Tuesday, October 27, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Ifahamu historia ya Taliban

TALIBAN maana yake ni Wanafunzi au jina jingine katika ardhi ya Afghanistan wanafahamika kama Pashto. Kundi hili la Taliban lina mrengo wa kisiasa za kihafidhina na kidini ambalo liliibuka katikati ya miaka ya 1990 baada ya majeshi ya Kisovieti kujiondoa katika ardhi ya Afghanistan.

Kujiondoa huko kuliendana sanjari na kuanguka kwa utawala wa Kikomunisti katika taifa hilo hali iliyosababisha utawala wa kiraia kuanguka. 

Neno Taliban limechukuliwa kutoka katika asili yake ambalo idadi kubwa ya walijiingiza katika kundi hilo walikuwa ni wanafunzi wa Shule za Kiislamu maarufu madrasah, ambazo zilianzishwa kwa wakimbizi wa Kiafghani miaka ile ya 1980 Kaskazini mwa Pakistan.

Wataliban waliibuka ili kuweka mfumo wa kuitawala Afghanistan wakitokea Kusini mwa taifa hilo katika jimbo la Kandahar na kwa haraka sana mfumo huo ukaangukia kwa miamba ya kivita ambayo ilianza kushikilia eneo la Kusini la Afghanistan.

Mwishoni mwa miaka ya 1996, Taliban ilipata uungwaji mkono kutoka kwa kabila la WaPashtun  na msaada mkubwa wa Wahafidhina wa Dini ya Kiislam waliokuwa nje ya Afaghanistan. 

Msaada huo uliwasaidia Wataliban na wakafanikiwa kudhibiti makao makuu ya Afghanistan wa Kabul, hivyo kujikuta wakilishikilia taifa lote. Upinzani uliendelea, hususani kwa wale ambao hawakuwa wa kabila la Pashtun ambao ni Tajiki, Uzbek na Hazara ambayo yote haya ni ya upande wa kaskazini, magharibi na katikati ya taifa la Afaghanistan.

Makabila hayo yalijionea Taliban ikiwa na idadi kubwa ya WaPashtun ambao walikuwa wakiendeleza utamaduni wao katika taifa hilo. Mnamo mwaka 2001 Taliban walikuwa wameshashika eneo kubwa la Afghanistan lakini wakishika kwa kiasi kidogo eneo la kaskazini ya taifa hilo.

Maoni ya wengi ulimwenguni hawakukubaliana na sera za kijamii za Taliban ikiwamo ya kuwatenga kabisa wanawake na huduma muhimu kama ajira na elimu.

Pia dunia iliwapinga Taliban kutokana na kuharibu mifumo ya wasio Waislamu zikiwamo sanaa na desturi kama ambavyo ilitokea katika mji wa Bamiyan uliopo umbali wa kilometa 130 kutoka Kabul. 

Kitendo ambacho walikifanya Taliban katika mji huo kilionyesha dhahiri kuwa walikuwa na azma nyingine kwani mji wa Bamiyan ni mji wa kihistoria miongoni mwa miji ya kale ambayo ilitajwa katika vyanzo vya Wachina mnamo karne ya tano (5) ambapo Viongozi wa Dini wa Buddha kutoka Uchina walikuwa na tabia ya kuuzuru mji huo.

Watu kama Wa Faxian (miaka ya 400) na Xuanzang (miaka 630) walikuwa wakifanya biashara vizuri na kufanya mambo ya kidini hususani Buddha. 

Ndipo katika kipindi hicho walipoinua sanamu ya Buddha katika karne ya nne na tano, sanamu hiyo ilikuwa na mita 53 kwa kimo na nyingine ndogo ilikuwa na kimo cha mita 40. Sanamu hizo zilitengenezwa kutokana na miamba iliyopo kwenye milima mjinihumo na ikamaliziwa kwa kuwekwa naksi na kupakwa rangi.

Taliban haikuishia hapo iliendelea kuiudhi dunia kwa utoaji wa adhabu kwa wanaopatikana na makosa. Adhabu hizo zilikuwa kinyume na haki za binadamu ambapo utawala huo uliungwa mkono na Saudia Arabia, Pakistan na Falme za Kiarabu.

Kilichosababisha kukubalika na mataifa hayo ni Taliban waliruhusu Afghanistan kuwa sehemu salama kwa Majeshi ya Kiislamu duniani kote, hapo ndipo raia wa Saudi Arabia Osama bin Laden alipokimbilia huko na kuwa kiongozi wa Al-Qaeda.

Akiwa huko alikuwa mratibu mkuu wa matukio ya kigaidi dhidi ya Marekani. Taliban iliikatalia Marekani kuhusu kumpeleka Bin Laden nchini Marekani akashtakiwe baada ya mashambulio ya World Trade Center jijini New York na Pentagon  jijini Washington yaliyofanyika Septemba 11, 2001.

