Monday, September 28, 2020

Klabu ya Waandishi wa Habari Kilimanjaro yapata viongozi wapya, Nyakiraria atetea nafasi yake

Viongozi wa Chama Cha Waandishi wa Habari mkoa wa Kilimanjaro (MECKI), wametakiwa kutumia nafasi zao  kwa  uaminifu, huku wakishirikiana katika kutatua changamoto za Wanahabari  kwa kuwaunganisha pamoja,  sambamba na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuiendeleza Klabu hiyo.

Ushauri huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Enos Masanja, wakati alipokuwa akitangaza matokeo ya uchaguzi kwa viongozi walioshinda katika nafasi mbalimbli za uongozi, uchaguzi uliofanyika katika kumbi wa Mkuu wa mkoa huo.

“Niwaombe sana viongozi mliochaguliwa kuiongoza Klabu hii kwa vipindi vya miaka mitano, nendeni mkashirikiane katika kutatua changamoto za wanahabari kwa kuwaunganisha pamoja na kuwa na vyanzo vipya vya mapato ndani ya klabu ili iweze kujiendesha na kuacha kutegemea wafadhili,”alisema Masanja.

Pia Msimamizi huyo wa uchaguzi, alimtangaza mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu hiyo kuwa ni Bahati Nyakiraria, aliyepata kura 29 dhidi ya kura 7 alizopata mshindani wake Dixson Busagaga.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilichukuliwa na Grace Munuo, aliyepata kura za Ndiyo 34 huku kura tatu akipata za Hapana.

Katika nafasi ya Katibu Nakajumo James alitetea nafasi yake kwa kupata kura  za ndiyo 35  ambapo kura 2 za hapana.

Nafasi ya Katibu Msaidizi ilichukuliwa na Deo Mosha, aliyejishindia kwa kupata kura 20 huku mshindani wake Omary Mlekwa akipata kura 17.

Pia katika uchaguzi huo Mweka Hazina wa klabu hiyo alichaguliwa Lucy Ollomi aliyepata kura 19 ambapo mshindani wake Upendo Mosha akipata kura 15.

Aidha Mwenyekiti wa Kamati hiyo aliwatangaza Wajumbe waliochanguliwa katika mkutano huo mkuu wa uchaguzi wa (MECKI), kuwa ni Zephania Renatus, Rosemary Ngoda, Edwin Lamtei, Sia Lyimo, Salma Shaban na Mary Mosha.

Akiwashukuru wanachama wa Klabu hiyo, kwa kuendelea kumuamini tena kuwaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano Mwenyekiti huyo Bahati Nyakiraria, aliwataka wanachama wa klabu hiyo kuiona klabu hiyo kama mali yao, hivyo wana kila sababu ya kutazama mwelekeo wa viongozi wao.




0 Comments:

Post a Comment