Wednesday, June 3, 2020

Nani atamfunga Paka kengele?

Tangu zamani Paka na Panya walikuwa maadui wakubwa. Paka hupenda kula Panya. Hadi leo Panya akimuona Paka hukimbia ili asikamatwe.

Siku moja Mfalme wa Panya aliwaita Panya wote ili watafute  njia ya kumshinda adui yao. Mkutano ulifanyika chini ya mti mkubwa nyumbani kwa mfalme. Uso wa mfalme ulionyesha huzuni kubwa.

Alipoona kuwa Panya wengi wamekwishafika, alisimama akasema, “Kwa kuwa Panya wengi wameshafika, tunawez akuanza mkutano. Hatuwezo kuwasubiri wenzetu ambao hatujui kama wako hai au wameliwa na Paka.”  Panya wakaitikia kwa kutikisa vichwa vyao.

Panya mmoja akasema, “Ni kweli Mfalme wetu. Hata mimi nimefika hapa kwa bahati tu. Njiani nilikutana na Paka. Alinifukuza sana. Niliingia shimo la Panya mweusi nikawakuta watoto wake tu. Panya mweusi alikuwa hajarudi nyumbani kwake tangu alipoondoka jana. Inawezekana kuwa ameuawa.” Panya wote walisikitishwa na habari ile.

Walikaa kimya kwa muda. Mfalme wao akasema, “Nimepata habari kuwa Panya mweupe, mkewe na watoto jana mchana wameuawa. Waliuawa walipokuwa wanatoka shambani. Panya mwekundu pia alijeruhiwa vibaya sana jana. Sijui kama atapona.”

Panya waliendelea kuzungumza kwa muda mfupi ndipo Mfalme wao akasema, “Sisi sote tumeona jinsi Paka anavyotukamata na kutuua. Sasa tufanye nini?.” Walianza mazungumzo kati yao yalikuwa hivi.

Panya Mabaka:       Nadhani sasa ni lazima tumuue Paka kama inabidi tuishi kwa raha.

Panya wote:            Ni kweli ni lazima tumuue Paka! Lazima Paka afe!

Mfalme:                    Hata mimi nakubaliana na ninyi. Lakini tutamuuaje huyu adui?

Paka Majivu:            Si rahisi kumuua Paka. Mimi ninashauri kwamba tumfunge Paka kengele shingoni. Akipita tutasikia sauti ya kengele kwa hiyo tutakimbia.          

Panya wote:            (Wanashangilia) Ni kweli! Tumfunge Paka kengele!

Mfalme:                    Sikilizeni! Sikilizeni sasa! Sote tunakubaliana kuwa tutamfunga Paka kengele?

Panya wote:            Ndiooo! Tumfunge Paka kengele!

Panya Majivu:         Vile vile mwenzetu akikamatwa na Paka, sote twende kumuokoa.

Panya Mjanja:         Haya ni mawazo mazuri, lakini nani atamfunga Paka kengele?

Panya wote wakanyamaza kimya kwa muda mfupi. Baadaye Panya Mabaka akasema, “Mimi simuogopi Paka. Najua la kufanya. Nitafunga kamba ya kengele kwenye kijiti kirefu kisha nitaitupa kengele hiyo shingoni mwaka.” Panya wote walifurahi na kushangilia.

Kumbe Paka alikuwa amekaa kimya juu yaule mti akiwasikiliza. Mara Paka akaruka na kumkamata Panya Mabaka. Panya wengine wote wakakimbilia kwenye mashimo. Panya Mabaka alipokamatwa aliita kwa sauti, “Mfalme! Nisaidieni! Tulikubaliana tusaidiane! Mbona sasa mnaniacha peke yangu? Nakufa! Jamani nakufa!”  

Panya wengi walitokeza vichwa vyao nje ya mashimo, lakini hawakwenda kumsaidia Panya Mabaka. Baadaye kidogo, Mfalme wa Panya alitokeza kichwa nje ya shimo akasema kwa haraka, “Mkutano umefungwa mpaka siku nyingine.” Kisha akarudi shimoni haraka. Panya mabaka akaliwa pale pale chini ya mti.


0 Comments:

Post a Comment