Mashambulio hayo ndio yaliyoleta mtafaruku baina ya Marekani na washirika wake hali iliyopelekea uvamizi wa Marekani katika ardhi ya Afghanistan. Hatua hiyo iliifanya Taliban ijiondoe katika kushikilia madaraka.

Taliban iliasi kuunga mkono Marekani na majeshi ya NATO. Taliban iliendelea kutoa fedha kwa vikundi mbalimbali hali iliyopelekea kuishiwa nguvu ya kushikilia serikali ya Afghanistan.

Kilichofanyika ni kwamba majeshi ya Marekani na washirika wake yaliifurumisha Taliban katika misingi yake huko Kandahar ambapo kiongozi wake Mullah Mohammad Omar alikuwa akitangazwa kuendelea na uasi wake kusikojulikana. 

Kuna wakati ilielezwa kuwa yupo Pakistan, licha ya Taliban kukataa. Julai 2015 serikali ya Afghan ilibaini kuwa Mullah Omar alishafariki mnamo mwaka 2013 katika hospitali moja nchini Pakistan.  

Mullah Akhtar Mansour alichukua mikoba ya Mullah Omar, naye huyo aliuawa na majeshi ya Marekani mnamo Mei 2016 nchini Pakistan. Haibatullah Akhundzada akachukua kijiti na kuongoza kundi hilo tena licha ya kusalia katika mrengo wa kisiasa na kidini. 

Kwa upande wa kijeshi Taliban iliendelea kushika hatamu kwa maelekezo ya mtandao wa Haqqani ambapo Sirajuddin akahudumu kama Msaidizi wa Akhundzada.

Mara kadhaa Taliban imeendelea kuidhoofisha serikali ya Afghanistan hali ambayo imefanya mara kadhaa viongozi wa juu wa taifa hilo kukaa kitako na Taliban kwa ajili ya mazungumzo. 

Maafisa wakati wa utawala Hamid Karzai walikuwa wakikutana mara kwa mara na viongozi wa Taliban, wa kwanza kabisa iliyowekwa wazi ilikuwa chini ya Rais Ashraf Ghani. Mara kadhaa Taliban imekuwa ikisisitiza inataka kuongea na mataifa yaliyowaweka madarakani moja kwa moja wakiitaka Marekani.

Hilo likafikiwa mnamo mwaka 2018 na mazungumzo yakaanza kwa msaada wa Saudia Arabia, Pakistan na Falme za Kiarabu (Imarati). Rekodi ikawawekwa ka mataifa haya ambayo yalionyesha ukomavu wa kutokuwa na upande katika masuala ya kidiplomasia.

Mazungumzo hayo yaliangazia kuondolewa kwa majeshi ya Marekani katika ardhi ya Afghanistan, japokuwa Marekani ilikuwa na matumaini makubwa ya kuishinikiza Taliban kuzungumza zaidi na serkali ya Afghanistan.

Mnamo Julai 2019  majadiliano yaliendelea kwa kuwahusisha maafisa wa serikali ya Afghanistan kwa mara ya kwanza ambao walikubaliana na wawakilishi wa Taliban kuhusu kanuni za makubaliano hayo. 

Wawakilishi wa Taliban hawakutatakiwa kufanya makubaliano yoyote ya kiofisi lakini waangalizi wa mazungumzo hayo waliyachukulia kama ni mazungumzo ya mafanikio.

Mapema Septemba 2019 iliripotiwa kuwa Marekani na Taliban wamefikia makubaliano ya kikanuni na yalipunguzwa nguvu wakati wa shambulio la Taliban mjini Kabul lililomwuua mhudumu wa Marekani. 

Siku chache baadaye mkutano wa siri baina ya Maafisa wa juu wa Marekani na wale wa Taliban ulitarajiwa kufanyika uliahirishwa huku Marekani ikiinyoshea kidole cha lawama Taliban kuhusika na shambulio hilo.

Mwishoni mwa Februari 2020, Taliban walikubali kuanza mazungumzo na serikali ya Afghanistan na walisaini makubaliano na kuizuia al-Qaeda na Dola la Kiislamu (ISIS) kufanya shughuli zake katika ardhi ya Afghanistan.

Kwa upande wake Marekani ilikubaliwa kuwa angeanza kuondoa majeshi yake ndani ya miezi 14 na hatua hiyo alianza mnamo Machi 2020. Mazungumzo mengine yalifanyika Septemba 12 mwaka huu baina ya Taliban na serikali ya Afghanistan.

0 Comments:

Post a Comment