Hali
ya utulivu katika klabu ya michezo ya Moshi mkoani Kilimanjaro maarufu Moshi
Club inaweza kutoweka kutokana na sintofahamu inayoendelea katika kitengo cha
mpira wa miguu baina ya wanachama kutokana na mtifuano kuhusu nani mwenye haki
ya kuutumia uwanja wa mpira wa miguu.
Hayo
yanajiri baada ya wanachama wa Moshi Veterans Club (MVC) kutifuana na wale
waliojiengua wanaofahamika kama Uhuru Veterans kwa kile kinachodaiwa na kila
upande una haki ya kuutumia uwanja wa mpira wa miguu.
Mtifuano
huo umeenda mbali zaidi na kusababisha mara kadhaa mazoezi kusimama kutokana na
uwepo wa timu mbili ndani ya uwanja mmoja ambapo kila upande unadai kuwa una
haki ya kuutumia hali ambayo imepelekea kauli za vitisho kutoka kwa maveterani
hao.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima wanachama hao wa Moshi Club walidai
walipofikia sasa ni pabaya kutokana na kauli za ubabe na vitisho zinazotolewa
na kila upande ikiwamo kutishiana kupasua mipira, kutembea na vitu vyenye ncha
kali.
Mwenyekiti
wa Maveterani wa Uhuru Robert Saturine alisema wao ni wanachama halali ambao
wamelipa stahiki zote za kuwa wanachama wa Moshi Club hivyo wana uhuru kama
jina lao lilivyo la kutumia uwanja huo kwa ajili ya shughuli za kimichezo
hususani mpira wa miguu.
“Sisi
tuna haki ya kutumia uwanja huu na ndio maana tupo hapa, tumelipa ada kama
wanachama wengine,” alisema Saturine.
Alipoulizwa
kuhusu kufikiwa kwa maridhiano baina ya pande mbili alisema kuwa ni vema
wakaketi kitako kujadili suala hilo kwa pamoja badala ya kutupia vijembe na
maneno licha ya kuendelea kusimamia msimamo wao wa kuwa na haki ya kuutumia
uwanja huo.
Kwa
upande wake Katibu wa Moshi Veterans Moses Chalamila alisema kinachofanyika
sasa ni ubishi wa hao waliojiengua kwani kuwa mwanachama wa Moshi Club hakutoi
nafasi ya moja kwa moja kkwa mwanachama kufanya kila kitu anavyojitakiwa kwani
kuna utaratibu kwenye kila kitengo ambapo mwanachama husika atapaswa kuufuata.
“Ukishalipa
laki moja ambayo ndio ada ya uanachama wa hapa Moshi Club hakutoi nafasi ya
mwanachama kufanya kila kitu, kila kitengo kama gofu, tenisi, football ukiingia
kuna utaratibu ambao mtu atatakiwa aufuate ili aweze kuishi na wenzake katika
kitengo husika, sasa wanachokifanya hao (Uhuru) ni ubishi na ubabe jambo ambalo
si jema,” alisema Chalamila.
Hata
hivyo Meneja wa Moshi Club Michael Mtenga alisema jambo hilo analifahamu lakini
hataweza kulizungumzia kwasababu yupo kwenye msiba akirudi ndio atafafanua kwa
kina kuhusu sintofahamu hiyo.
Chokochoko
za pande hizo zilianza kujitokeza mwishoni mwa mwaka 2019 baada ya baadhi ya
wanachama kujiengua kutoka MVC na kuanzisha Uhuru Veterans kutokana na kushindwa
kukubaliana baadhi ya mambo hali ambayo imesababisha sintofahamu hiyo katika
kitengo hicho cha mpira wa miguu.
0 Comments:
Post a Comment