Diwani wa zamani wa kata ya Kibosho Magharibi Deogratius Mushi
amemtaka Mbunge wa zamani wa Moshi Vijijini Anthony Komu kuacha kutumia jina
lake kutafuta huruma za kurudi kwenye kinyang’anyiro cha ubunge baada ya
kutimuliwa kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Hayo yalijiri ikiwa ni siku chache baada ya Komu aliyetangaza
kuhamia NCCR-Mageuzi Machi mwaka huu baada ya Bunge kumalizika kuonyesha
wasiwasi mkubwa dhidi ya mgombea anayeonekana kutajwa kuwania jimbo hilo wa
Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na Tanzania Daima Mushi alisema Komu amefilisika
kisiasa hivyo asitumie kivuli chake kutafuta kura za huruma katika jimbo ambalo
ameshindwa kuwasaidia wananchi tangu alipotoa ahadi zake katika kampeni
zilizopita.
“Mimi mwaka 2019 niliachana na Chadema na wala sikushauriana na
Komu kuwa yeye awe msemaji wangu. CCM ni taasisi ambayo inaendeshwa kwa mfumo,
sharia, kanuni na taratibu za kumpata mgombea, Komu hajatekeleza ahadi kwa
wananchi wake. CCM hahitaji huruma za upinzani kushinda jimbo la Moshi
Vijijini,” alisema Mushi.
Mushi aliongeza kuwa yeye kama anayewania ubunge katika jimbo
hilo hategemei huruma za chama kumchagua kwani chama chake kina utaratibu wake
wa kupata wagombea wa nafasi mbalimbali.
“Vyama vya upinzani vimezoea kupeperusha bendera za watu na sio za
vyama kwa hiyo namtahadharisha Komu ajiandae kupambana na CCM zaidi kuliko
kujiandaa kupambana na mtu,kumnadi mgombea wa chama ni suala la wanachama
wenyewe na sio nje ya hapo,” aliongeza Mushi.
Katika uchaguzi wa mwaka 2015 Komu alishinda kiti cha ubunge wa
jimbo la Moshi Vijijini kwa kuzoa jumla ya kura 55,813, akifuatiwa kwa mbali na
mgombea wa CCM Dr. Cyril Chami ambaye pia alishawahi kuwa Waziri Viwanda na
Biashara aliyepata kura 24,415.
0 Comments:
Post a Comment