Monday, June 1, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Nkosi Johnson ni nani?

Juni 1, 2001 alifariki dunia mwanaharakati mtoto wa Afrika Kusini Nkosi Johnson. Mwanaharakati huyo alikuwa maarufu katika mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi. Nkosi alitoa ushawishi mkubwa duniani kabla ya kifo chake akiwa na umri wa miaka 12 kuhusu mtazamo kwa watu walioathirika na maradhi hayo. 

Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) lilimuweka katika nafasi ya tano kwenye orodha ya Watu Wakubwa nchini Afrika Kusini. Kabla ya kifo chake aliandika kitabu kinachoitwa, “Care for us and accept us”. 

Nkosi aliweka rekodi nyingine ya kuwa mtoto ambaye aliishi muda mrefu akiwa ameathirika kwa virusi vya Ukimwi  nchini Afrika Kusini. Rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini Nelson Mandela alimtaja Nkosi kuwa ni Nembo ya Mapambano ya Maisha. 

Nkosi alizaliwa kwa Nonthlanthla Daphne Nkosi karibu na kijiji cha Dannhauser mnamo Februari 4, 1989. Hakuwahi kumfahamu baba yake. Alizaliwa akiwa ameathirika kutokana na maradhi hayo. Nkosi aliasiliwa kisheria na msemaji wa Johannesburg Gail Johnson kutokana na mama yake kushindwa kumtunza. 

Nkosi alianza kufahamika zaidi mnamo mwaka 1997 pale ambapo shule ya msingi moja katika kitongoji cha Melville jijini Johannesburg ilipokataa kumpokea kutokana na kuwa na maradhi hayo. Hapo kuliibua hisia za wanaharakati wengi wa ubaguzi na serikali ndipo shule hiyo ilipokubali kumpokea. Akiwa na mama yake mlezi, Nkosi alitoa ushawishi mkubwa kuanzishwa kwa kambi ya watu walioathirika na maradhi hayo hususani kina mama na watoto ya Nkosi Haven jijini Johannesburg. 

Miaka minne baada ya kifo chake Gail aliwasilisha kwa urefu kumhusu Nkosi ambapo alitunukiwa tuzo ya Kimataifa ya Amani kwa Watoto ambayo aliipokea kutoka kwa Mikhail Gorbachev. Hatimaye Nkosi Haven ilipokea kiasi cha dola laki moja kutoka kwenye Mfuko wa KidsRights. Nkosi alizikwa katika makaburi ya Westpark jijini Johannesburg. 

Anakumbukwa sana Nkosi kutoka na hotuba yake kwenye Kongamano la 13 la Kimataifa la Ukimwi lililofanyika Durban, Afrika Kusini, mbele ya washiriki 12,000 Nkosi alihutubia hadhira hiyo kuhusu maradhi ya Ukimwi hatimaye alihitimisha kwa maneno haya, “Care for us and accept us – we are all human beings. We are normal. We have hands. We have feet. We can walk, we can talk, we have needs just like everyone else – don't be afraid of us – we are all the same!” 

0 Comments:

Post a Comment