Kuna methali isemayo, Choko mchokoe pweza, binadamu hutomuweza. Hii ni miongoni mwa methali za Kiswahili ambazo zinamtaja pweza.
Tafsiri sahihi ya methali hii ni epukana na mtu ambaye huenda akaleta matatizo kwani mpiga ngumi ukuta huumiza mkonowe au mpiga mbizi nchi kavu huchunua usowe. Jambo la msingi kwanini walimtaja pweza wasitaje kiumbe mwingine?
Jibu ni rahisi pweza ni wanyama wa bahari wenye
minyiri (mikono) minane inayobeba vikombe vya kumung'unyia na inayotumika kwa
kukamata wanyama wadogo. Wana mdomo unaofanana na ule wa kasuku.
Pweza huogelea kwa kuondoa maji kwa nguvu kupitia
mrija wake. Wanaweza kubadilisha rangi yao na pengine umbo wao ili kufanana na
kinyume na kujificha kwa mawindo na maadui. Wakivumbuliwa huruka wakitoa
ghubari la kiwi (maada kama wino) ili kukanganya adui.
Pweza wanaweza kushambulia watu lakini hii ni adimu.
Wakichochewa wanauma kwa domo lao na wanatoa sumu, lakini spishi moja tu, pweza
mizingo-buluu, ana sumu inayoweza kuua watu. Adui mkubwa viumbe hawa ni samaki
aina ya pomboo na binadamu.
Kiumbe huyu huliwa sana na watu waishio pembezoni mwa
bahari kwa sababu ana nyama nzuri tu, ila huwa na chumvi nyingi. Katika
utamaduni hasa wapwani supu ya samaki huyu hupendwa sana na kumekuwa na imani
kuwa supu yake si supu tu ya kawaida kama ulizowahi kunywa.
Daktari mmoja wa masuala ya virutubisho nchini anasema
Pweza ana protini na madini ya selenium; ambayo yana umuhimu mkubwa. Pweza
amejawa na wingi wa virutubisho ambavyo husaidia mwili kujikinga dhidi ya
magonjwa kama vile saratani kama saratani ya mdomo, utumbo mkubwa, tumbo,
matiti, shingo ya kizazi na pia kansa ya mapafu.
Faida nyingine pweza ana virutubisho vinavyosaidia
kuukinga mwili dhidi ya kupungukiwa na uwezo wa ubongo hasa kwa wenye umri
mkubwa. Kitaalamu tatizo hili huitwa Alzheimer. Pweza huwasaidia walaji
kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Pumu.
Wataalamu wamegundua kuwa mlaji wa pweza yupo katika
hatari ndogo ya kuugua ugonjwa wa pumu. Hata wenye ugonjwa huo huweza kupata
virutubisho vya kupunguza athari za ugonjwa. Pweza husaidia mwili kufanya kazi
zake vizuri ikiwamo mmeng’enyo wa chakula, upumuaji na hata mzunguko wa damu.
Minofu ya pweza huusaidia mwili kuzalisha haemoglobin
ambazo ni muhimu katika damu. Hii ni kwa sababu pweza ana madini aina ya shaba
ambayo ni muhimu kwa kazi hiyo. Kwa upande wa kina mama, pweza husaidia katika
uzalishaji wa maziwa pindi wanapojifungua.
Watumiaji wa supu na minofu ya pweza ni kuwa huongeza
madini joto mwilini. Virutubisho vilivyomo ndani ya pweza husaidia kupunguza
athari za maradhi ya moyo kwa kuwepo mafuta ya omega-3 fatty acid.
Licha ya watanzania wengi hususani wa pwani kumpenda
pweza, lakini wavuvi wa aina ya samaki huyo wanasema kuwa kazi ya kumtafuta
pweza ni ngumu sana kwani mtu huhitaji kuwa na ujuzi maalum, afya bora na vifaa
vilivyo vinavyostahili.
Oktoba 8 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya Pweza;
sababu kuu ni kutambua mchango wa kiumbe huyu kwa maisha ya watu kama sababu
mbalimbali zilivyoanishwa za kiafya na kiuchumi.
Pia siku hii iliwekwa kwa ajili ya kutambua kiumbe
huyu kwani ni miongoni mwa viumbe wa zamani sana kutambuliwa na mwanadamu,
mabaki ya kiumbe huyo yanaonyesha alikuwepo miaka milioni 300 iliyopita.
Pweza ana damu ya rangi ya bluu ambayo ina madini ya shaba
kwa jina hymocianin ambayo humsaidia kuishi chini ya bahari. Hata hivyo umri
wao wa kuishi duniani hususani kwa pweza mkubwa ni miaka mitano
0 Comments:
Post a Comment