Juni 19, 1903 ambapo Benito Mussolini wakati huo akiwa
mwanamapinduzi wa Kisoshalisti alikamatwa na Polisi wa Bern huko Uswisi kwa
kuwa chanzo cha kuanzishwa kwa mgomo.
Mwanasiasa na mwandishi wa habari huyu wa Italia ambaye
baadaye alikuja kuwa kiongozi wa taifa la Italia kwa mabavu (1922-1945) alienda
nchini Uswisi kwa ajili ya kufanya kazi zake za uandishi wa habari.
Alikimbilia nchini Uswisi baada ya kugundua kwamba hali
haikuwa shwari nchini mwake kutokana na kubeba itikadi za kisoshalisti ambazo
kama kijana zilimkaa vilivyo.
Juni 1902 alikimbilia nchini Uswisi baada ya kutua katika
ardhi hiyo alifanya kazi kama mfyatua matofali na shughuli za ujenzi pia mwandishi
wa habari baadaye akajiunga na vyama vya kibiashara kuendeleza harakati zake.
Mussolini akiwa nchini Uswisi alikuwa imara katika vuguvugu
la Kisoshalisti wakati huo akifanya kazi na gazeti la L’Avvenire del Lavoratore, akiratibu mikutano, kutoa hotuba na kuhudumu
katika nafasi ya Katibu kwenye Chama cha Wafanyakazi wa Kiitaliano mjini
Lausanne.
Mnamo Juni 1903 alikamatwa na polisi kwa ajili ya ushauri
wake ambao ulisababisha vurugu kubwa. Mussolini alitupwa jela kwa majuma mawili
kisha akarudishwa nchini Italia lakini baadaye alirudi tena nchini Uswisi.
Aliporudi mnamo mwaka 1904 alikamatwa tena mjini Geneva
kutokana na kudanganya nyaraka zake hivyo ikabidi aende zake huko Lausanne
ambako alienda kusoma Chuo Kikuu katika Idara ya Sayansi ya Jamii baada ya
kupata ushauri mzuri na Vilfredo Pareto
ambaye alikuwa mhandisi wa Italia, mchumi, mwanasayansi, mwanasiasa na
mwanafalsafa.
Desemba 1904 alirudi nchini Italia ambako alijiunga na vikosi
vya jeshi vya Bersaglieri huko Forli.
Baada ya miaka miwili ya kuwapo jeshini kutoka Januari 1905 hadi Septemba 1906
alirudi zake kufundisha.
Baada ya kuondolewa jeshini, Mussolini aliandika na kuhariri
magazeti kadhaa ya kisoshaliti na alikuwa akichukuliwa kuwa ni nyota inayokuja
kwa kasi yenye mrengo wa kushoto nchini Italia.
Benito Mussolini alikuwa mtoto wa kiume wa Alessandro Mussolini
ambaye alikuwa mhunzi na mfanyabiashara wa zana za chuma pia mrengo wa kulia wa
itikadi za kisoshaliti na mpinzani wa Ukatoliki. Mama yake alikuwa mwalimu na
mwamini wa Ukatoliki asiyeyumba.
0 Comments:
Post a Comment