REKODI ya kwanza katika Michezo ya
Kubahatisha au kubeti kama ambavyo tunaita siku za leo inaonesha ni zaidi ya
miaka 2,000 iliyopita watu walikuwa wakifanya. Wagiriki walikuwa ni wapenzi wa
michezo na hii ndio sababu ya kuanzisha michezo ya Olimpiki ambayo dunia
inaicheza na ambayo imejizolea umaarufu mkubwa. Wakati walipoanzisha michezo
hiyo inaelezwa kuwa walianza kubeti
kwenye michezo ya riadha ambako walibashiri ni nani atayeibuka na ushindi na
yupi atayeshindwa.
Baada ya Wagiriki kueneza utamaduni
huo, zama za Warumi zilifika na wao wakaukubali utamaduni huo wa kubeti katika
medani ya michezo licha ya kuufanyia marekebisho kidogo kutokana na namna siasa
na utamaduni wao ulivyokuwa ili kupata uungwaji mkono.
Warumi waliendeleza kubeti kupitia
michezo ya kutumia mapanga (gladiator games) ambayo ilifikia kikomo katika
karne ya 2 BK lakini suala la kubeti halikuisha ambapo lilizidi kutawanyika kwa
kasi zaidi katika falme nyingine.
Nyakati za katikati kutoka karne ya
5 hadi karne ya 15 baadhi ya viongozi wa dini walipambana kuzuia michezo hiyo
ya kubeti wakidai kuwa ni kinyume na kanuni za dini. Watu wa nyakati hizo
waliwaheshimu sana viongozi wao wa dini kwa kuogopa kutengwa na dini zao
waliendelea kubeti kwa siri hadi wakati ambapo matukio ya michezo mipya na ya
kisasa ilipoingia katika jamii zao.
Miaka ya baadaye michezo hiyo ya
kubahatisha ambayo ilionekana dhahiri kuwa ni kamari iliyohalalishwa ilikuwa
maarufu kwenye ardhi ya England. Nchini humo kubeti kulikuwa maarufu katika
Mbio za Farasi ambako watu walicheza. Waingereza ndio waliousambaza katika
muundo wa kisasa katika mataifa ya Amerika hususani nchini Marekani na kuwa
kubeti kukawa maarufu kwa watu wengi hadi hivi sasa.
Kupanuka kwa matukio ya michezo
mbalimbali ulimwenguni ndio sababu kubwa ya umaarufu wa kubeti unavyokuwa.
Baadhi ya michezo unayoiona sasa haikuwepo katika karne chache zilizopita
lakini leo mtu anayetaka kubeti anaweza akacheza zaidi ya mchezo mmoja kwa
maduka tofauti ya kubeti ambayo kila kukicha yamekuwa yakiongezeka.
Mwanzoni mwa miaka ya 1950 huko Las
Vegas nchini Marekani katika Jimbo la Nevada waliruhusu michezo ya kubahatisha
katika makasino ambako watu waliokuwa wakitaka kubeti walipeleka fedha zao
hapo. Lakini changamoto kubwa wakati huo ilikuwa ni mwendo wa kwenda katika kasino
husika na kupeleka kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kubeti. Umbali mrefu
ilikuwa changamoto kwani ilikuwa lazima uende Las Vegas.
Kwa sasa udhibiti wa kubeti unakuwa
mgumu kutokana huduma hiyo kupatikana mtandao na mshindi wa kubeti hujipatia
fedha yake hapo katika simu yake.
Nchini Tanzania wazazi wamekuwa
wakiinyoshea kidole cha lawama michezo hiyo ya kubeti kuwa inaharibu maadili ya
familia zao, lakini swali la kujiuliza wazazi au walezi hao watafanya nini ili
kuzifanya familia zao zisiathirike na kubeti? Hasa ikizingatiwa sheria zipo za
kudhibiti michezo hiyo na faida yake kwa taifa imekuwa ikionekana kutokana na
mapato yanayokusanywa?
DINI ZINASEMAJE KUHUSU KU-BETI?
Kwa watanzania walio wengi kila mtu
ana dini yake, wengine ni wakristo na wengine ni waislamu licha ya kwamba kuna
Wahindu, Waba’hai na kadhalika. Kila unayemuuliza wewe unasali au unaswali
wapi? Lazima atakwambia mimi ni wa kanisa fulani, au mimi ni wa msikiti fulani.
