Oktoba 5 kila mwaka ni siku ya Walimu duniani.
Maadhimisho haya hufanywa kwa ajili ya kutambua mchango wa mwalimu katika
jamii. Mwalimu ni kutoka neno la Kiarabu; kwa Kiingereza teacher, school
teacher na pengine educator) huyu ni mtu anayesaidia wengine kupata ujuzi,
maarifa na tunu.
Kazi hiyo inaweza kufanywa na yeyote katika nafasi
maalumu, kwa mfano mzazi au ndugu akimfundisha mtoto nyumbani, lakini kwa
wengine ndiyo njia ya kupata riziki inayomdai karibu kila siku kwa miaka mingi,
kwa mfano shuleni. Huko mwalimu anatakiwa kuwa na shahada au stashahada, kadiri
ya sheria za nchi na ya ngazi ya elimu inayotolewa.
Katika jamii yetu fani hii ya ualimu inaonekana kuwa
kazi rahisi kwa wengine, mwalimu anaweza kukabili magumu mengi, kama vile kuwa
na watoto wengi mno darasani, kushughulikia karatasi nyingi, urasimu unaolemea,
wanafunzi wasiotaka kujifunza, na mshahara mdogo.
Mtu mmoja aliwahi kusema hivi: “Ualimu si kazi rahisi
hata kidogo. Ni lazima mwalimu ajitolee kabisa. Hata hivyo, licha ya magumu,
naona ualimu kuwa kazi yenye kuridhisha kuliko kazi yoyote ya kibiashara.”
Walimu wanaweza kulemewa na matatizo katika shule
zilizopo mijini kutokana na kukithiri kwa vitendo viovu vinavyotokana na
ukosefu wa maadili ikiwamo matumizi ya dawa za kulevya, uhalifu, na wazazi
wasiojali huathiri sana hali na nidhamu shuleni. Kutotii ni jambo la kawaida
katika maeneo hayo.
Kwa nini, basi, watu wengi huchagua kuwa walimu? Kuna
sababu mbalimbali za watu kuchagua kazi ya ualimu miongoni mwa hizo ni kuiga
mfano wa wazazi wao hasa ukizingatia mtoto wa Simba ni Simba na Wengine husukumwa na upendo kwa watoto.
Hata hivyo wakati wa maadhimisho haya ni vema
kukumbuka wajibu wa pande zote mbili kwa upande wa wazazi au walezi, na walimu
wenyewe.
Katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu
serikali imekuja na mkakati wa elimu bure kwa shule za umma kama ilivyainishwa
katika waraka wa elimu namba tatu wa mwaka 2016. Ambao pamoja na mambo mengine
umeondoa baadhi ya michango iliyokua ikitolewa na wazazi kusaidia upatikanaji
wa elimu kwa kundi kubwa la watanzania ambao bila mpango huo wangekosa nafasi
ya kupata elimu.
Jukumu la kuhakikisha mwanafunzi anapata elimu na sio
kuhudhuria shule tu ni la jamii nzima na sio la mwalimu pekee. Wajibu wa mzazi
sio tu kuhakikisha kuwa mwanafunzi anakula, anapata sare za shule daftari na
kalamu pekee.
Mzazi ana nafasi kubwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba
mwanafunzi au mwanae anahudhuria shule na anajifunza pia anakua na nidhamu ili
aweze kufanya vizuri katika masomo yake.
Wanafunzi wanapofanya vizuri katika masomo yao
hupongezwa sana na wazazi pamoja na serikali, lakini wanapofanya vibaya wazazi
huwanyooshea kidole walimu na kushindwa kujiuliza je wao walikua wapi? Je
wametimiza wajibu wao kama wazazi na walezi?
Alipata kuandika Mwalimu Nyerere kuwa "It takes a
village to raise a child" kwa tafsiri isiyo rasmi ni jukumu la jamii au
kijiji kumkuza mtoto.
Kwa upande wao walimu wanapaswa kuzingatia haya;
Fahamiana na wazazi. Kufanya hivyo si kupoteza wakati bali nyote mtanufaika.
Kutakupatia nafasi ya kuwasiliana na wale wanaoweza kukusaidia sana katika kazi
yako.
Mwalimu zungumza na mzazi kwa heshima, na usiongee
naye kana kwamba hajui chochote. Epuka kutumia usemi asioweza kuelewa.
Pia unapozungumzia watoto, kazia sifa zao nzuri.
Pongezi italeta matokeo mazuri kuliko shutuma. Eleza kile ambacho wazazi
wanaweza kufanya ili kumsaidia mtoto kufaulu.
Acha wazazi wajieleze, kisha usikilize kwa makini na elewa
hali ya nyumbani ya mtoto. Ikiwezekana, watembelee nyumbani. Panga tarehe ya
mazungumzo ya wakati ujao. Kufuatilia mazungumzo ni muhimu. Kunaonyesha kwamba
unajali kwelikweli.
Kumbuka mwalimu bora ni rafiki wa wanafunzi
anaowafundisha, kutokana na urafiki huu wanafunzi wanakua huru kumweleza
matatizo yao pasipo kumwogopa, watamwona ni rafiki na sio adui hivyo watakua
naye karibu zaidi na hali hii itamfanya mwalimu kutambua udhaifu wa kila
mwanafunzi na kumsaidia kama yeye.
Lakini kama mwalimu hatakua rafiki, basi ni vigumu
kumtambua mwanafunzi udhaifu wake na kumsaidia, pia mwalimu atakua kama adui
kwa wanafunzi.
Aidha kumwadhibu mwanafunzi iwe ni hatua ya mwisho
kabisa ya maamuzi katika kumsaidia. Kumkosoa mwanafunzi wakati anaendelea na
kutoa maelezo wakati wa kujifunza ni makosa bali subili amalize,ndipo umweleze
kilicho sahihi. Msaidie mwanafunzi kuelewa na siyo kukariri.
0 Comments:
Post a Comment