Monday, June 29, 2020

Lazarus Chakwera: Rais wa kwanza Mlokole nchini Malawi

Nchini Malawi kumeshuhudiwa Kiongozi wa chama cha upinzani cha Malawi Congress (MCP) Lazarus Chakwera, akiapishwa jana (Juni 28, 2020) kama rais mpya wa nchi hiyo baada ya kuibuka mshindi kwa asilimia 58.7 za kura.

Katika sherehe hiyo ya kuapishwa katika mji mkuu wa Lilongwe, Chakwera aliapa kufanya majukumu yake vyema, kuilinda na kuitetea katiba ya nchi hiyo. Chakwera pia alitoa hakikisho kwa wafuasi wa rais wa sasa aliyeshindwa katika uchaguzi huo Peter Mutharika kwamba hawapaswi kuwa na hofu na kwamba Malawi mpya ni nchi yao pia.

Tume ya uchaguzi nchini humo jana usiku ilimtangaza kiongozi huyo kuwa rais mteule wa sita wa taifa hilo baada ya kumshinda rais wa sasa Peter Mutharika wa chama cha Democratic Progressive Party.

Uchaguzi huo mpya uliandaliwa baada ya mahakama kuu nchini humo kufutilia mbali ushindi wa Mutharika katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2019 kutokana na dosari nyingi zilizobainika ikiwemo kutumika kwa wino wa kufanya marekebisho katika karatasi za matokeo. Juni 27, 2020 Mutharika aliutaja uchaguzi huo uliofanywa Juni 23 kuwa mbaya zaidi katika historia ya nchi hiyo.

LAZARUS CHAKWERA NI NANI? 

Jina lake halisi ni Lazarus McCarthy Chakwera. Alizaliwa Aprili 5, 1955 jijini Lilongwe ambao ni mji mkuu wa Malawi. Wakati huo taifa hilo lililikuwa mikononi mwa utawala wa Uingereza.

Familia yake ilikuwa ni ya wakulima katika viunga vya jiji hilo. Kaka zake wawili waliozaliwa kabla yake walifariki dunia wakiwa bado wadogo. Baba yake alipozaliwa mwanaye huyo akampa jina lake Lazarus (Lazaro) ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu kwa mujibu wa maandiko ya Biblia.

Baba yake hakuwa na tumaini tena kutokana na watoto wake kufariki dunia. Lazarus alimwoa Monica na wawili hao wamefanikiwa kuzaa watoto wanne na wana wajukuu. Chakwera ni mwanasiasa mbapo kabla hajaiingia katika siasa alikuwa mwanatheolojia.

Alikuwa kiongozi wa MCP tangu mwaka 2013 na zamani walikuwa kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa nguvu zote alipinga uchaguzi uliojawa na mkanganyiko wa Mei 21, 2019 ambao ulipigwa chini na Mahakama ya Katiba. Alikuwa Rais wa Kanisa la Malawi Assemblies of God kutoka mwaka 1989 hadi Mei 14, 2013.  

Alihitimu masomo ya Sanaa (Falsafa) katika Chuo Kikuu cha Malawi mnamo mwaka 1977. Alisoma masomo ya theolojia na kutunukiwa shahada yake katika Chuo Kikuu cha North nchini Afrika Kusini. Pia alipata shahada ya uzamili (MTh) katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini mnamo mwaka 1991.

Pia mnamo mwaka 2000 alitunukiwa shahada ya uzamivu nchini Marekani katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Trinity kilichopo Deerfield huko Illinois. Alitunukiwa Uprofesa katika Pan-Africa Theological Seminary mnamo mwaka 2005.

Chakwera aliwahi kuhudumu kama Mwalimu katika shule za Kitheolojia za Assembilies of God kutoka mwaka 1983 hadi 2000 ambako alikuja kuwa Principal mnamo mwaka 1996. Pia alikuwa instructor na lecturer katika All Nation Theological Seminary.

Tangu Aprili 14, 2013 aliustaajabisha ulimwenguni hususani kanisa lake la Assemblies of God  alipotangaza kwamba ataongoza upinzani nchini humo wakati huo akiwa Rais wa Assemblies of God hatimaye alifanikiwa na sasa ni Rais wa taifa la Malawi.

0 Comments:

Post a Comment