Friday, June 26, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Nasir al-Din al-Tusi ni nani?

Juni 26, 1274 alifariki dunia msomi na mwanazuoni wa Kiajemi Nasir al-Din Al-Tusi. Jina lake halisi ni Khawaja Muhammad ibn Muhammad ibn Hasan Tūsī.

Amekuwa akichukuliwa kuwa ni msanifu, mwanafalsafa, mwanafizikia, mwanasayansi na mwanatheolojia wa Kiajemi.

Nasir al-Din alikuwa miongoni mwa wanasayansi wakubwa katika kipindi cha kati cha Uislam. Na amekuwa akichukuliwa kuwa ndiye mvumbuzi wa Trigonometriki katika masuala ya Hisabati.  

Nasir al-Din alifanya kazi 150, miongoni mwa hizo zipatazo 25 aliziandika kwa lugha ya kiajemi na zilizobaki ziliandikwa kwa lugha ya Kiarabu.

Pia kuna moja ambaye iliandikwa kwa lugha tatu ya Kiajemi, Kiarabu na Kituruki. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 huko Al Yassin Mosque, Baghdad, Iraq. Nasir al-Din alipendelea pia kutunga mashairi miongoni mwa mistari katika mashairi yake ni “Yeyote ambaye hajui, na kwamba hajui kuwa hajui ni wazi kwamba milele yote atakwama kwenye ujinga mara mbili.”

Mara kadhaa mchango wake umetambuliwa na wasomi mbalimbali ambapo katika mbalamwezi upande wa kusini kuna crater ambayo ina kipenyo cha kilometa 60, kwa heshima ya Nasir al-Din eneo hilo limetajwa kwa jina lake kama ‘Nasireddin’. 

Chuo kikuu cha Teknolojia cha K. N. Toosi nchini Iran kimetajwa kwa heshima yake.

Pia Observatory of Shamakhy huko Jamhuri ya Azerbaijan imetajwa kwa heshima yake. Nchini Iran kumbukizi ya kuzaliwa kwake imekuwa ikisheherekewa na kama Siku ya Mhandisi. Nasir al-Din alizaliwa Februari 18, 1201 huko Tus, katika jimbo la Khorasan karibu na Mashhad.

Huko Mashhad kuna sanamu ya Nasir al-Din kutokana na mchango wake katika sayansi, unajimu, kemia, fizikia na hisabati.

Alizaliwa katika familia ya Kishia, akiwa bado mdogo alimpoteza baba yake.  Kwa ajili ya kutimiza kile ambacho baba yake alimtaka afanye Nasir al-Din alianza kujifunza kwa bidii. Alisafiri maeneo mbalimbali akifuatilia masomo ya walimu na kujipatia maarifa.

Alikuwa akifanya kwa bidii zote huku akitiwa moyo na imani yake katika Uislamu. Akiwa na umri mdogo alienda zake kaskazini Mashariki ya Iran katika mji wa Nishapur, ambako alijifunza falsafa chini ya uangalizi wa Farid al-Din Damad na Hisabati chini ya mwalimu Muhammad Hasib.

Akiwa Nishapur alikutana na mkongwe wa Kisufi Abū Ḥamīd bin Abū Bakr Ibrāhīm maarufu Attar wa Nishapur ambaye alikuja kuuawa na Wamongolia waliovamia mji  huo. Akiwa hapo alihudhuria masomo ya Qutb al-Din al-Misri.

Mnamo mwaka 1242 alienda zake kaskazini mwa Iraq katika mji wa Mosul uliopo kaskazini ya Baghdad yapata kilometa 400 ambako alisomea Unajimu na Hesabu pamoja na Kamal al-Din Yunus, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Sharaf al-Dīn al-Muẓaffar. Baadaye alijumuika na mwanafalsafa wa Kisufi Sadr al-Din al-Qunawi.

Wakati huo wote jamii yao ilikuwa ikivamia sana na Wamongolia kutoka Mongolia na China.

Hata hivyo Nasir al-Din alifanikiwa kuweka mizizi yake na kuwa miongoni ya watu waliochangia pakubwa katika medani ya sayansi na falsafa.

0 Comments:

Post a Comment