Tuesday, October 27, 2020

Oktoba 27: Siku ya Paka Mweusi

KATIKA jamii nyingi duniani kumekuwa na tafsiri mbalimbali kuhusu Paka Weusi, kila anapoonekana paka mweusi jamii hizo hushistushwa na uwepo wa viumbe hao.

Mnamo mwaka 2018 nchini Kenya wakati shughuli za bunge la nchi hiyo zikiendelea, ghafla zilisimama kwa muda kufuatia kuingia kwa kishindo kwa paka mweusi ndani ya jengo hilo kabla ya kuanza kupiga mayowe ya kuhofisha. Huku wabunge wakiujadili mswaada wa kibiashara, paka huyo alianza kutoa sauti za ajabu ajabu na kutatiza shughuli nzima.

Mbunge wa Suba Kaskazini wakati huo, Millie Odhiambo, alionekana kuwa miongoni mwa wale waliokinaishwa na uwepo kwa paka huyo bungeni huku akitaka aondolewe angalau waweze kukamilisha kuujadili mswaada uliokuwa mezani.

Baada ya muda mfupi, kamera za CCTV zilinasa paka mweusi akitembea tembea kwenye makao hayo ya Bunge bila wasiwasi. Odhiambo alihoji kuwa kuwepo kwa paka huyo mweusi kunatia hofu na hivyo panahitajika kuandaliwa maombi na viongozi wa dini ili kupatakasa. Hatimaye waliamua kuwa paka huyo aondolewe katika eneo hilo kuruhusu ajenda za bunge kuendelea.

Kumekuwa na tafsiri nyingi miongoni mwa hizo ni hii; Ukitaka kumuona mchawi au mwizi akija kwako usiku wakati upo usingizini utachukua mifupa ya paka mweusi aliyekufa au kuuliwa bila wewe kujua ameuliwa na nani kisha utaiweka katika pembe nne za nyumba au milangoni na madirishani basi akija mchawi au mwizi wakati ukiwa usingizini utamuona bila yeye kujua kuwa anaonekana na utamtambua.

Imekuwa ni kawaida kwa madereva kuvigonga viumbe mbalimbali lakini linapokuja suala la paka mweusi, dereva anasema huo ni mkosi.

Kama haitoshi tafsiri hii imekuwa ikizungumzwa sana kuwa Paka ni mnyama mwenye hisia kali sana na pia paka ana uwezo mkubwa wa utambuzi, na paka anapoona roho yoyote katika nyumba kitu cha kwanza cha kufanya hujaribu kuangalia kama roho hiyo ni nzuri au mbaya.

Paka amewahi kuabudiwa kama mwenye kuleta neema na ameshawahi kunyoshewa kidole cha lawama kwa kuleta bahati mbaya sehemu mbalimbali. Nchini Uingereza wanaamini kwamba paka mweusi ni ishara ya uchawi na paka ambaye siyo mweusi basi ni bahati nzuri.

Baadhi wanaamini kwamba Paka Mweusi akikupitia mbele yako ni ishara ya bahati mbaya na wengine wanadai ni bahati nzuri hasa ikiwa paka huyo anatokea kushoto kuelekea kulia.

Wengine wanasema kwamba Paka Mweusi akija nyumbani kwako usimfukuze vinginevyo ataondoka na bahati yako yote. Amerika Kusini inachukuliwa paka mweusi ni mchawi ambaye anaweza kusababisha ugonjwa hata kifo. Katika nchi nyingi za Ulaya na Amerika paka mweusi ni ishara ya Shetani na matendo yake ni ya Kishetani.

Amerika Kusini wao wanamchukulia Paka Mweusi kama tiba ya maradhi yasiyotibika. Wale wanaougua humchukua Paka wakamchinja na nyama yake huchemshwa na kuliwa na mgonjwa, na mgonjwa huyo hupona.

Wafuatiliaji wa mambo ya jamii wanasema licha ya kukamata panya ana faida nyingi ikiwamo dawa ya mapenzi; hii ilianza kuthibitishwa nchini Misri ambako walikuwa wakitumia wakitumia ini lake kwa kulikaanga na kupata unga wake kisha kuwalisha wapenzi wao kwa kuwawekea katika chai majira ya asubuhi.

Oktoba 27 kila mwaka kutokana na tafsiri hizo ambazo kwa upande mmoja zinaonekana kuwa kikwazo kwa maendeleo na utunzaji wa paka weusi, mnamo mwaka 2011 wanaharakati wa wanyama hususani paka waliketi pamoja na kuanza kuadhimisha siku hii ikiwa ni sehemu ya kutambua uzuri wake.

Mnamo mwaka 2017 Taiwan ilipiga marufuku uuzaji na ulaji wa paka kufuatia visa kadhaa vya ukatili dhidi ya wanyama na kuzua ghadhabu ya umma.

Sheria mpya ya kulinda wanyama imeweka adhabu ya faini ya shilingi milioni 20 za Tanzania kwa yule anayepatikana akiuza, kula au kununua nyama hiyo. Wanaopatikana wakiwadhulumu wanyama nao watapigwa faini ya shilingi milioni 160 za Tanzania na miaka miwili gerezani.

Taiwan ndilo taifa la kwanza kuweka marufu hii barani Asia. Sheria hiyo ilinuia mpya kukabili baadhi ya imani kuhusu ulaji paka. Kwa mfano kuna baadhi wanaamini kumla paka mweusi wakati wa msimu wa baridi kunamsaidia mtu kupata joto mwilini.

Licha ya kutokuwepo na takwimu rasmi, China inaaminika kuongoza duniani katika ulaji na uuzaji wa paka. Kila mwaka karibu paka milioni 5 wanaaminika kuchinjwa nchini China. Wakati dunia ikiadhimisha siku hii ni vema jamii ikatambua umuhimu wa kulinda haki za wanyama.

0 Comments:

Post a Comment