Mapinduzi ya Viwandani
barani Ulaya yalijitokeza katika karne ya 18 hadi karne ya 19 ambapo yalitokea
mabadiliko makubwa katika kilimo, utengenezaji wa bidhaa, uchimbaji wa madini
na uchukuzi hali ambayo iliathiri kwa kiasi kikubwa uchumi, jamii na utamaduni
wa watu. Yalianzia Uingereza na hatimaye kuenea Ulaya nzima, Amerika ya
Kaskazini na mwishowe duniani kote.
Mwanzo wa Mapinduzi ya
viwanda ulidokeza mabadiliko muhimu katika historia ya binadamu; karibu kila
kipengele cha maisha ya kila siku hatimaye kiliathirika kwa njia fulani. Katika
siasa za mataifa barani humo kuliongeza uhitaji wa mali ghafi kwa ajili ya
viwanda hali iliyosababisha mataifa mbalimbali kutanua himaya zao. Miongoni mwa
himaya iliyofikiwa ilikuwa ni Afrika.
Waingereza, Wareno,
Wafaransa na Wajerumani walijikuta wakitafuta maeno ya kumiliki ili waweze
kuendesha viwanda vyao na wakafanikiwa kwa kiasi kikubwa kumiliki. Walipofika
walijikuta wakigongana wenyewe kwa wenyewe hali iliyowafanya wakae chini na
kukubaliana kumiliki kwa mipaka.
Wakati wazungu
wanagawana bara la Afrika kupitia Mkutano Mkuu wa Berlin mnamo mwaka 1884, Otto
Van Bismarck ndiye aliyesimamia mkutano huo. Tanganyika ilichukuliwa na
Wajerumani waliotawala hadi walipopigwa laza na Waingereza 1918.
Wajerumani walipokuja
walikuta baadhi ya maeneo kuna tawala zenye nguvu, zilizokua na mfumo rasmi wa
uongozi. Wao waliziita tawala za jadi.
Moja ya tawala
iliyokua na nguvu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ni dola ya wachaga.
Zilikuwepo nyingine zenye nguvu kama Himaya ya Sultani wa Zanzibar, dola ya
Buganda, Wanyamwezi, Wangoni, Wahaya, Wahutu, Watutsi, Wahehe n.k
Wachaga walikuwapo
pembezoni mwa mlima Kilimanjaro kuanzia maeneo ya Rongai hadi Siha.
Eneo hili lilikua na
mtawala mkuu mmoja (aliyeitwa Mangi Mkuu). Huyu alikuwa kama Rais ama Mfalme wa
jamii hiyo.
Chini yake walikuwepo
watawala wakuu wawakilishi wa majimbo. Hawa waliitwa 'Mangi Waitori'. Chini yao
walikuwepo watawala wa wa maeneo madogo, hawa waliitwa Mangi kama vile Mangi
Meli wa Old Moshi, Mangi Sina wa Kibosho, Mangi Salakana wa Useri.
Kwa mfano eneo kama
Rombo lilikuwa na Mangi wengi. Alikuwepo Mangi wa Keni, Mangi wa Mashati, Mangi
wa Mengwe. Lakini wote waliunganishwa na Mangi Mwitori wa Rombo. Vivyo hivyo
katika maeneo mengine kama Kibosho, Machame, Siha, Old Moshi na Marangu.
MANGI MELI AWATISHA WAJERUMANI
Baada ya Ujerumani
kuingia Tanganyika, upande wa kaskazini wa Koloni lao la Afrika ya Mashariki,
walikuwepo Wachaga nao, chini ya Mangi Meli wa Moshi, walikataa katakata
kutawaliwa na Wajerumani.
Katika jitihada za
kuwaweka kwenye umiliki wao, serikali ya kikoloni ya Wajerumani ilipeleka jeshi
la askari mkoani Kilimanjaro, lililoongozwa na Von Bulow akisaidiwa na Luteni
Wolfrum.
Juni 1892 Jeshi hilo
la Wajerumani lilishambuliwa na askari wa Mangi Meli waliolizingira kwa ghafla
kutoka maoteoni ndani ya siku mbili walichemsha na Mangi Meli akaibuka mshindi.
Von Bulow,
Luteni Wolfrum pamoja na askari wengi wa Wajerumani waliuawa. Askari wa
Kijerumani walionusurika walirudi haraka Marangu, mahali ambapo makao yao makuu
yalikuwa yamehamishiwa.
