Kahawa ni kinywaji maarufu na kinachopendwa sana na
watu wengi. Kahawa pia imekuwa ni zao mashuhuri la kibiashara duniani kwa muda
mrefu. Kwa hakika umaarufu na kupendwa kwa kinywaji cha kahawa unatokana na
manufaa kadhaa yanayopatikana ndani ya kinywaji hiki.
Kwa Afrika Mashariki hususani maeneo yote yanayolima
kahawa kinywaji cha kahawa ndicho kinachoongoza kupendwa. Hata hivyo juhudi
mbalimbali zimekuwa zikifanyika ulimwenguni kote kuhakikisha unywaji wa kahawa
unaongezeka katika jamii. Kama ilivyo chai watu wanavyoongezeka katika unywaji
wa chai ndivyo kilimo cha chai kinavyopewa uzito.
Shirika la Kimataifa la Kahawa (ICO), liliamua kwa
dhati kuongeza unywaji wa kahawa na kilimo chake pale lilipoamua kwa moyo mmoja
kuanza maadhimisho ya siku ya Unywaji wa Kahawa kila Oktoba Mosi. Mnamo mwaka
2015 kila siku ya kwanza ya mwezi Oktoba huwa maalum kwa ajili ya kuikumbusha
jamii kuhusu unywaji wa kahawa.
Kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yalifanyika jijini
Milan, Italia kwa ajili ya kuongeza unywaji wa kahawa. ICO ilisema Oktoba Mosi
ni maadhimisho ambayo ni maalum kwa ajili ya kuunga mkono mamilioni ya wakulima
ambao wamekuwa wakitegemea kuendesha maisha yao kupitia zao hilo muhimu la
kahawa pia kuwapa fursa wale ambao wamekuwa wakipenda kahawa na bidhaa zake
kuendelea kutumia kinywaji hicho.
Utafiti umeonyesha kuwa unywaji kahawa una faida kubwa
kwa mwanadamu. Mtu anayekunywa vikombe vitatu hadi vinne vya kahawa kwa siku, huishi
kwa muda mrefu ukilinganisha na asiyekunywa kabisa.
Utafiti uliofanywa katika chuo kimoja mjini London
umeonyesha kuwa mtu mwenye kunywa kahawa huwa na uelewa zaidi ukilinganisha na
asiyekunywa. Magonjwa kama saratani, kisukari, matatizo ya maini na vilevile
akili yameonekana kuwapata kwa nadra wanywaji kahawa. Wanawake wajawazito pia
hufaidika kwa wingi endapo watakunywa kwa kiasi walau kikombe kimoja kwa siku. Ripoti
zinaonyesha kuwa faida za kunywa kahawa ni kubwa kuliko hasara.
Watafiti walipolinganisha watu wasio kunywa kahawa, na
wale wanaokunywa takriban vikombe vitatu vya kahawa kwa siku walionekana
kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi.
Kunywa kahawa huchangamsha mwili ikiwa na maana
humfanya mnywaji asijisikie kuchoka na huongeza kiwango cha nguvu za mwili. Caffeine
inayopatikana kwenye kahawa huuchangamsha ubongo na kuufanya mwili kuwa katika
hali nzuri. Hii ndiyo sababu watu wengi wenye kazi nyingi hupenda kunywa kahawa
wakati wa kazi au baada ya kazi zao.
Pia unywaji wa kahawa huyeyusha mafuta mwilini; Tafiti
mbalimbali zinaeleza kuwa kahawa huchangia katika kuyeyusha mafuta mwilini na kusababisha
kupunguza uzito wa mwili. Utafiti mmoja uliofanyika ulibaini kuwa kahawa
iliweza kusaidia kupunguza mafuta kwa watu wanene kwa asilimia 10 na kwa
asilimia 29 kwa watu wembamba.
Faida nyingine ya unywaji wa kahawa ni kuwa kahawa ina
virutubisho muhimu; Inaelezwa kuwa kikombe kimoja cha kahawa kina virutubisho kama
Riboavin (Vitamini B2): 11%, Asidi ya Pantothenic (Vitamini B5): 6%, Manganese
na Potasiamu: 3%,Magnesiamu na Niacin (B3): 2%. Hivyo kunywa vikombe visivyozidi
vitatu kwa siku kutaongeza kiwango cha virutubisho hivi.
Huzuia maradhi ya kupoteza kumbukumbu; maradhi ya
kupoteza kumbukumbu huwakabili watu wengi hasa wenye umri wa kuanzia miaka 65. Kwa
sasa hakuna tiba ya maradhi haya lakini yanaweza kuzuiwa au kupunguzwa kwa
lishe bora pamoja na mazoezi. Wataalamu wa afya wanasema watu wanaokunywa
kahawa hupunguza kama siyo kukabili athari za maradhi haya kwa asilimia 65.
Unywaji wa kahawa ni mlinzi mzuri wa afya ya ini; Ini
ni kiungo muhimu sana kwenye mwili wa binadamu. Hata hivyo maradhi kama vile
uvimbe kwenye ini (hepatitis) pamoja na tatizo la seli za ini kugeuka makovu
(cirrhosis) hupungua kutokana na unywaji wa kahawa.
Kwa wale wenye msongo wa mawazo unywaji wa kahawa
hupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo; kwani msongo wa mawazo ni tatizo
baya la kiakili na kisaikolojia ambalo linaweza kuathiri maisha kwa kiasi kikubwa
hata kusababisha kifo.
Hivyo basi umuhimu wa kilimo cha kahawa unapaswa
kupewa kipaumbele hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ni nchi ya nne barani Afrika
kwa uzalishaji wa kahawa; ikizidiwa na Ethiopia (39%), Uganda (23%) huku nafasi
ya tatu ikishikwa na Ivory Coast (13%). Asilimia 6 ya uzalishaji huo inatoka
Tanzania hivyo ni muhimu kuendelea kutilia mkazo kilimo cha zao hili kwa
manufaa zaidi.
0 Comments:
Post a Comment