Juni 8, 1998 alifariki dunia
Rais wa kumi wa Nigeria Jenerali Sani Abacha. Kiongozi huyo wa kijeshi
alipoteza maisha ghafla kwenye Ikulu yake mjini Abuja.
Taarifa ya serikali ilieleza
kwamba Abacha alikufa kwa shambulio la moyo, lakini ripoti ya uchunguzi ya
gazeti la NewYork Times iliyochapwa Julai 11, mwaka 1998 ilieleza kuwa huenda
Abacha aliuawa kwa sumu na makahaba aliokuwa amewakodi kutoka Dubai ili kwenda
kumburudisha.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa
makahaba hao huenda walikuwa makachero wa shirika la ujasusi la Marekani (CIA)
lakini Abacha hakugundua. Usiku wa kuamkia Juni 8, 1998 Abacha alikesha na
makahaba hao wawili wakilewa, kuogelea na kucheza mziki katika Ikulu ya nchi
hiyo. Majira ya saa 10 alfajiri Abacha alidai kutojisikia vizuri na kwenda
kupumzika, na ilipofika saa 12 asubuhi alifariki dunia.
Baada ya kifo chake,
yaliibuka madai mbalimbali ya ubadhirifu wa mali na matumizi mabaya ya fedha.
Ilibainika kwamba licha ya Abacha kulalamikia matajiri kuhujumu rasilimali za
taifa hilo, na kujifanya yeye ni Rais wa wanyonge, lakini alitumia nafasi yake
kujilimbikizia mali na kuifilisi nchi. Familia ya Abacha ilikutwa na dola bilioni
tano (karibu trilioni 12 za Tanzania) zikiwa kwenye akaunti mbalimbali nje ya
nchi hasa Ulaya na Marekani.
Uchunguzi wa kimataifa ulionesha
kuwa jina la Abacha lilitumika mara 419 kuidhinisha malipo na kuchukua pesa
kutoka makampuni makubwa nchini humo kwa ajili ya familia yake. Ndugu zake
walipotaka fedha aliwaandikia 'memo' kwenda benki kuu au kwenye makampuni
makubwa ya kuchimba mafuta na kupewa kiasi walichotaka.
Katika utawala wake mkono wa
chuma ulikwenda hadi kwa waandishi wa habari, makala na vitabu. Mwanafasihi
mkongwe na mwenye heshima kubwa barani Afrika, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya
Nobel, Wole Soyinka aliponea chupuchupu kuuawa na serikali ya Abacha mwaka
1997. November 16 mwaka 1997, Abacha alitangaza Wole Soyinka akamatwe, lakini
alitoroka kwa baiskeli kwa kupitia njia za ‘panya’ hadi Benin, ambapo alipanda
ndege kwenda Marekani na kupata hifadhi ya kisiasa. Hata hivyo Abacha alisaini
hati ya adhabu ya kifo kwa Wole Soyinka licha ya kutokuwepo Nigeria.
Pia Abacha alishughulika na
yeyote aliyekosoa utawala wake hata kama ni kwa nia njema. Aliagiza kunyongwa
kwa mwanaharakati wa mazingira kutoka jamii ya Ogoni, Ken Saro-Wiwa, baada ya
kuanzisha kampeni ya kupinga uharibifu wa mazingira uliokuwa ukifanywa na
makampuni ya kuchimba mafuta kwenye eneo lao. Saro-Wiwa aliuawa November 10
mwaka 1995 kwa agizo la Abacha. Mauaji yake yalichochea hasira kutoka mataifa
mbalimbali na kusabisha Nigeria kufutiwa uanachama wa Jumuiya ya Madola kwa
miaka mitatu.
Abacha aliingia madarakani
Novemba 17 mwaka 1993, baada ya kumpindua aliyekuwa Rais wa mpito Ernest
Shonekan. Kabla ya mapinduzi hayo Shonekan alikuwa amekaa madarakani kwa miezi
mitatu tu baada ya kujiuzulu kwa Jenerali Ibrahim Babangida.
Baada ya kuingia madarakani
Abacha alianza kulalamika kuwa tawala zilizopita hasa ya Babangida iliharibu
nchi na kuzorotesha maendeleo ya taifa hilo. Aliahidi kufufua njia kuu za
uchumi, kujenga viwanda, kuboresha ufanisi katika sekta binafsi na na kuogeza
wigo wa ajira kwa vijana.
Alifariki dunia akiwa na
umri wa miaka 54. Alizaliwa Kano, Nigeria mnamo Septemba 20, 1943. Aliingia
jeshini na kupata mafunzo ya kijeshi nchini humo na vyuo vya kijeshi vya
Uingereza. Alipanda katika vyeo vya kijeshi na mnamo mwaka 1983 alipata cheo
cha Ubrigedia pale alipomsaidia Jenerali Ibrahim Babangida kumpindua Shehu Shagari
aliyechaguliwa katika awamu ya pili ya Urais mnamo mwaka 1983. Muhammad Buhari
akawa kiongozi wa Nigeria hata hivyo miaka miwili baadaye Babangida alimpindua
Buhari na kujitangazia kuwa Rais na kamanda wake akawa Abacha.
0 Comments:
Post a Comment