Mangi Meli alikuwa na
kamanda wake aliyefahamika kwa jina la Ndaskoi Msehiye Massamu ambaye alikuwa
akiwaongoza wachagga kuvamia na kuteka mifugo katika milima ya Upareni na
Taveta nchini Kenya.
Ndaskoi alikuwa
akiishi Masamunyi ambako alijenga huko na ndugu zake wengi walikuwa wakiishi
Msaranga, Old Moshi.
Agosti 1893 Wajerumani
hawakukubali kirahisi kwani waliamua kuazima askari kutoka Unubi huko Sudan na
wengine askari wa Kizulu kutoka Afrika Kusini ambao walipambana na Mangi Meli
nao wakamshinda kwa siku mbili.
Safari hii jeshi hilo
la Wajerumani lilitokea pwani kuelekea Kilimanjaro, liliongozwa na Gavana
mwenyewe Friedrich von Schele.
Baadhi ya Wamangi wa
Uchaggani waliokuwa na uhasama na walichomekea na akakamatwa huko Tsudunyi
akiwa na wafuasi wake 19 kisha kunyongwa. Kichwa chake kilikatwa na kupelekwa
Ujerumani hakijarudi hadi leo.
MNYAKA SURURU MBORO NI NANI?
Mnyaka Sururu Mboro ni
mwalimu wa Kichaga na mwanaharakati kutoka nchini Tanzania ambaye taarifa
zilizopo ni kwamba anaishi jijini Berlin, Ujerumani kwa takribani miaka 30
sasa.
Huyu ni miongoni mwa
waanzilishi wa asasi isiyo ya kiserikali ya Berlin Postkolonial e.V ambayo
imejikita katika kufanya utafiti kuhusu kumbukumbu mbalimbali za siri za
kihistoria zilizofichwa katika mji huo mkuu wa Ujerumani.
Katika suala ya
uanaharakati wake inaelezwa kwamba Mnyaka Sururu Mboro bado anaendelea
kupigania majina ya mitaa nchini Tanzania hususani katika ardhi ya Uchagani
kuwa na majina ya waafrika ambao waliwapinga wakoloni kukalia ardhi yao
kimabavu.
Chanzo kimoja kilisema
mwanaharakati huyu amekuwa akipambana kila kukicha kuhakikisha majina ya
kiafrika yanapewa nafasi katika mitaa ili hata kizazi kijacho kipate kutambua
uwepo wa waliopinga licha ya wengine kutofanikiwa.
Kazi yake mpaka sasa
nchini Ujerumani ambayo ni shauku ya Mnyaka Sururu Mboro ni kuhakikisha anarudi
nchini Tanzania akiwa na fuvu la Mangi Meli ambalo Wajerumani waliondoka nalo
baada ya kumaliza utawala wao nchini.
Msukumo wa Wajerumani
kupeleka mabaki ya watu wa Afrika ulipewa uzito na mwanaanthropolojia wa
Ujerumani Felix von Luschan mnamo mwaka 1899 ambaye alipeleka ujumbe wake
katika makoloni yaliyokaliwa na Ujerumani kupeleka mabaki hayo ili kusalia na
ushahidi wa kianthropolojia.
Zaidi ya mafuvu 6,300
yalikusanywa na kupelekwa nchini humo. Binafsi nashiwishika na maneno ya Balozi
wa Tanzania nchini Ujerumani Dkt. Abdallah Saleh Possi aliyoyasema mwaka 2018,
“Kwa mawazo yangu, unapozungumza kuhusu miili ya binadamu unazungumza kuhusu
utu wa mtu. Ni sawa na kusema ni kwa namna gani utu huo una umuhimu kwa
Tanzania. Huwezi kuchukua mwili wa mtu kwa ajili ya utafiti.”
Maneno hayo ya mguso
kuhusu utu wetu kama watanzania upo wapi na ndio sababu nauliza ni lini Mnyaka
Sururu Mboro atarudi na fuvu la Mangi Meli ambalo alijitolea kwenda kulifuata
huko Ujerumani. Pia serikali ya Ujerumani inatutazama vipi kwa sasa kama
iliweza kurudisha la Mkwawa tunahitaji shujaa mwingine Mangi Meli aweze kurudi
katika ardhi yetu ili tuweze kutunza kumbukumbu zetu na vizazi vyetu.
0 Comments:
Post a Comment