufu na ya haraka sana ya kumtumia ujumbe (barua) mtu aliye mbali. Kinachohitajika ni kwa mtumaji kujua anuani ya barua pepe ya mtu anayetaka kumpelekea barua hiyo.

Mtu yeyote yule ambaye anatumia kompyuta iliyounganishwa na intaneti anaweza kunitumia barua pepe na ikanifikia baada ya sekunde au dakika chache tu. Kutegemeana na wapi ujumbe wa barua pepe ulipotokea, na njia iliyotumiwa mpaka kuufikisha ujumbe huo kwenye kisanduku changu cha barua pepe, inaweza kuchukua zaidi ya dakika chache.

Siku hizi pia kuna namna ya kumtumia mtu ujumbe kwa njia ya barua pepe, na ukamfikia kwenye simu yake ya kiganjani (cellular phone). Au pia unaweza mtu kumtumia ujumbe kwa njia ya barua pepe ukamfikia kwenye ukurasa wake.

Uvumbuzi wa intaneti ni miongoni mwa maendeleo makubwa ya teknolojia katika historia ya binadamu kutokana na ukweli kuwa teknolojia za kisasa ni suluhisho katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi, kijamii na kimazingira katika karne ya sasa ya 21.

Mapinduzi yaliyoletwa na kiteknolojia  ya kisasa yanaleta  matumaini makubwa zaidi katika kukomesha umasikini  endapo mashirika makubwa na nchi tajiri zitajumuisha nchi zinazoendelea katika kubuni sera zitakazosimamia maadili na kulinda mazingira.

Uchumi wa Viwanda unategemea kwa kiasi kikubwa matumizi ya mtandao wa intaneti. Hii inatokana na ukweli kuwa serikali ya awamu ya tano imejipambanua kuwa inataka Tanzania ya Viwanda.

Tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015 imekuwa ikiweka mkazo zaidi katika uendelezaji wa miradi ya kielelezo; Kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu; na Kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji na uendeshaji biashara.

Aidha mazingira na usimamizi wa uwekezaji wa sekta binafsi hususani viwanda vya nguo, ngozi, nyama, samaki, mafuta ya kula, madawa na vifaa tiba, vyakula vya binadamu na mifugo na katika sekta ya madini.

Mpaka kufikia mwaka 2008 zaidi ya nusu ya watu duniani waliweza kupata kiwango fulani cha kuunganishwa na huduma za mawasiliano kupitia simu.

Inakadiriwa kuwa mwaka 2007 peke yake, jumbe za maandishi zipatazo trilioni 1.9 zilitumwa si tu kama njia rahisi ya mawasiliano lakini pia kama miamala ya kifedha, taarifa za masoko na bei za bidhaa, na hivyo kuwezesha uzalishaji wa takribani dola za Kimarekani bilioni 52 kwa kampuni za mitandao ya simu za mkononi.

Oktoba 29 kila mwaka huadhimishwa mojawapo wa tukio kubwa la uvumbuzi katika historia ya binadamu la matumizi ya Mtandao (Intaneti). Siku hii ilianza kuadhimishwa mnamo mwaka 2005. Ni ukweli kwamba Oktoba 29, 1969 kwa mara ya kwanza matumizi ya intaneti yalianza kutumika ikiwa ni siku chache baada ya Mmarekani Neil Armstrong kuanza safari yake kwenda mwezi ilipoanza.

Mchango mkubwa wa Armstrong, Buzz Aldren, Leonard Kleinrock, Charley Kline na Bill Duvall ambao walikuwa wa kwanza kuvumbua matumizi ya intaneti wakati huo wakifanya na ARPANET iliyokuwa ikifadhiliwa na Idara ya Ulinzi ya Marekani.

Vita Baridi ilichochea kukua kwake kutokana na kwamba mfumo  huwa ni  hauwezi kuharibiwa kwa bomu. Ikiwa sehemu fulani ya mfumo huo ingeharibiwa, bado habari ingesafiri hadi kikomo chake kwa msaada wa sehemu zilizobaki.

Madhumuni makuu yalikuwa kuunganisha taasisi za kijeshi na kielimu nchini Marekani. Mtandao wa kwanza ulihusisha kompyuta nne tu kutoka vyuo vikuu mbalimbali ambazo zingeweza kupeleka data kwa kila mmoja wao.

Hii leo karibu nusu ya wakaazi wa dunia wanatumia intaneti. Kusambazwa kwa intaneti kumechangia kuleta mabadiliko katika nyanja zote za maisha.

Wakati dunia inaadhimisha  uwepo wa matumizi ya intaneti ambayo kwa kiasi kikubwa yamebadilisha maisha ya watu kwa ujumla ni vema kutambua uchumi wa viwanda wa Tanzania unapaswa kuendana na kasi ya mabadiliko makubwa ya teknolojia hii ya intaneti.

0 Comments:

Post a Comment