Monday, June 22, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Muhammad Ahmad bin Abd Allah ni nani?

Juni 22, 1885 alifariki dunia kiongozi wa kidini wa Kinubia nchini Sudan Muhammad Ahmad. Jina lake halisi ni Muhammad Ahmad bin Abd Allah.

Miezi sita baada ya kuiteka Khartoum, Muhammad Ahmad alifariki dunia kwa homa iliyosababishwa na kung’atwa na viroboto.

Vipele vilijitokeza mwili mzima na kifua kubana. Alizikwa mjini Omdurman karibu na magofu ya Khartoum na wafuasi wake waliteua watu watatu ambao walikuwa wasaidizi wake kuchukua mahali pake.

Alizaliwa Agosti 12, 1844 alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 40. Kiongozi huyo alikuwa kijana, mwamini wa orthodoksi na msomi wa tafsiri ya imani ya Kiislam. Juni 29, 1881 alitangazwa na wafuasi wake kuwa ni Mahdi (mkombozi wa dini ya Kiislam).

Kutangazwa kuwa Mahdi kulitokea katika kipindi ambacho idadi kubwa ya Wasudan walikuwa chini ya sera za ukandamizaji kutoka kwa watawala wa Dola la Ottoman (Turco-Egyptians) na pia walikuwa wakiungwa mkono na baadhi ya watu wa imani ya Kiislam katika ardhi hiyo ya Sudan.

Ahmad aliongoza vita dhidi ya Jeshi la Ottoman lililokuwa Misri na pia alipata ushindi mkubwa dhidi ya Waingereza.

Pia aliongeza eneo la kiutawala kutoka Bahari ya Shamu hadi Afrika ya Kati. Ahmad alianzisha vuguvugu ambalo lilisalia kama nukta muhimu kwa karne iliyofuata katika ardhi ya Sudan. Kutokana na tangazo lake la Mahdiyya mnamo Juni 1881 hadi 1898 maandiko mengi ya kitheolojia na kisiasa ya Ki-Mahidyya yalianzishwa na kuingizwa kwa wafuasi wake (Ansar).

Baada ya kifo chake ambacho hakikutarajiwa mnamo Juni 22, 1885  msaidizi wake Abdallahi ibn Muhammad alikalia mahali pake na kuliongoza taifa hilo dhidi ya uonevu wa Utawala wa Ottoman katika ardhi hiyo (Sudanese Mahdiyya).

Hata baada ya ukoloni bado Mahdi wanasalia kuwa alama muhimu nchini Sudan. Uzao wa kizazi cha Ahmad ulionekana tena wakati ambapo Sadiq al-Mahdi aliposhika mara mbili kuwa Waziri Mkuu wa Sudan 1966–1967 na 1986–1989 na kuweka sera za kidemokrasia katika taifa hilo.

0 Comments:

Post a Comment