Juni 12, 1525 msomi, mwanazuoni, mchungaji, mtunzi wa nyimbo
na mtumishi wa Kanisa wa Kijerumani Martin Luther alimwoa Katharina von Bora kinyume
na taratibu za Kanisa la Roman Katoliki kwa watumishi wake.
Luther ambaye anachukuliwa kuwa kiungo muhimu katika
kuanzisha Uprotestanti barani Ulaya. Luther alimwoa mwanamke huyo baada ya
kumsaidia kutoka katika jengo la utawa alimokuwa akiishi kupitia katika mfereji
na kumtotorosha hadi Wittenberg hivyo kuwa Mrs Martin Luther.
Katharina alizaliwa mnamo mwaka 1499 akiwa ni mtoto wa mtu
mashuhuri. Mnamo mwaka 1504 Katharina alienda shule ya Watawa wa Benedikti huko
Brehna karibu na Halle. Pia aliingia tena mnamo mwaka 1508 huko Nimbschen
karibu na Grimma. Mnamo mwaka 1515 Katharina alikuala kiapo na kuwa mtawa wa
Kanisa. Mnamo mwaka 1523 aliachana na utawa huo.
Kipindi wakati anaolewa Katharina kilikuwa kipindi ambacho
watumishi wa zamani wa kanisa barani Ulaya walikuwa wakioa na kuolewa.
Katharina wakati anaolewa na Luther alikuwa mdogo kwa miaka 16 na wawili hao
walibahatika kupata watoto sita.
Luther aliacha alama kwa familia yake kubwa lakini aliweza pia
kufanya starehe za maisha, kutunza bustani, utunzi wa nyimbo (muziki). Katharina
alichukua majukumu yote ya familia ikiwamo kazi za ndani na alimshauri Luther
asiajili wafanyakazi wa ndani kwa ajili ya utunzaji wa familia yake hali ambayo
ilimpa heshima ya kuwa mwanamke mwenye heshima na anayejua majukumu yake pia
hakuacha kutunza bustani.
Luther pia aliwatunza wanafunzi nyumbani kwake waliokuwa na hali
mbaya ya kifedha katika familia zao. Katika familia ya wawili hawa walikuwa pia
wafugaji wa mbwa kwani walikuwa na mbwa wao na chakula chao walitegemea zaidi
katika bustani waliyolima huko Black Cloister na baadaye walipata shamba nje kidogo
ya Wittenberg.
Luther na Katharina walikuwa wazazi wenye bidii, wakiwaadhibu
watoto wao, lakini wakifanya hivyo kwa upendo. Nyumba yao ilijulikana kutokana
na muundo wa maisha waliutengeneza maisha yenye furaha yake. Katharina
alifariki dunia mnamo Desemba 20, 1552 huko Torgau wakati akikimbia maambukizi
ya ugonjwa wa tauni huko Wittenberg.
Luther alikuwa akichukuliwa kuwa kiungo muhimu katika kutoa
changamoto katika Ukristo wa Magharibi katika karne ya 16 barani Ulaya. Changamoto
hiyo ilisababisha masuala ya dini na siasa kwa kanisa la Roman Katoliki kuwa
katika wakati mgumu pia mamlaka ya Papa katika kanisa Katoliki yalikuwa katika
changamoto hiyo.
Luther alichapisha mawazo yake 95 mnamo mwaka 1517 na kupitia
hapo ndipo mtafaruku ulipozidi katika kisiasa na kidini katika Kanisa la Roman
Katoliki. Licha ya Luther kutoa chapiso lake hilo lenye mambo 95 lakini hakuwa ameligawa kanisa Katoliki hadi
ilipofika mwaka 1521 wakati ambao mtawala wa Dola ya Rumi Charles V
alipotangaza kwamba Luther achukuliwe kama mkaidi na msaliti na asiwepo yeyote
wa kufuata aliyoyaandika.
Kwa kuanza Charles V alitangaza kufuta uraia wake katika dola
la Rumi. Mkutano huo ulifanyika katika
Bustani ya Heylshof kwenye mji wa Worms ambao upo umbali wa kilometa 60
Kusini-Kusini Magharibi ya Frankfurt na baadaye katika miji mingine iliyokuwa
ikijitawala katika dola la Rumi. Charles V aliendesha mkutano huo kumhusu
Luther na matokeo ya kuibuka kwa Uprotestanti barani Ulaya kutoka Januari 28
hadi Mei 25 mwaka 1521.
Alizaliwa Novemba 10, 1483 huko Eisleben, nchini Ujerumani
wakati huo ikiwa katika dola la Kirumi. Luther aliingia katika utumishi wa
Kanisa mnamo mwaka 1507. Akiwa na kanisa la Roman Katoliki alipinga mafundisho
mbalimbali ya kanisa hilo pia adhabu zilizokuwa zikitolewa kwa yeyote aliyekuwa
akitenda dhambi.
0 Comments:
Post a Comment