SEPTEMBA
23 ya kila mwaka ni maadhimisho ya Lugha za Ishara au Lugha za Alama. Lugha
hizi zimejikita katika miendo ya mikono, uso, kichwa, mabega na pia sehemu
nzima ya juu ya mwili badala ya kuhusisha sauti. Jambo la muhimu katika lugha
za alama ni lazima zionekane kwa sababu hazisikiki. Lugha hizi sio kwa kila mtu
bali hutumiwa hasa na watu viziwi, lakini vilevile wanaosikia wanaweza
kujifunza hizo.
Unajua
kuwa takribani watu milioni 72 duniani kote ni wenye usikivu hafifu (viziwi)?
Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Shirikisho la Wenye Usikivu Hafifu na linasema
kuwa watu hao wanatumia zaidi ya alama 300. Watu wengi wamekuwa wakishindwa
kufahamu kuwa matumizi ya lugha za alama kuwa ni jambo la asili ambalo lina
mfumo wake ambao upo tofauti na lugha nyingine.
Historia
ya Lugha za Alama imetoka mbali. Haijafahamika idadi ya lugha hizi duniani
kote, lakini kwa ujumla ni kwamba kila nchi ina aina yake ya lugha ya asili ya
alama. Baadhi ya nchi duniani zina lugha za alama zaidi ya moja. Unaweza
kujiuliza ni lini lugha hizi zilianza rasmi kutumika.
Katika
historia ya ulimwengu lugha hizo zimekuwa zikitumika na kundi la watu wenye
usikivu hafifu (viziwi). Mojawapo ya maandishi ya kwanza kurekodiwa kuhusu
lugha za alama ilikuwa katika karne ya 5 K.K katika kitabu cha mwanafalsafa wa
Ugiriki aliyefahamika kwa jina la Plato kinachoitwa Cratylus.
Katika
kitabu hicho Cratylus na Hermogenes wanamfuata Socrates ambaye alikuwa mwalimu
na rafiki mkubwa wa Plato katika mdahalo wao kuhusu lugha.
Socrates
aliwahi kusema kuhusu lugha za alama, “Kama tusingekuwa na sauti au ulimi na
tukawa tunataka kuzungumzia vitu fulani kwa mtu mwingine, tungeweza kujaribu
kutumia alama kwa kuichezesha mikono yetu, vichwa vyetu na maeneo mengine
katika miili yetu, si ndio watu wasioweza kuzungumza (bubu) wanavyofanya?
Hakuna
historia kubwa sana kuhusu lugha za alama mwishoni mwa karne ya 19, taarifa
nyingi kuhusu matumizi ya lugha za alama yanaonekana zaidi kabla ya karne ya 19
ambapo shule ya kwanza kwa watoto kuanzishwa duniani ya lugha za alama
ilianzishwa pale jijini Paris. Ilianzishwa na Abbé de l’Épée na hiyo ilikuwa
mwaka 1755 huku miongoni mwa wahitimu wa shule hiyo alikuwa ni Laurent Clerc
(1785-1895).
Clerc
alipoondoka katika shule hiyo, alikwenda nchini Marekani na kutoa hamasa ya
kuanzishwa kwa shule ya lugha za alama maalum kwa viziwi ambapo mnamo mwaka 1817
ilipofunguliwa shule hiyo na Thomas Hopkins Gallaudet. Na unaweza kusema shule
hiyo iliyofunguliwa huko West Hartford, Connecticut ambayo kwa sasa inaonekana
kuwa na wanafunzi wengi wa nchini humo zaidi ya 100 wanasoma siku za leo.
Nchini
Tanzania juhudi zimekuwa zikifanywa na mtu mmoja mmoja, taasisi zisizo za
kiserikali na serikali yenyewe lakini
kubwa zaidi ni pale ambapo wakati wa taarifa za habari katika runinga
mbalimbali kumekuwa na wakalimani wa taarifa hizo kwa lugha ya alama lakini
swali la msingi je, ambao hatuna changamoto ya usikivu hafifu tuna uelewa na
lugha hizo. Jibu ni rahisi tu asilimia kubwa hatuna uelewa na lugha za alama
hivyo huwa tunatazama kama picha tu zinazotembea.
Sasa
basi kutokana na kuwa na muundo tofauti na lugha nyingine hususani lugha hizi
zinazozungumzwa, lugha za alama zinatakiwa kupewa uzito wa hali ya juu na
umuhimu katika jamii.
Changizo
kwa ajili ya taasisi zinazojitoa kusaidia watu wenye changamoto ya usikivu
hafifu ni jambo la msingi ambalo jamii inapaswa kuliona na kulifanya. Pia taasisi au watu wenye ufahamu wa lugha za
alama wanapaswa kujitolea kuifundisha jamii kwani viziwi tunakaa nao kwenye
jamii zetu ambao wana haki na wajibu sawa kama mtu mwingine.
Kwa
sasa matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa makubwa hivyo ni vema kuchukua
fursa hiyo kwa wale wanaofahamu lugha hizo kuwafundisha wasiojua ambao hawana
matatizo ya usikivu hafifu na wakishapata elimu hiyo wataweza kuisambaza kwa
urahisi kwa watu wenye changamoto hiyo.
0 Comments:
Post a Comment