Katika maduka ya kubeti niliyopita
majina ya kina Hassan, Dula, Khamis, Roger, Baraka, Iddi na mengine mengi
utayasikia yakiitwa humo, hiyo ikiwa na maana kuwa wanaobeti ni watu ambao wana
dini zao wanasali au kuswali; sasa imani zao zinasemaje kuhusu suala hili?
Mchungaji wa Kanisa la Tanzania
Assemblies of God (TAG) Chanika jijini Dar es Salaam Fidelis Kalinga anasema,
Kamari katika Biblia ijapokuwa haitaji moja kwa moja michezo ya kamari,
huzungumzia michezo fulani ya bahati nasibu kama kupiga kura katika Mambo ya
Walawi kuchagua baina ya mbuzi wa sadaka na mbuzi wa lawama.
Aidha Mchungaji Kalinga anasema
Biblia inaonya kwamba “wale ambao wameazimia kuwa matajiri huanguka katika
jaribu na mtego na tamaa nyingi za kijinga na zenye kudhuru, ambazo hutumbukiza
watu katika maangamizi na uharibifu.” (1 Timotheo 6:9) Watu hucheza kamari kwa
sababu ya tamaa, na “tamaa” ni mbaya sana hivi kwamba Biblia inaitaja kuwa
miongoni mwa tabia tunazopaswa kuepuka kabisa. (Waefeso 5:3)
Katika Uislamu, Naaswir Haamid
anasema Maisha ya Muislamu daima ni yenye mabadiliko katika hali yoyote ile.
Muislamu yeyote yule hatoweza kuishi pekee bila ya kuchanganyika na wenzake na
bila ya kwenda huku na kule ili kutafuta njia mbali mbali za kujitafutia rizki
za kimaisha.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Kawaamrisha waja Wake waende kutafuta rizki katika Ardhi hii kwa kusema: {{Yeye
Ndiye Aliyefanya Ardhi iwe inaweza kutumika (kwa kila myatakayo) kwa ajili
yenu. Basi nendeni katika pande zake zote na kuleni katika riziki zake, na
Kwake Yeye ndiyo marejeo (nyote)}} [Al-Mulk: 15]
Naaswir Haamid anaongeza kuwa
hakika kutafuta riziki ni jambo la lazima katika maisha ya Muislamu. Riziki
hizo huenda zikachumwa kwa njia za halali au haramu. Miongoni mwa rizki zilizo
haramu ni ile inayotokana na kamari.
{{Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi,
kamari, kuabudu masanamu na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shaytwaan.
Basi jiepusheni navyo ili mpate kufanikiwa}} [Al-Maaidah: 90].
JE, KU-BETI KUNAWEZA KUKOMESHWA?
Mwandishi na mfuatiliaji wa masuala
ya ku-beti kwa muda mrefu sasa John Milton anasema watu wamekuwa wakibeti katika michezo kwa
muda mrefu kutokana na michezo yenyewe kuwa inaendelea kuchezwa. Milton
anapendekeza kwamba haoni sababu ya
kuamini kwamba suala la kubeti litakuja kubadilika au kuachwa kabisa katika
jamii.
“Michezo miwili mikubwa duniani
ambayo imekuwa kipaumbele katika kubeti yote inaitwa mpira wa miguu (football),
maeneo mengine duniani wanaita soka. Soka limekuwa licheza mechi maelfu kila
mwaka kwa mashabiki wake ambao wanavutiwa kubeti. Mabilioni ya pesa yamekuwa
yakitumika katika kubeti kila mwaka, sioni kama kutakuwa na mabadiliko katika
siku za usoni,” anasema Milton katika mojawapo ya makala zake kuhusu Michezo ya Kubahatisha.
Milton ambaye amewahi kukaa katika
kitengo cha masoko kwenye baadhi ya maduka ya michezo ya kubahatisha anasema
michezo mingine maarufu imekuja kwa kasi katika kubeti ikiwamo kikapu, magongo
na baseball.
“Pia nimekuwa nikiona betting
ikichezwa katika badminton, mbio za farasi, mbio za magari, michezo ya
olimpiki, pool, vishale, gofu, kuogelea na kufukuza mbuni,” anaongeza Milton.
Hata hivyo Milton anasema matumizi
ya intaneti na simu yamekuwa kichocheo kikubwa katika michezo ya kubahatisha,
hatua hiyo imeondoa usumbufu mkubwa wa mtu au watu wanaotaka kubeti kupitia
madirishani kwenye maduka sasa wanaweza kufanya wakiwa nyumbani kwao na simu
zao kwa njia ya mtandao kwenye sites za kubeti.
MAKALA NYINGINE ZA SPORTS BETTING au KU-BETI
0 Comments:
Post a Comment